• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
JAMVI: Uhuru anavyotumia teuzi kama chambo cha kuinasa jamii ya Wasomali

JAMVI: Uhuru anavyotumia teuzi kama chambo cha kuinasa jamii ya Wasomali

Na WANDERI KAMAU

UTEUZI wa Noordin Haji kama Mkurugenzi Mpya wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Rais Uhuru Kenyatta ni sehemu ya msururu wa teuzi za hivi punde zaidi ambazo wachanganuzi wasema ni mikakati yake kudumisha uungwaji mkono wa jamii ya Somali kwa viongozi wa Jubilee.

Wadadisi wasema hatua hiyo pia ni mbinu ya Bw Kenyatta kuhakikisha eneo la Kaskazini Mashariki, hasa jamii ya Somali, linaunga mkono Chama cha Jubilee (JP) kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Kufikia sasa, jamii hiyo inawakilishwa serikalini na viongozi wa sehemu hiyo wenye ushawishi mkubwa kama vile Waziri wa Elimu Amina Mohamed, Kiongozi wa Wengi Aden Duale, Waziri wa Ustawi na Viwanda Adan Mohamed miongoni mwa wengine.

Wachanganuzi wasema ni kwa misingi hiyo ya kutaka kuvutia wapiga kura wa eneo hilo ambapo Waziri wa Elimu Amina Mohamed alitunukiwa wadhifa muhimu wa elimu ili “aweze kuonekana zaidi” hasa na wenyeji wa eneo hilo.

Ingawa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ina mvuto mkubwa, kuna hisia kwamba, waziri huyo hakupata muda wa kutosha wa kutangamana na wakazi kunadi sera na ufanisi wa Jubilee.

 

Kupanua usemi 

“Bi Mohamed na Nordin wameteuliwa kimakusudi ili kupanua usemi wa jamii hiyo katika serikali ya Jubilee,” asema Hassan Ole Naado, mchanganuzi wa kisiasa.

Ni mkakati huo pia ulichangia kudumishwa kwa Bw Mohamed kama Waziri wa Ustawi wa Viwanda, huku wenzake kadha wakichujwa.

Kulingana na Bw Naado, uteuzi wa wawili hao unalenga kuvunja ukiritimba wa kisiasa wa Bw Duale, ambaye ndiye sura ya jamii hiyo katika serikali ya Jubilee.

“Mkakati wa Rais Kenyatta ni kuhakikisha jamii ya Wasomalia, ambayo kwa kawaida hujihusisha na serikali iliyo mamlakani inasalia huko kuelekea 2022.

Mpango wake ni kukuza watu wengine kadhaa, ambao watakuwa na usemi mkubwa ili kurahisisha kibarua cha kupenya kisiasa eneo hilo kurai wenyeji kuunga mkono azima ya Naibu Rais William Ruto kuwania urais,” asema Bw Naado.

Kutokana na hayo, anasema huenda kukawa na teuzi nyingi za wazaliwa wa jamii hiyo kushikilia nyadhifa muhimu serikalini.

“Lengo la Jubilee ni kuhakikisha imedumisha uungwaji mkono wa jamii hiyo, kwani takwimu zinaonyesha idadi yao inaongezeka maradufu,” asema Bw Ole Naado.

Baadhi ya wachanganuzi  hata hivyo wanataja mkakati huo kama unaosukumwa na Bw Ruto, ili “kuwakuza” viongozi wapya ambao watamsaidia kupenya katika jamii anazolenga kutumia kujikuza kisiasa.

 

Idadi inaongezeka

Ni dhahiri kwamba, Jubilee pia inawekeza kisiasa katika jamii hiyo baada ya takwimu kuonyesha kwamba, idadi yake inazidi kuongezeka.

Kulingana na takwimu zilizotolewa na Shirika la Kukadiria Idadi ya Watu Kenya (KIHBS) hivi majuzi, jamii hiyo inakisiwa kuwa miongoni mwa tatu kubwa zaidi nchini.

Mbali na hayo, imeibuka kwamba hatua ya rais kuishirikisha jamii hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa “muafaka wa siri” wa kutatua suala la kutengwa kwake na serikali nyingi zilizotangulia.

Wadadisi wanashikilia kwamba, lengo kuu la Rais Kenyatta ni kuondolea mbali dhana kwamba, “viongozi wa bara” wanalichukia eneo hilo, hasa kutokana na kumbukumbu za Vita vya Shifta vya 1969 ambapo jamii hiyo iliathirika pakubwa.

Kulingana mchanganuzi Wycliffe Muga, kumbukumbu za madhila ya kijadi kama Mauaji ya Wagalla mnamo 1984 dhidi ya jamii ya Oromo, yamechangia pakubwa kusambaa kwa vitendo vya kigaidi katika eneo hilo.

Ripoti zasema, Mzee Jomo Kenyatta alituma vikosi vya usalama kukabili Wasomali ambao walikuwa wakitaka eneo lao kurejeshwa nchini Somalia, wakidai kwamba si Wakenya.

 

Uhasama

Hilo linatajwa kusababisha uhasama mkubwa ambao umekuwa ukidhihirika hadi sasa. Ni hali hiyo ambayo Rais Kenyatta anajizatiti kutatua.

“Kuna dhana miongoni mwa wakazi wa eneo la kaskazini mwa nchi kwamba, walitengwa kwa muda mrefu na serikali zilizopita. Hili ndilo jambo ambalo Rais Kenyatta analenga kulimaliza anapong’atuka uongozini,” asema Bw Muga.

Asema huo ni mkakati wa muda mrefu ambao utazima mashambulio ya kigaidi kama lile lililotokea katika Chuo Kikuu cha Garissa mnamo 2015, ambapo zaidi ya watu 150 waliuawa.

Lakini hayo yakiendelea, kuna mgawanyiko wa hisia kuhusu aliyechangia zaidi kukuza hadhi ya jamii hiyo kisiasa, kati ya Rais Kenyatta na Bw Ruto.

Baadhi ya viongozi wamekuwa “wakimshukuru” Bw Ruto kama “chemichemi” ya ufanisi wao, wakirejelea chama cha URP ambapo Bw Duale alikuwa mhusika mkuu.

Hata hivyo, Bw Duale amekuwa akiwataja mabw Kenyatta na Ruto kuwa nguzo kuu za kisiasa kwa uthabiti wa jamii hiyo na ukanda wa Kaskazini Mashariki kwa jumla.

You can share this post!

JAMVI: Wazika tofauti zao kisiasa, masaibu ya Mutua yaanza...

JAMVI: Sifuna atadhibiti ngalawa kwenye bahari ya kisiasa...

adminleo