• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Jinsi mboga aina ya spinachi zinavyompa mkulima faida

Jinsi mboga aina ya spinachi zinavyompa mkulima faida

Na SAMMY WAWERU

KWA muda wa zaidi ya miaka 20 mfululizo, Bw Charles Mwangi amekuwa akikuza mboga aina ya spinachi katika eneo la Mathira, Kaunti ya Nyeri.

Akizilinganisha na mboga kama kabichi na sukumawiki, mkulima huyo anasema spinachi zina mapato ya haraka. Isitoshe, ni zao linalochukua muda mfupi kuanza kuchumwa.

“Spinachi ni rahisi mno kupanda na kutunza. Changamoto zake ni finyu ikilinganishwa na mboga zingine,” anasema. Kulingana na mwanazaraa huyo, shamba lake halikosi mboga hizo kwenye robo ekari kila mwezi, ili kukata kiu cha wateja wake.

Alianza kilimo cha kabichi kwenye kipande cha shamba anachokadiria kuwa thumni ekari. Alitumia Sh3, 000 kama mtaji, ambazo alinunua mbegu na fatalaiza ya kuzinawirisha.

“Mbolea niliitoa katika zizi la ng’ombe wangu, shughuli zote; kulima, upanzi na palizi nikajifanyia mwenyewe,” anaambia Taifa Leo.

Spinachi zinapandwa kupitia miche, ambayo inakuziwa kitaluni. Shughuli hiyo huchukua kipindi cha wiki nne hadi tano, sawa na mwezi mmoja, mche ukiwa na majani matatu au manne.

Eneo zinakopandwa spinachi, wataalamu wa masuala ya kilimo wanapendekeza udongo uwe na uchachu, pH, kati ya 6.4 – 7. “Zinafanya bora zaidi katika udongo tifutifu (loamy soil). Asidi nyingi au uchachu ukizidi kiwango kinachohitajika, hulemaza ukuaji wake,” asema mtaalamu Njeri Murage.

Mkulima anashauriwa kuandaa shamba wiki mbili au tatu kabla ya shughuli za upanzi. Lima kimo cha karibu sentimita 20 kuenda chini. “Ufanye udongo uwe mwepesi na mwororo, wakati huo pia unaweza kuuchanganya na mbolea, ingawa wengi wetu huitia kwenye mashimo au mitaro,” aeleza Bw Charles Mwangi.

Ili kuzuia mboga kuhangaishwa na maji, mkulima huyo huinua udongo juu karibu sentimita 15, kuunda mfano wa kitanda (beds). “Urefu unategemea ukubwa wa shamba la mkulima, kwa mfano vitanda vyangu huviandaa na urefu wa mita 70 na 40 upana. Hilo pia husaidia mizizi ya spinachi kupenyeza udongoni,” afafanua.

Kulingana na maelezo ya mkulima huyo, mashimo kati ya mche hadi mche yawe na nafasi ya sentimita 15, laini ya mashimo akipendekeza ziwe kati ya sentimita 30 – 40.

Anasema shughuli za uhamishaji na upanzi wa miche zinapaswa kutekelezwa siku yenye mawingu au majira ya jioni, wakati jua limepunguza makali ya miale.

Kauli yake inapigwa jeki na mtaalamu Njeri Murage, akihimiza kitalu kimwagiliwe maji kabla ya kung’oa mimea hiyo michanga.

“Hilo linasaida kutodhuru mizizi na kuepushia miche mzongo wa mshtuko,” aeleza mjuzi huyo.

Muhimu zaidi baada ya upanzi ni utunzaji kwa njia ya maji na mbolea ya kisasa au fatalaiza.

Shughuli nyingine muhimu kutilia maanani ili kudhibiti umeaji wa makwekwe ni kupalilia.

Makwekwe huleta ushindani mkali wa lishe; mbolea na maji.

“Mkulima anapaswa kuwa makini wakati wa kupalilia kwa sababu mizizi ya spinachi haina nguvu vile,” ashauri Bw Mwangi.

Ili kuzuia uvukizi wa maji, nyasi za boji zinaweza kutumika. Mfumo huo pia husaidia kuzuia ukuaji wa makwekwe, ikiwa ni pamoja na kuongeza rutuba udongoni nyasi zinapooza.

Nyasi zinazopaswa kutumika ni zilizokauka, kwa kuwa hazina wadudu.

Viwavi, viwavijeshi, vidukari,na sota, ni miongoni mwa wadudu sugu kwa spinachi. Dumping-off, root rot, leaf spot na downy mildew, ni magonjwa yanayoshuhudiwa kwa mboga hizo.

Wataalamu wanaonya kuwa upanzi wa spinachi eneo moja kwa muda mrefu huchangia kusalia kwa wadudu na magonjwa udongoni.

Ni muhimu kufanya mzunguko wa mimea, kwa kupanda maharagwe, maharagwe asilia, nyanya au viazi.

Spinachi huvunwa baada ya wiki sita au nane, zikiwa na majani sita, na kulingana na aina yake zinaweza kuvunwa hata zaidi ya miezi mitatu.

Wakati wa mahojiano, mkulima Mwangi alisema robo ekari humpa wastani wa kilo 600 kila wiki.

Wateja wake ni wa kijumla, na kilo moja hununuliwa kati ya Sh15 – 25. Hata hivyo, wakati zimesheheni sokoni, hushuka hadi Sh6 kwa kilo, bei anayosema hukandamiza wakulima.

You can share this post!

‘Mvua iliyopitiliza kiwango kuendelea kunyesha hadi...

Pengo katika ofisi ya msimamizi wa bajeti laathiri serikali...

adminleo