• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Dada 2 wakiri kuua baba yao kuhusu pesa za mazishi

Dada 2 wakiri kuua baba yao kuhusu pesa za mazishi

Na MWANDISHI WETU

DADA wawili wa toka nitoke Ijumaa walikiri kwamba walimuua baba yao wakizozania pesa za mazishi ya ndugu yao.

Hii ni baada ya kukaa rumande kwa miezi mitatu wakikabiliwa na mashtaka ya mauaji,

Emily Wanjira Mwangi, 24 na dadake Esther Kagendo Mwangi, 28, walikiri shtaka la kuua baba yao Zachary Kiura Mutindi bila kukusudia mbele ya Mahakama Kuu ya Embu mnamo Ijumaa.

Wawili hao walishtakiwa pamoja na mama yao Tabitha Weruma ambaye alikanusha mashtaka hayo mbele ya Jaji Florence Muchemi.

Dada hao wawili waliomba korti kuwapa kifungo cha nje kwa kuwa ndio wameachwa kulinda familia kufuatia kifo cha baba yao huku mama yao akizuiliwa gerezani.

Bi Kagendo na Bi Wanjira walieleza mahakama kwamba, walijutia kumuua baba yao.

Awali, walishtakiwa kwa kumuua Bw Mutindi lakini mnamo Oktoba 16, 2019 shtaka lilibadilishwa na kuwa la kuua bila kukusudia.

Jaji Muchemi aliagiza upande wa mashtaka kuwasilisha ripoti kuhusu tabia yao kabla ya kuhukumiwa Disemba 16, 2019.

Ilidaiwa kuwa walimshambulia marehemu mnamo Septemba 7, 2019, nyumbani kwao katika kijiji cha Kathita, Kaunti ya Embu.

Taarifa ya kesi inaeleza Bi Weruma alivyochukua pesa zilizochangishwa na wasamaria wema ili kusaidia katika mazishi ya mtoto wao mwenye umri wa miaka 19, aliyefariki baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Mshukiwa alieleza korti jinsi mumewe alivyotoweka nyumbani kwa siku tatu na kurejea bila hela.

Alisimulia jinsi ugomvi ulivyozuka alipomuuliza mumewe kuhusu pesa na kisha akawapigia simu binti zake wawili waliokuwa wakiishi katika kijiji cha Kathoge, Kirinyaga.

“Tulijawa na ghadhabu kwa sababu bado tulikuwa tunamwomboleza kaka yetu ilhali baba yetu alitumia pesa zote ulevini,” dada mmoja alieleza mahakama.

Bw Mutindi alifariki kutokana na majeraha mnamo Septemba ambapo mwili wake ulipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Embu Level Five.

Mwili wake ulipofanyiwa upasuaji siku mbili baadaye, matokeo yalionyesha kwamba kifo chake kilitokana na majeraha kichwani yaliyosababishwa na kifaa butu.

Baba na mwanawe walizikwa siku moja huku mkewe na binti zake wawili wakikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji mnamo Oktoba 16, 2019, kufuatia uchunguzi.

You can share this post!

Pengo katika ofisi ya msimamizi wa bajeti laathiri serikali...

Ngilu kulipa nusu milioni kwa kupotosha seneti

adminleo