Ngilu kulipa nusu milioni kwa kupotosha seneti
Na CHARLES WASONGA na DAVID MWERE
GAVANA wa Kaunti ya Kitui, Charity Ngilu, atalazimika kulipa Sh500,000 kama faini kwa kuwasilisha habari kwa kutumia uongo mbele ya kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu na Uwekezaji (CPAIC).
Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Homa Bay, Moses Kajwang’ ilimtoza Bi Ngilu faini hiyo baada ya kubaini kuwa stakabadhi alizowasilisha mbele yake zilikuwa na habari za kupotosha kuhusu matumizi ya fedha katika kaunti ya Kitui katika mwaka wa kifedha wa 2017/2018.
Aidha, aliwasilisha kuchelewa stakabadhi hizo zilizoonyesha kuwa tangu alipoingia afisini baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017, kaunti hiyo ilikuwa imetumia angalau Sh18 bilioni katika miaka miwili ya kifedha.
Kulingana na sehemu ya 62 (1) (c) and (d) ya Sheria ya Ukaguzi wa Umma, (Public Audit Act) ni hatia kwa yeyote kuwasilisha habari za kupotosha, kimakusudi, kwa lengo la kupotosha Afisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.
Na atakayevunja sheria hiyo anaweza kupewa adhabu ya faini Sh5 milioni au kifungo cha miaka mitatu gerezani.
Bw Kajwang’ alimwamuru Ngilu kutumia pesa zake kulipia faini hiyo ya Sh500,000 wala sio pesa za serikali ya kaunti ya Kitui “kwa sababu hili ni kosa lako mwenyewe”
Bi Ngilu anatarajiwa kulipa pesa hizo katika afisi ya karani wa Seneti Bw Jeremiah Nyengenye.
“Hatutawaruhusu magavana kuendelea na mtindo huu mbaya wa kuwasilisha stakabadhi dakika za mwisho ilhali wanapaswa kufanya hivyo wiki moja kabla ya kufika mbele yetu. Kitendo cha Ngilu na serikali yake kinaonyesha kuwa alipanga sio tu kuhadaa kamati hii, bali pia alitaka kukwepa kuhojiwa,” akasema Bw Kajwang’.
Kufuatia hatua hiyo, Bi Ngilu sasa anajiunga na orodha ya magava Mike Sonko (Nairobi) na Salim Mvurya (Kwale) ambao pia wamewahi kutozwa faini na kamati hiyo ya CPAIC kwa kudinda kufika katika vikao vyake.
Lakini mara tu baada ya kamati ya Seneta Kajwang kutoa uamuzi huo, Bi Ngilu aliupinga na kusema atakata rufaa kwa sababu hakupewa nafasi ya kuwasilisha barua kutoka kwa afisi ya karani wa Seneti ikionyesha kuwa serikali yake iliwasilisha stakabadhi hitajika mapema.
Gavana huyo alikosoa hatua ya kamati hiyo dhidi yake akisema haikufaa na kwamba ilitolewa kwa nia mbaya.