NDIVYO SIVYO: Neno mwafaka la kuhusisha mtu au kitu na kingine ni kunasibisha
Na ENOCK NYARIKI
WATU wanaposema kwamba fulani ‘anaitanishwa’ na watu fulani, kauli hiyo hutarajiwa kufahamisha kuwa anayezungumziwa anahusiana kiukoo au kwa namna nyingine na watu wanaozungumziwa.
Kuna uwezekano kuwa wanaoitumia dhana hiyo kwa maana hiyo huikanganya na neno ‘itwa’ kwa maana ya kupewa utambulisho.
Mathalani, mtu anapokuuliza unaitwa nani(?), huwa anataka kujua jina lako. Kwa hivyo, neno ‘itanishwa’ nalo hukusudiwa kuibua dhana ‘unahusishwa na nani?’ au ‘unahusishwa na ukoo au daraja gani?’ Yamkini pia kwamba neno ‘itanishwa’ linakurubiana kwa namna fulani na lugha za kwanza za watu fulani. Lakini jinsi watu hao wanavyotagusana na wengine, hujikuta wakishiriki dhana hiyo kwa maana tuliyoitaja. Kwa vyovyote vile, ‘itanishwa’ ni dhana ambayo si sahihi ila hutumiwa tu kufanikisha mawasiliano ya barabarani.
Neno ita ambalo dhana *itanishwa hudhaniwa kuundwa kutoka kwalo lina zaidi ya maana tatu. Kwanza, ni kumwalika mtu katika hafla au mkutano. Pili, ni kumtaja mtu kwa jina na kumwashiria aje kwako. Tatu ni kumtambulisha mtu kwa kumpa jina.
Kutokana na kitenzi ita tunapata minyambuliko itia, itika, itisha, itiwa, itana. Minyambuliko hii yote ina maana zinazohusiana kwa namna fulani na dhana iliyoizaa.
Mnyambuliko itia, kwa mfano, una maana ya ‘ita kwa ajili ya’ ilhali itika una maana ya jibu unapoitwa au kukubali mwaliko. Jambo moja linalobainika wazi hapa ni kuwa hatuna dhana itanishwa!
Dhamira ya watu iwapo ni kutaka kueleza kuwa mtu fulani ni wa ukoo fulani, anahusishwa na daraja fulani au kundi fulani la watu, neno mwafaka linalopaswa kutumiwa katika mazingira hayo ni nasibisha.
Kwa hiyo, tunapaswa kusema mtu fulani ananasibishwa na ukoo fulani, daraja fulani au kundi fulani la watu. Kuna uwezekano mkubwa kwamba kitenzi nasibisha kinatokana na nomino nasaba.
Nomino hii ina maana ya uhusiano wa kizazi baina ya watu; uhusiano kutoka katika mlango au ukoo. Maelezo haya ni kwa mujibu wa toleo la awali la Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Kutokana na maana hii tunapata methali: Mtaka nyingi nasaba hupata mwingi msiba; yaani anayejitapa kutokana na ukoo au kabila hufikwa na tabu nyingi.
Kadiri ya wakati, ile dhana ‘uhusiano’ katika neno nasaba ilianza kutumiwa kimtambuko kujumuisha mahusiano mengine yasiyo ya kiukoo au kimlango.
Kwa hivyo kitenzi nasibisha kina maana ya husisha na au fanya kuwa moja na. Alhasili, hatusemi ‘kuitanishwa na mtu fulani’ bali kauli mwafaka ni kunasibishwa na mtu fulani.