• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 12:46 PM
KIKOLEZO: Umesota? Yaliwafika wasanii hawa pia

KIKOLEZO: Umesota? Yaliwafika wasanii hawa pia

Na THOMAS MATIKO

TUNAISHI katika kipindi ambacho kila mtu analia kaishiwa na hela mfukoni isipokuwa Rais Uhuru Kenyatta.

Wiki kadhaa alibaki kutushangaa wananchi ni vipi tumesota. Lakini bwana hakuna asiyesota isipokuwa Rais. Wapo watu maarufu pia ambao wamekuwa kuwa na mtonyo wa maana ila pia nao waliishia kukaukiwa.

Rose Muhando

Enzi za ustaa wake Muhando alifanikiwa kukafunga kwelikweli. Hakuna sehemu au taifa katika ukanda wetu huu ambao hakuwahi kuitiwa shoo. Pesa hazikuwa shida kwake. Alifanikiwa kujenga nyumba ya kifahari na kununua magari yapatayo matatu ya kifahari. Mara ghafla akapotea. Zikazuka taarifa kwamba alikuwa ameingilia ulambaji poda. Kidogo kidogo akaanza kuuza mali zake, magari yote akayapiga mnada. Mwisho wa siku watu walipomchoka, wakamwachanisha. Siku hizi Muhando anaishi Kenya kama omba omba tu.

Ray C

Ni msanii mwingine aliyetisha zaidi ya mwongo umepita. Hungezungumzia muziki wa bongo flava bila ya kumtaja huyu kichuna. Alikusanya noti, akawekeza kwenye maduka ya nguo, umiliki wa majumba na hata magari. Lakini baadaye akajiingiza kwa maunga baada ya kutambulishwa na aliyekuwa mpenzi wake Lord Eyez. Kilichofuata ni kushindwa muziki na kuanza kuziuza mali zake ili kukimu kiu yake ya poda. Mpaka leo hana kitu, anaishi kwa imani tena sio Tanzania. Anazunguka kwenye mataifa tofauti. Duru zinaarifu kuwa kwa sasa yupo Oman kwa jamaa wake mmoja baada ya kuishi Kenya sana.

Mr Nice

Imedaiwa kuwa Mr Nice ambaye amekuwa akihangaika kurejea kimuziki alifilisishwa na tabia yake ya kupenda mademu na kula bata kupita kiasi. Inasemekana aliuza mali yake kibao ikiwemo magari yake manne ya kifahari aliyofanikiwa kupata enzi za ustaa wake. Baadhi ya tetesi hizo pia zimedai kwamba jamaa alipenda sana kwenda Afrika Kusini kuponda raha. Tetesi hizo pia zimedai kuwa Ilifikia wakati hata maji ya kuosha magari yake alitumia ya chupa kwa madai kuwa maji ya bomba/mfereji yangemharibia gari. Baada ya kuparara aliishia kuanza kufuga kuku.

Chris Tucker

Mchekeshaji huyu maarufu wa Marekani na mwigizaji yupo kwenye pilka pilka za kuandaa filamu mpya na mkongwe Jackie Chan Rush Hour 4 baada ya ile ya Rush Hour 3 kufanya vyema sokoni miaka kadhaa iliyopita.

Mnamo 2007, Tucker aliangukia dili nzito ya dola milioni 25 (2.5 bilioni) kuwa staa wa Rush Hour 3 pamoja na Jackie Chan, dili iliyomfanya kuwa mwigizaji wa Hollywood aliyelipwa mkwanja mnene mwaka huo.

Miaka mitatu baadaye, ikabainika kuwa Tucker alikuwa akidaiwa na serikali ushuru wa dola milioni 11, aliyokuwa akikwepa kulipa toka mwaka wa 2001 hadi 2007. Staa huyo kwa kuhofia kwenda jela, akalazimika kuuza majumba yake mawili ya kifahari kule Florida na lingine la tatu alilokuwa nalo kule Los Angeles, ili kufuta deni hilo. 2016, aliripotiwa kulipa deni la kitita kingine kizito cha dola milioni moja. Madeni mengi yamemwacha akiwa na hali mbaya ya kifedha.

Wesley Snipes

Alivuma sana miaka ya nyuma na msururu wa filamu zake za The Blade. Snipes ambaye ni staa wa aksheni alirejea hivi majuzi kwenye uigizaji baada ya kutoka jela alikokuwa ametupwa kufuatia kushindwa kulipa deni la ushuru alilokuwa akikwepa kwa kipindi cha miaka sita.

Ni kitu cha kushangaza ikizingatiwa kwamba miaka ya 1990s, hakuna mwigizaji alikuwa akipiga noti kama yeye na mvunja mbavu Eddie Murphy. Lakini licha ya kutengeneza mkwanja wa maana, aliendelea kukwepa kulipa ushuru na 2006 alitangazwa kuwa kafilisika baada ya kushindwa kulipa deni la dola milioni 12. Hali hiyo ndiyo iliyompelekea yeye kufungwa jela kwa miaka mitatu hadi Aprili 2013 alipomaliza kifungo na kuachiliwa huru.

Toni Braxton

Toni alikuwa miongoni mwa wanamuziki wa RnB waliotisha sana miaka ya 90s. Enzi za ustaa wake Toni aliuza zaidi ya nakala milioni 40 za albamu zake kote ulimwenguni chanzo kilichoweza kumtengenezea utajiri wake unaokadiriwa kuwa dola 10 milioni kufikia Mei 2017.

Ni utajiri uliopungua kweli kweli ikizingatiwa kwamba alitangaza kuwa kafilisika 2010 baada ya kushindwa kulipa deni la dola milioni 50. Mwaka jana karipotiwa kununua mjengo wa dola milioni tatu ikiwa ni baada ya kuanza upya tena kusaka hela. Kipato hicho kimetokana na mauzo ya muziki wake alioachia mwaka jana na kipindi chake cha televisheni Braxton Familly Values.

50 Cent

Kipindi akiwa anatesa na kundi lake la G-Unit, rapa 50 Cent alikuwa kajitengenezea utajiri wa dola 400 milioni kutokana na muziki. Lakini 2016 alitangaza kuwa kafilisika baada ya mahakama kumtaka amlipe fidia ya dola milioni saba kichuna Lastonia Leviston kwa kumharibia jina.

Kando na masaibu hayo, kwenye kesi nyingine aliamuriwa alipe dola milioni 17 baada ya kuruka dili la kibiashara la headphone alilokuwa ameingia. Akitangaza kufilisika mahakamani, 50 Cent alisema utajiri alionao kwa sasa unafikia dola milioni moja pekee, kiwango ambacho hakiendani na madeni yake.

DMX

Jina lake lilivuma miaka ya 1990 akitajwa kuwa mmoja wa marapa wakali. Lakini maisha yamembadilikia kabisa akapoteza mali zake nyingi na hivi majuzi katupwa tena jela miezi michache tu baada ya kuachiliwa huru kutoka jela kutokana na makosa ya matumizi na uuzaji wa madawa ya kulevya na pia kupatikana na silaha pasi na kuwa na leseni. Uraibu wake wa dawa za kulevya ni mojawapo ya chanzo cha yeye kufilisika. Lakini hata zaidi ni kesi kibao za kushindwa kutoa malezi ya watoto wake aliozaa na wanawake tofauti akiwa na jumla ya watoto 15. Alihukumiwa jela Julai 2015 kwa kushindwa kutoa malezi ya watoto hao yaliyokuwa yamekadiriwa kufikia Sh41 milioni na sasa karushwa tena huko kisa ukwepaji wa kulipa kodi.

You can share this post!

Juhudi za kufua panga kuwa majembe barani Afrika

ANA KWA ANA: ‘Nimevunja wengi moyo kutengana na...

adminleo