• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
UMBEA: Usiwe zuzu wa mapenzi, kama wataka mume jibebe ipasavyo

UMBEA: Usiwe zuzu wa mapenzi, kama wataka mume jibebe ipasavyo

Na SIZARINA HAMISI

WANASEMA mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.

Na mwenye ndoa ni yule anayetaka ndoa.

Dada, iwapo unataka kuingia kwenye uhusiano ambao baadaye utazaa ndoa na familia bora, ni muhimu kuwa makini na mtu unayeanzisha naye uhusiano.

Vijana siku hizi wameharibikiwa. Wengi wapo kwa ajili ya kukidhi tamaa zao za binafsi kuliko mapenzi ya dhati.

Ninakudokeza kwamba uhusiano mzuri ambao unaweza kuzaa ndoa na familia bora, ni vyema uanzie kwenye urafiki.

Iwapo utauliza kwa nini uanze urafiki na mwenzako kabla ya kuchukua hatua za ndoa, maana yangu ni kwamba mnapoanzia kwenye urafiki wa kawaida, ni rahisi mtu kuonyesha tabia zake halisi.

Marafiki huzungumza mambo mengi, hata yale yasiyofaa!

Marafiki husimuliana mambo mengi sana yanayohusu maisha yao ya baadaye au yaliyopita, rafiki yako atakuwa huru kukueleza yake ya moyoni bila kuhofia kukukwaza ama kukusikitisha.

Tofauti yake, wapenzi hawapati muda wa kutosha wa kujadili kwa upana mambo mbalimbali yanayowahusu, tayari kunakuwa na mipaka ambayo huwezi kuivuka kwa urahisi.

Iwapo rafiki yako kijana anakupenda kwa dhati, hata kama hajakutamkia, ni rahisi kujua kwa zile ishara na matendo anayokufanyia mkiwa marafiki wa kawaida na jambo ambalo wengi hawalijui, hisia zinazoanza kuchipuka mkiwa tayari mnafahamiana, zina nafasi kubwa ya kuwavusha kutoka hatua ya urafiki wa kawaida, uchumba na hatimaye ndoa.

Utakapokuwa na uhakika kwamba ni kweli anakupenda, hapo ndipo unapokuja ule usemi maarufu wa ‘kushikilia hapo hapo.’ Ukishajua anakupenda, na wewe unampenda, unapaswa kuhakikisha hakuna mtu anayekuja kuingilia uhusiano wenu na kuwavurugia.

Umeshawahi kusikia mtu analalamika kwamba mchumba wake alimsaliti kwa kutoka na rafiki yake na mpaka leo wameoana na huyo rafiki?

Kuwa makini, ukishajua anakupenda, muda mwingi fikiria namna ya kumfanya aendelee kukupenda daima, epuka maudhi, epuka vikwazo au masharti yasiyo na kichwa wala miguu, onyesha uaminifu, onyesha kumjali na kumfanyia yale yote ambayo unapaswa kuyafanya kwa mtu unayempenda.

Mume na mke halali

Sio ajabu kwamba baada ya muda fulani, yeye au wewe, au nyote kwa pamoja mnaanza kuitamani ndoa, kwa pamoja mnapanga malengo yenu na mwisho wa siku mnakuwa mume na mke halali. Zinabaki tu kumbukumbu tamu za namna mlivyoanzisha safari yenu ya mapenzi.

Kuna baadhi ya watu ambao kwa kujua au kutokujua, aina ya maisha wanayoishi, yanawafanya hata wale watu wenye nia njema nao, kuwaogopa na mwisho wanapishana na bahati.

Unaweza kupata rafiki mwenye malengo ya kuja kuwa mume au mke, lakini kwa sababu umeshajiwekea akilini maisha ya ujana yanavyotakiwa kuwa, utakachoangalia ni kupata mwanaume ambaye atakuwa na uwezo wa kukupatia pesa kila mnapokutana, tena mnapokutana lojingi.

Unategemea atakuja kuwa mumeo huyo?

Imekuwa ni kawaida siku hizi kwamba leo mnakutana asubuhi, jioni mmeshachangamshana mwili. Hujui alikotoka, hujui aliyekuwa naye na ikitokea bahati mbaya amekuja na maradhi yake, basi anakuwa ameshakuambukiza.

Imekuwa ni kawaida pia kwa akina dada kuchagua na kuweka masharti kwa aina za mume wanazotarajia kupata. Na ukisikia hayo masharti yao mengine huwa yanachekesha, mengine yanasikitisha na mengine yanashangaza.

Wengi wana matarajio ya kupata waume wenye uwezo mkubwa wa kuwatunza badala ya kuangalia jinsi gani wanavyoweza kutunzana pamoja.

Usiwe limbukeni wa mapenzi, ufundishe moyo wako kuwa na subira ili hata ukiamua kuingia kwenye uhusiano, unakuwa na uhakika na unachokifanya.

 

[email protected]

You can share this post!

SHERIA: Wosia wa maandishi una nguvu kuliko ule wa matamshi

CHOCHEO: Usiende deti ukiwa mlevi, pombe ni adui wa penzi...

adminleo