MWANASIASA NGANGARI: Wakili aliyetetea kundi la Maumau bila ya malipo
Na KEYB
ALIKUWA shujaa halisi wa harakati za kupigania uhuru wa taifa la Kenya.
Kujitolea kwake, ukakamavu na ujasiri wake ni kielelezo bora kwa vijana wa enzi hizo na hata wa nyakati hizi.
Huyu sio mwingine ila ni mwanasiasa ngangari tunayemuangazia juma hili, C. M. G Argwing-Kodhek ambaye ndiye mbunge wa kwanza wa Gem aliyehudumu kuanzia taifa hili lilipopata uhuru 1963 hadi 1969.
Herufi CMG katika jina lake zilimaanisha; Chiedo Moa Gem (yaani aliyekaangwa kutoka Gem). Alipewa jina hilo la wazazi wake kama kumbukumbu ya mababu zao. Alitumia jina hilo katika ulingo wa siasa kuvutia ufuasi.
Kando na hayo marehemu Argwings-Kodhek ni miongoni mwa mawakili wa kwanza wa asili ya Kenya ambaye alisomea uanasheria nchini Uingereza. Alikuwa katika tapo aliyokuwa Mkuu wa Sheria Charles Njonjo na aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge na Mbunge wa Tinderet (kati ya 1963 na 1975) Jean Marie Seroney.
Alifanya kazi ya uwakili jijini Nairobi mapema miaka ya 1960s, akiegemea nyanja ya haki za kibinadamu.
Hii ndio maana utawala wa ukoloni ulimchukulia kama “a hot head” (kichwa moto) kutokana na uanaharakati wake huku akiwatetea wapiganiaji wa kundi la Mau Mau kama vile Waruru Kanja, miongoni mwa mibabe wengine.
Ni wakati huo, akiendesha kazi yake ya uwakili na uanaharakati, jijini Nairobi ambapo alijiunga na siasa na hatimaye akabuni chama cha kisiasa cha Nairobi Congress Party. Chama hicho kilishindana na kile cha Nairobi People’s Convention Party, kilichoasisiwa na marehemu Tom Mboya.
Kenya ilipopata uhuru mnamo 1963, Waziri Mkuu Jomo Kenyatta alimteua Argwings-Kodhek kuwa Waziri Msaidizi wa Ulinzi. Na mnamo 1966, alipandishwa cheo kuwa Waziri wa Mali Asili na hatimaye mnamo 1967 aliteuliwa kuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni.
Argwing- Kodhek alizaliwa mnamo 1923 katika kata ya Malanga, eneobunge la Gem, wilaya ya Siaya, (sasa kaunti ya Siaya).
Alisomea katika shule ya upili ya St Mary’s Yala na kisha akajiunga na Chuo cha King’s College Budo, Uganda. Anatoka ukoo wa Kagola Ojuodhi ambayo pia ndio anatoka aliyekuwa mbunge wa Gem Isaac Omolo Okero (kuanzia 1969 hadi 1979). Huo pia ndio ukoo wa msomi mashuhuri Profesa Bethwel Allan Ogot, mumewe Grace Ogot ambaye alihudumu kama mbunge wa Gem kati ya 1985 hadi 1992.
Baada ya kuhitimu kutoka chuo cha Budo, Argwing-Kodhek alifunza katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Kapsabet, ambako alikutana na Rais mstaafu Daniel Moi. Ni baada ya hapo ambapo alipata udhamini kwenda kuwa masomo ya juu nchini Uingereza, ambako alitakiwa kusomea taaluma ya ualimu. Hata hivyo, alivutia na kozi ya uanasheria ambayo serikali ya ukoloni haikutaka asomee. Kwa hivyo, baada ya mwaka mmoja, udhamini wa masomo aliopewa ulikatizwa..
Hii ilimlazimu babake kuuza mifugo wake ili kugharamia karo yake aweze kusomea shahada ya kwanza katika uanasheria. Baada ya kuhitimu kama wakili akaanza kuhudumu kama wakili katika kituo cha Lincoln Inn ambapo alikuwa akipokea mashahara mzuri.
Lakin siku moja aliwashangaza wenzake, alipowajulisha kwamba angetaka kurejea nyumbani, Kenya. Baada ya kurejea nyumbani Argwings- Kodhek, almaarufu CMG, aliajiriwa na serikali ya mkoloni kama mshauri wa masuala ya sheria katika afisi ya Msajili Mkuu ambako alifanyakazi pamoja na Njonjo, Seroney na Mareka Gecaga.
Baada ya mwaka mmoja, CMG alijiuzulu kazi hiyo na kuamua kuhudumu kama wakili wa kundi la Mau Mau, kazi aliyofanya kwa malipo duni au nyakati zingine bila malipo.
Ni kutokana na kazi ambapo alichukiwa na serikali ya mkoloni lakini watu weusi walimwona kama shujaa ambaye aliweza kuondoa dhana iliyoendelezwa na Wazungu kwamba Waafrika walielewa tu kazi za sulubu.
Na Wazungu walimchukia zaidi kwa sababu CMG alikuwa ameoa mke wa asili ya Kizungu.
Katika Kongamano la Lancaster House katika miaka ya 1960 na 1962, alikuwa ni mmoja wa wanasheria ambao waliwaelekeza wajumbe kutoka Kenya kusudi wasihadaiwe na wakoloni.
Mbinu moja iliyotumiwa na serikali ya mkoloni ilikuwa ni ile ya gawanya utawale. Nchini Kenya, waliendeleza sera ya kugawanya nchi kwa misingi ya kikabila. Hii ndio maana mnamo 1956 Argwing-Kodhek alipoanzisha chama cha kitaifa serikali ilipitisha sheria ambayo iliwaruhusu Waafrika kubuni vyama vya ngazi ya wilaya pekee.
Wakati wa mapambano ya uhuru wa taifa hili, Bw Argwing-Kodhek pamoja na Achieng Oneko na Paul Ngei ndio walikuwa ni watu wasio wa kabila la Agikuyu ambao walishirikiana moja kwa moja na kundi la Mau Mau.
Na hii ndio maana Rais Kenyatta aliwateuwa watatu hao katika baraza lake la kwanza la mawaziri mnamo 1963.
Katika siasa, waliomuenzi Kodhek walimtaja kama mtu aliyekirimiwa sifa ya uanadiplamasia. Hata hivyo, alidhihirisha sifa nyingine ya umahiri katika mijadala bungeni. Hii ni kwa mujibu wa kumbukumbu za bunge, maarufu kama Hansard wakati wa mjadala mkali kuhusu majukumu ya serikali kuu na serikali za majimbo.
Argwing-Kodhek ambaye wakati wa mjadala huo alikuwa Waziri Msaidizi wa Mali Asili akasema: Mheshimiwa Spika, ingawa wabunge wa upinzani wamefurahi wengi wao wamepiga kura ya “La” kwa sauti kubwa kwa kasuku, inasikitisha kwamba watu kama hao ambao wamechaguliwa na raia hawaoni aibu kupotosha umma kuhusu Katiba ya Kenya.
“Tunataka kujenga taifa: taifa moja. Hali hili linacheleweshwa na wabunge wa upinzani ambao hawaelewi wajibu wao,”
Vilevile, Argwings – Kodhek alikuwa ni mwanasiasa ambaye alichukia ukabila. Hii ndio maana nyakati zote alihubiri amani na umoja miongoni mwa makabila ya magharibi mwa Kenya, haswa Waluo na Waluhya.
Mnamo 1966, Jaramogi Oginga Odinga alipogura Kanu na kuunda chama cha Kenya People’s Union (KPU), tofauti na wanasiasa wengine kutoka Luo Nyanza, Kodhek aliamua kusalia katika chama hicho tawala.
Hii ndio maana Rais Kenyatta alimdumisha katika baraza lake la mawaziri ambapo kati ya 1967 na 1969 alihudumu kama Waziri wa Masuala ya Kigeni. Alifariki mnano 1969 gari lake lilipohusika katika ajali ya barabarani katika eneo la Kilimani, Nairobi.
Hadi wakati huu, barabara ambako tukio hilo lilitokea lilipewa jina lake. Argwings-Kodhek alifariki miezi michache kabla ya aliyekuwa mshindani wake kisiasa Tom Mboya kufariki katikati mwa jiji la Nairobi.
Mwanawe Kodhek Caesar anasema katika majawapo ya hafla za kumbukumbu ya kifo chake: “Sasa ni miaka 40 baada ya kifo cha babangu, taifa linafaa kutizama nyuma na kutafakari kuhusu namna alivyojitolea kupigania uhuru wa taifa hiyo kutoka minyororo ya ukoloni. Inapasa tuendeleza maadili ambayo baba yetu aliendeleza wakati wa uhai wake. Kama Wakenya, tuendelee kuwakumbuka mashujaa wetu.”
Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke