Michezo

NJE! Kichapo cha Europa kilizamisha kabisa chombo cha Emery

November 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

UNAI Emery sasa si kocha wa Arsenal tena, baada ya kuangukiwa na shoka hapo Ijumaa.

Emery ambaye aliteuliwa kuchukua nafasi ya Arsene Wenger mwaka 2018, aliachishwa kazi miezi 18 baadaye kutokana na msururu wa matokeo duni.

Arsenal haijashinda mechi saba mfululizo kwa mara ya kwanza tangu 1992.

Baada ya kuzimwa 2-1 na Eintracht Frankfurt katika Ligi ya Uropa siku ya Alhamisi, ripoti kutoka jijini London zilisema mapema Ijumaa kuwa, viongozi wa ngazi za juu Arsenal waliandaa kikao. Uamuzi wa kikao hicho ulikuwa kuagana na kocha huyo Mhispania.

Mbali na msururu wa matokeo ya kusikitisha, uhusiano wake mbaya na baadhi ya wachezaji, ikiwemo viungo Granit Xhaka na Mesut Ozil, unaaminika pia ulimsababishia masaibu hayo.

Emery ni kocha wa tatu kutimuliwa kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu, baada ya Javi Gracia (Watord) na Mauricio Pochettino (Tottenham Hotspur).

Mhispania huyo aliingia mechi dhidi ya Frankfurt akiwa tayari na presha, ambayo iliongezeka hata zaidi baada ya vijana wake kutupa uongozi wa bao moja, katika mechi ambayo waliishia kuchapwa na Wajerumani hao uwanjani Emirates.

Emery alitarajiwa kuwa mtu atakayerejeshea Gunners sifa nchini Uingereza, baada ya klabu hiyo kusikitisha kwa miaka kadhaa ya mwisho ya Mfaransa Arsene Wenger.

Hata hivyo, kocha huyo wa zamani wa Paris Saint-German (PSG) alikabiliwa na shinikizo kali baada ya kumaliza mechi tano za ligi bila ushindi. Arsenal ndio klabu pekee katika mduara wa 10-bora, ambayo imefungwa mabao mengi kuliko yale ambayo imefunga.

Kipindi chake na Arsenal kilionekana kuvurugwa hata zaidi siku ya Alhamisi, pale bao la kipindi cha kwanza kutoka kwa Pierre-Emerick Aubameyang lilifutwa na Daichi Kamada aliyesawazisha na kisha kufungia Frankfurt bao la ushindi katika kipindi cha pili.

Mashabiki wachache wa Arsenal waliofika katikaa uwanja wao wa nyumbani walikejeli matokeo hayo.

Inasemekana kuwa, kusakata mechi saba bila ushindi ndiyo matokeo mabaya kabisa ambayo Arsenal imewahi kuandikisha tangu mwaka 1992.

Emery, 48, alikuwa amepata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wa Arsenal ligi ilipoenda mapumziko mafupi kupisha mechi za timu za taifa, huku mahasimu wao Tottenham wakijaza nafasi ya Pochettino kwa kumuajiri Jose Mourinho.

Hata hivyo, Emery alionekana kufahamu siku zake uwanjani Emirates zimefika ukingoni, aliposema baada ya kichapo cha Frankfurt kwamba “sasa mambo yetu si mazuri kabisa.”

Kitulizo cha Arsenal, ambayo huenda ikarukia nafasi ya tano kutoka nambari nane matokeo yakiwa mazuri kwake wikendi hii, ni kwamba imepoteza mara moja tu katika mechi 15 zilizopita dhidi ya Norwich kwenye mashindano yote. Arsenal itazuru Norwich hapo kesho Jumapili chini ya kocha msaidizi Freddie Ljungberg, ambaye pia anasimamia kikosi cha Arsenal cha wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23.

Muda kutafuta kocha

Tetesi zinasema kuwa, Mswidi Ljungberg atashikilia wadhifa huo angalau hadi Februari ili kupatia wakuu wa klabu hiyo ya Uingereza muda wa kutafuta kocha.

Baadhi ya makocha ambao Arsenal inaaminika kumezea mate ni Nuno Espirito Santo (Wolves), Carlo Ancelotti (Napoli) na naibu kocha wa Manchester City, Mikel Arteta.

Makocha hao watatu wako na kandarasi na klabu zao, kwa hivyo haitakuwa rahisi kupata huduma zao kwani itagharimu ada kubwa. Pochettino, ambaye hana klabu wakati huu, pia amehusishwa na Arsenal.

Wakufunzi wengine, ambao wanaaminika wako katika hatari ya kupoteza kazi kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ni Marco Silva (Everton) na Manuel Pellegrini (West Ham).

Everton, ripoti zinadai, imefanya kikao kuhusu wadhifa wa Silva. Silva na vijana wake wa Everton wako nafasi mbili pekee nje ya mduara hatari wa kutemwa, baada ya kuambulia vichapo saba katika mechi 13 za ligi. Wako na mechi ngumu ya ugenini dhidi ya Leicester kesho Jumapili.

Kocha wa zamani wa Everton, David Moyes anasemekana kuwa mbioni kurejea uwanjani Goodison Park. Mambo ya Everton yanatarajiwa kuwa magumu wiki chache zijazo itakapovaana na Liverpool, Chelsea, Arsenal, Manchester United na Manchester City.

Naye Pellegrini na timu yake ya West Ham hawana ushindi katika mashindano yoyote tangu Septemba. Italimana na Chelsea ya kocha Frank Lampard, ambayo inatisha kwa matokeo ya kufana, wikendi hii.