• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 PM
DAU LA MAISHA: Mwenge wa haki za wasichana na wanawake vitongojini

DAU LA MAISHA: Mwenge wa haki za wasichana na wanawake vitongojini

Na PAULINE ONGAJI

YEYE ni mmoja wa mabinti ambao wamejitolea kuelimisha wasichana na wanawake katika vitongoji duni vikuu nchini kuhusu masuala wanayokumbana nayo kila siku.

Ni kazi ambayo Bi Nancy Wanjiru, 30, amekuwa akiendesha pamoja na wenzake watano katika vitongoji duni vya Mathare, Kayole, Mukuru na Dandora kupitia shirika la Fortress of Hope Africa.

Kwa upande wake jukumu lake hasa linahusisha kuunganisha wasichana kila wiki katika ukumbi wa kijamii wa Undugu mtaani Mathare na kuwapa elimu kuhusiana na masuala yanayowahusu.

Kupitia shughuli hii wanaelimisha wasichana kuhusu haki yao kufikia huduma ya afya ya uzazi, kuelewa aina tofauti ya dhuluma, huduma bora za afya, kutoa ushauri nasaha na hata kuwaelekeza panapohitajika hasa ikiwa wamewahi kukumbana na dhuluma za kijinsia.

Pia wamekuwa wakiwapa waathiriwa mazingira salama ya kuzungumzia pengine suala ambalo wanapaswa kufanya ili kulifuatilia kuhakikisha kwamba mhusika anapata haki.

Aidha, wamekuwa wakisaidia wanawake kuhusu afya ya uzazi kwa kuwapa habari kuhusu jinsi ya kufikia mbinu za upangaji uzazi na kutetea haki zao, vile vile kujua jinsi ya kuzungumza kwa uhuru ikiwa wamedhulumiwa.

“Tuna jukwaa la dharura kwa jina Aunty Jane ambapo wanawake wanapata maelekezo ya huduma za afya ya uzazi,” aeleza.

Ni shughuli ambayo imekuwa na matokeo mema huku wakifikia zaidi ya wasichana 500 kila mwezi katika kipindi cha miaka mitatu kufikia sasa.

“Nakumbuka hasa kisa kimoja cha ufanisi tulipomsaidia msichana mmoja mtaani Huruma ambaye alikuwa ameolewa licha ya kuwa mchanga. Isitoshe, mwanamume huyo alikuwa akimdhulumu ambapo jitihada zetu zilimuokoa msichana huyo kutokana na ndoa hiyo na kuhakikisha kwamba mhusika anashtakiwa sio tu kwa tuhuma za dhuluma za kijinsia, bali pia kimapenzi. Kwa sasa anahudumu kifungo cha miaka mitano,” aeleza.

Mbali na hayo, jitihada hizi zimeimarisha huduma kwa vijana na sasa wasichana eneo hilo wanaweza fikia mbinu za upangaji uzazi wazitakazo kutokana na huduma bora wanazopata kule.

Sababu yake

Azma yake inatokana na maisha magumu aliyopitia tokea utotoni.

“Nilizaliwa na kusomea katika kitongoji duni cha Mathare. Mtaa huu kama vitongoji duni vingine nchini, unafahamika kwa uhalifu na maovu mengine kama vile dhuluma dhidi ya wanawake, ubakaji, mimba zisizotarajiwa na ndoa za mapema. Kwa hivyo nilipokuwa nikikua nilishuhudia haya na hivyo nikawa na moyo wa kutaka kubadilisha mambo na njia ya kipekee ya kufanya hivyo ilikuwa kuelimisha wasichana na wanawake,” aeleza.

Hasa uamuzi wake wa kurejea katika jamii yake na kuelimisha wasichana na wanawake kuhusu jinsi ya kujishughulikia na kusimama kidete kutetea haki zao ulichochewa na rafiki yake ambaye tayari alikuwa ameanzisha shirika hili ambapo wakati huo liliendesha shughuli mtaani Kayole.

“Na hivyo niliona shirika hili kama jukwaa mwafaka la kuokoa jamii yangu. Mradi huu ulitarajiwa kuendelea kwa miaka mitatu, na hivyo tukachagua wasichana kadhaa ambao walikuwa mawakala wetu wa kuleta mabadiliko. Tuliwapa mafunzo na hivyo ndivyo tulivyoanzisha jukwaa la kuwafikia wasichana 500 kila mwezi,” aongeza.

Anatumai kwamba mradi huu ambao kwa sasa umefikia kikomo utaendelea baada ya kupata ufadhili, na hivyo kuwawezesha kuendeleza shughuli sio tu katika vitongoji duni hivi, bali pia kupanua huduma zao katika sehemu zingine nchini.

You can share this post!

Black Junior FC yazidi kujiimarisha mashinani

MWANAMKE MWELEDI: Alitikisa riadha akibeba Golden League...

adminleo