• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
GWIJI WA WIKI: Wangu Kanuri

GWIJI WA WIKI: Wangu Kanuri

Na CHRIS ADUNGO

Kuandika ninapenda, yatokayo aushini,

Kusimulia napenda, sikitiko la moyoni,

Kukariri ninapenda, asubuhi na jioni.

Niliandike shairi, niyakidhi yote haya.

KUFAULU katika maisha ni zao la nidhamu, bidii na stahamala.

Waandishi wengi chipukizi huwa na pupa ya kukata tamaa upesi. Uvumilivu ni sifa muhimu na ya lazima kwa mtu kuwa nayo ili afanikiwe katika kazi ngumu ya uandishi. Hata anapotunga, inamlazimu mwandishi ajikakamue na kusoma vitabu anuwai kwa sababu uandishi unahitaji utafiti mwingi wa mara kwa mara ambao si lazima uwe na uhusiano wa moja kwa moja na bahari unayopania kuizamia.

Yawezekana kitabu ulichokiandika kikose kukuletea natija yoyote hata baada ya kuchapishwa. Usivunjike moyo. Badala yake, endelea kuandika tena na tena ili upate uzoefu utakaochangia pakubwa makuzi ya kipawa chako. Sawa na ukulima, uandishi huhitaji subira tele ndipo uvune heri hatimaye.

Huu ndio ushauri wa Bi Wangu Kanuri – mwandishi chipukizi wa Kiswahili na mshairi shupavu ambaye kwa sasa anasomea taaluma ya Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Daystar, Athi River, Kaunti ya Machakos.

Maisha ya awali

Wangu alizaliwa mnamo Disemba 25, 1996, katika Kaunti ya Nyeri akiwa kitindamimba katika familia ya watoto wanne wa Bi Marion Wairimu na Bw Patrick Kanuri.

Alipata elimu ya awali katika Shule ya Msingi ya Master Education Centre (MEC), Kirinyaga alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mnamo 2010 kisha kujiunga na Shule ya Upili ya Wasichana ya Naromoru, Nyeri mwanzoni mwa 2011.

Aliufanya mtihani wa kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) shuleni humo mwishoni mwa 2014.

Waliochochea ari yake ya kukipenda Kiswahili na kumakinika zaidi katika lugha hii ni walimu wake katika Shule ya Msingi ya Master Education Centre, Bw Joseph Chomba na Bw Leonard Mwai.

Wawili hao walijitolea sabili kuhakikisha kuwa wanafunzi wao wanakithamini Kiswahili kwa kiwango sawa na masomo mengine. Mbali na kumpokeza Wangu malezi bora zaidi ya kiakademia, walitangamana naye kwa karibu sana na wakamfaa kwa hali na mali.

MEC ilikuwa imetenga Jumatano ya kila wiki kuwa siku ya kuzungumza Kiswahili miongoni mwa walimu na wanafunzi. Hii ni ada ambayo Wangu anaungama kuwa ilichangiwa kuinua pakubwa kiwango chake cha umilisi wa lugha.

Isitoshe, ni hatua iliyowafanya wengi wa walimu wa MEC kuwasherehekea vilivyo wanafunzi wao waliojitahidi kuyaendesha mawasiliano yao yote ya siku kwa Kiswahili mufti. Gharadhi hii ilimpa Wangu msukumo wa kuipa lugha ya Kiswahili hadhi yake na kuichangamkia ipasavyo.

“Nilijifunza misamiati ya kila sampuli na nyingi za insha nilizokuwa nikiziandika zikaanza kuwa za kuvutia kiasi cha kunizolea tuzo anuwai za haiba kubwa.”

Wangu anatambua pia ukubwa wa mchango wa aliyekuwa mwalimu wake wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Naromoru Girls, Bw Geoffrey Charagu. Zaidi ya kuotesha mbegu za mapenzi ya dhati kwa Kiswahili ndani ya mwanafunzi wake huyu, Bw Charagu alimhimiza Wangu kujitahidi masomoni na akampa majukumu ya kuwaongoza wanafunzi wengine katika uendeshaji wa mijadala na shughuli za Chama cha Kiswahili Shuleni Naromoru Girls. Majukumu haya yalimpa Wangu majukwaa mwafaka ya kuhakikisha kwamba kisu chake cha umahiri wa Kiswahili hakisenei hata kidogo.

Makongamano mengi yaliyohudhuriwa na Wangu kupitia Chama cha Kiswahili yalichangia kuyanoa makali yake katika sanaa ya ulumbi na wanafunzi wengi wakatamani sana kuiga mfano wake.

Vingi vya vitabu vya Kiswahili alivyovisoma chini ya uelekezi wa Bw Charagu vilimwamshia ari ya kutaka kuwa mwandishi arifu wa Isimu na Fasihi ya Kiswahili.

Wangu alijitosa katika ulingo wa uandishi pindi alipokamilisha masomo yake ya sekondari. Alitunga shairi lake la kwanza lenye anwani ‘Mama’ ambalo lililenga kuwahongera akina mama kwa bidii wanazozifanya katika uendeshaji wa masuala ya familia zao na jamii kwa ujumla.

Shairi hili lilifichua utajiri wa kipaji cha Wangu katika sanaa ya utunzi wa kazi bunilizi.

Baada ya kujifunza mbinu mbalimbali za utunzi wa mashairi ya kila aina, alipania sasa kuyakariri mbele ya umma kwenye hafla tofautitofauti za makuzi ya sanaa zilizoandaliwa katika Kenya National Theatre, Nairobi.

Uzoefu huo wa kutunga mashairi kwa azma ya kuburudisha wasomaji, watazamaji na wasikilizaji wake; ulimtia baadaye hamasa ya kuandika hadithi fupi zilizo na mtiririko na mnato mkubwa ajabu.

Nyingi za kazi za Wangu zimekuwa zikilenga kuangazia utepetevu uliopo katika makuzi ya misamiati ya Kiswahili.

Kwa ubunifu mkubwa, amekuwa akiyaandaa mafumbo (puzzles) katika kumbi za fumbo magazetini. Mafumbo haya ni ya kuzingua mawazo, kufikirisha sana na kuwaburudisha wote wanaojitahidi kuyafumbua. Ni mafumbo yanayojikita katika masuala ya makuzi ya lugha kwa kushirikisha pia ufahamu wa watu kuhusu habari mbalimbali za Kenya, Afrika na dunia.

Wepesi wa lugha katika uandaaji wa mafumbo haya unatoa fursa kwa idadi kubwa ya aina mbalimbali ya watu kushiriki kwa kuwa hayalengi tu wanafunzi, walimu au wataalamu wa lugha.

Wangu kwa sasa amechapisha diwani ambayo kulingana naye, itawasaidia sana walimu na wanafunzi wa shule za upili kuizamia fani ya ushairi kwa urahisi zaidi. Mbali na kubadilisha sura ya usomaji na ufundishaji wa mashairi, kitabu hiki kinachoangazia mengi ya masuala ibuka katika jamii, kitampa mwanafunzi yeyote changamoto ya kupanua mawazo yake na kumweka katika nafasi ya kumaizi maana ya juu na ya ndani ya kila shairi.

Maazimio

Wangu ananuia kuwa mtangazaji wa habari za Kiswahili katika runinga au redio pindi atakapohitimisha masomo yake. Zaidi ya hayo, anakusudia kuwa mmiliki wa blogu ya Kiswahili itakayokuwa na masimulizi ya hadithi anuwai zitakazoburudisha na kuwaelimisha wasomaji.

Aidha, anadhamiria kukuza sanaa ya uandishi wa mashairi kwa kutumia picha. Uandishi huo utakuwa jukwaa zuri kwa mtunzi yeyote kuangazia zaidi ya mawili katika shairi moja. Sanaa hii ambayo haijakuzwa sana, itamsaidia mchoraji na malenga kushirikiana ipasavyo katika ukuzaji wa ushairi.

Jivunio

Katika Chuo Kikuu cha Daystar anakosomea shahada yake ya kwanza, Wangu ni mhariri wa Kiswahili katika Jarida la Involvement. Kupitia chapisho hilo, Wangu ameweza kuwahamasisha wanafunzi wenzake kuzungumza na kuandika Kiswahili kwa ufasaha zaidi huku akiwaongoza katika utunzi wa hadithi zenye mnato na mtiririko wenye mantiki wa kimawazo.

Isitoshe, ameweza kuwapa motisha ya kujiendeleza kitaaluma huku akiwa mfano wa kuigwa miongoni mwa waandishi chipukizi chuoni humo.

Kupitia usomaji wa kazi nyingi za kitaaluma na kuzihariri tungo mbalimbali za kibunifu, Wangu anakiri kwamba amejifunza misamiati anuwai ambayo kwa sasa ni ya manufaa tele kwa timu ya waandishi chipukizi wa Kiswahili anaowaelekeza.

Pamoja na hayo, Wangu amewahi kuangaziwa kwenye ukumbi wa ‘Mshairi Wetu’ katika gazeti hili la Taifa Leo ambapo alisimulia safari yake katika uandishi na utunzi wa mashairi ya Kiswahili.

Mengi ya mashairi yake yamekuwa yakichapishwa takriban kila wikendi katika gazeti hili. Mashairi haya yamechochea ari ya wanafunzi wengi ndani na nje ya Chuo Kikuu cha Daystar kutaka kujua jinsi ya kuyasarifu mashairi ya arudhi.

Wangu anajivunia upekee wa fursa za kuwahi kuhojiwa katika vipindi vya makuzi ya sanaa katika vituo vya Y-254 TV, KU-TV na Radio Citizen. Weledi wake katika lugha uliwahi kumpa fursa ya kutafsiri hadi kwa Kiswahili kitabu ‘Save the Elephants’ cha Dkt Lucy King.

You can share this post!

BBI: Baadhi ya mawaziri kuteuliwa kutoka miongoni mwa...

WASIA: Kumthamini mwalimu ndiyo msingi wa kumthamini...

adminleo