Wabunge wazima mpango wa kuwaongeza walinzi ujira
Na OTIATO GUGUYU
WABUNGE wamezima mpango wa kuwaongezea mishahara walinzi 500, 000 wa kibinafsi kwa kutupilia mbali kanuni mpya ambazo zingelazimisha kampuni za ulinzi kupandisha mishahara ya wafanyakazi hao kuanzia Januari mwakani.
Kamati ya bunge kuhusu sheria zinazotungwa na asasi za serikali, chini ya uongozi wa Mwakilishi Mwanamke wa Uasin Gishu, Bi Gladys Shollei, ilisema kuwa kanuni hizo zilizotayarishwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i zina kasoro.
Wanachama wa kamati hiyo pia walisema Dkt Matiang’i hana mamlaka ya kuunda kanuni hizo.Bi Shollei aliongeza kuwa umma haukuhusishwa kikamilifu wakati wa utayarishaji wa kanuni hizo kama inavyohitajika kikatiba.
Hii ni licha ya Katibu wa Wizara hiyo Karanja Kibicho kuiambia kamati hiyo kwamba wizara yake ilianza kuandaa kanuni hizo mnamo Machi 2016, baada ya Sheria kuhusu Walinzi wa Kibinafsi kupitishwa na kwamba, wadau wote katika sekta hiyo walihusishwa.
“Kamati hii inapendekeza kanuni hizi zifutiliwe mbali kutokana na sababu nyingi, ikiwemo kucheleweshwa kwa uchapishaji na uwasilishaji wa kanuni hizo bungeni.,” akasema Bi Shollei.
Endapo kanuni hizo zingepitishwa, maslahi ya walinzi wa kibinafsi yangeimarika kwa kiwango kikubwa kwani kampuni zilizowaajiri zingehitajika kuwaongezea mishahara.
Katika miji mikuu kama Nairobi, Mombasa na Kisumu, walinzi wa usiku wangetia kibindoni Sh27,993 kila mwezi huku wenzao wa mchana wakipokea Sh25,641.
Na katika miji yenye hadhi ya manispaa kama vile Nakuru, Nyeri na Kakamega, walinzi wa usiku wangepokea Sh25,905 na wale wa mchana Sh16,119.
Nao walinzi wanaohudumu katika maeneo mengine nchini wangepokea mashahara wa Sh13,575 kutoka Sh8, 567 wanazopokea wakati huu.
Hata hivyo, mapendekezo hayo yamepingwa na kampuni za ulinzi zinazodai kuwa haziwezi kumudu kulipa viwango hivyo vya mishahara.
Vyama vya Sekta ya Ulinzi Nchini (KSIA), kile cha Protective Industry Association na Protective and Safety Association of Kenya viliungana kuunda chama kwa jina Joint Security Industry Association kupinga kanuni hizo.