Habari Mseto

Mwanamume auguza majeraha baada ya 'mkewe' kumdunga kisu kisa mapenzi

November 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MISHI GONGO

MWANAMUME katika mtaa wa mabanda wa Moroto Tudor mjini Mombasa anauguza majeraha ya kisu aliyosababishiwa na mkewe wiki iliyopita kwa madai kuwa alikuwa akimsaliti kimapenzi.

Katika mahojiano na Taifa Leo hapo Jumanne Bw Mwaya Ndoko, 43, alieleza kuwa mashambulizi hayo huenda yakawa yamesababishwa baada ya mkewe huyo kupekuwa simu yake.

Bw Ndoko alisema mwanamke huyo Bi Mwanajuma Kenga aliyeishi naye kinyumba – come we stay – kwa muda wa miaka mitatu alikuwa na mazoea ya kutumia simu ya mumewe kama tochi anapoenda msalani usiku.

Hata hivyo siku ya kisa hicho kilichomuacha na jeraha kwenye kiuno na mkono, mkewe alitoka akamuacha akiangalia filamu. Baada ya muda wa saa moja alirudi akiwa amejawa na ghadhabu huku akimmiminia mumewe matusi.

“Niliangalia kwa muda kisha nikalala. Niligutushwa na kelele za mke wangu aliyekuwa aking’ang’ana kufungua mlango ambao kufuatia mvua kubwa ulikuwa unafunguka kwa shida,” akasema.

Anaeleza baada ya kufungua mlango, Bi Kenga alimvamia kitandani na kumdunga kisu kwenye kiuno kabla ya kumkata katika mkono wake wa kushoto.

“Siku ya Jumanne wiki iliyopita alichukuwa simu yangu na kutoka nayo nje lakini aliporudi alikuwa amejawa na hasiri akifoka kuwa ‘mwanamume wewe ni malaya sana kabla hujaniangamiza acha nichukue hatua’ kisha kunishambulia kwa kisu,”  Bw Ndoko alieleza.

Majirani walipowasili Bi Mwanajuma alichukuwa fursa hiyo kutoroka katika eneo la mkasa akimuacha mumewe akivuja damu.

Bw Mwaya Ndoko amuonyesha Mzee wa Mtaa Bw Shaban Mgalla alivyodungwa kisu katika kisa ambapo mshukiwa ni Mwanajuma Kenga. Picha/ Wachira Mwangi

Bw Ndoko alipelelekwa katika hospitali kuu ya mkoa wa pwani Makadara.

Baada ya matibabu aliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Makupa chini ya nambari ya unakili OB59/13/11/2019.

Mwanamume huyo alieleza kuwa hawakuwa wamejaliwa mtoto na Bi Kenga katika kile kinaelezwa na sababu za kiafya.

Maafisa wa polisi bado wanamsaka mwanamke huyo.

Mzee wa mtaa katika eneo hilo Shaban Mgalla alisema katika mtaa huo wa mabanda visa vya wanandoa kupigana na kuumizana vinaongezeka kila uchao.

Alisema vingi vya visa hivyo husababishwa na hali duni ya kifedha na kukosa uaminifu ndoani.

“Unakuta mwanamke anataka maisha ya hali ya juu wakati mume wake hana uwezo,akitaka vitu ama matumizi ambayo mumewe hawezi kumkidhi hapo huzuka mvurugano,”alisema akiongezea wivu kama sababu nyegine ya vita kati ya wanandoa.

Hata hivyo alisema vingi ya visa hivi huishia majumbani kwani wengi kuamua kutafuta vita hivi bila kuhusisha serikali.

“Kutatua vita kati ya wanandoa kinyumbani ni vizuri lakini pia kuna hasara zake. Wanandoa kama hawa hutakikana kupata ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu ilikuwawezesha kutatu. Lakini wakisuluhisha nyumbani hubakisha hasira ndani ya nyoyo zao ambazo huweza kuripuka wanapokosana kidogo,” alieleza.

Aliwashauri wanandoa kutafuta msaada wa wataalamu au watu wenye busara kuwasaidia kutatua matatizo sugu ndani ya ndoa zao.