Rais ahukumiwa miaka 20 kwa mauaji ya wapinzani 15
NA AFP
RAIS Desi Bouterse wa nchi ndogo ya Surinam, Amerika ya Kusini, amehukumiwa miaka 20 gerezani kwa tuhuma za kuagiza mauaji ya wapinzani wake 15 wa kisiasa.
Uamuzi huo ulitolewa na majaji watatu mnamo Ijumaa. Kesi hiyo dhidi yake ilianza mnamo Novemba 2007 na haijabainika mara moja hatua itakayofuata baada ya hukumu hiyo.
Majaji hawakutoa agizo la kukamatwa kwa kiongozi huyo baada ya wakili wake, Bw Irvin Kanhai, kuwasilisha rufaa mara tu baada ya hukumu hiyo.Wakili huyo alikosoa vikali hukumu huyo, akiitaja kuwa “yenye msukumo wa kisiasa.”
Bouterse aliliongoza taifa hilo katika miaka ya themanini kama kiongozi wa serikali ya kijeshi, ambapo baadaye alitwaa mamlaka tena mnamo 2010.
Alichaguliwa tena kuhudumu kama rais kwa miaka mitano.Kwenye uamuzi wake, mahakama ilisema kuwa kiongozi huyo alitumia serikali yake kuwateka nyara wakosoaji 16, wakiwemo mawakili, wanahabari na wahadhiri wa vyuo vikuu ambapo 15 kati yao waliuawa katika jengo moja la kikoloni jijiji Paramoribo mnamo 1982.
Rais Bouterse, 74, yumo katika ziara ya kikazi nchini Uchina na hajatoa taarifa yoyote kuhusu uamuzi huo.
Kiongozi huyo alitarajiwa kurejea nchini mwake jana ama leo, kulingana na naibu kiongozi wa chama chake cha National Democratic Party (NDP) De Ware Tijd.
Muda mfupi baada ya mahakama kutoa uamuzi huo, serikali iliwaomba raia kuwa watulivu.
Nchi hiyo ina raia nusu milioni “Tunawaomba kuwa watulivu, kwani hiyo ndiyo maana kamili ya demokrasia ya kweli,” wakasema maafisa wakuu wa serikali kwenye taarifa.
Kiongozi mkuu wa upinzani Angelic del Castillo alisema kuwa kiongozi huyo anapaswa kujiuzulu kama rais wa nchi hiyo mara moja.
“Ili kudumisha hekima kwa afisi ya rais na nchi yetu, anapawa kujiuzulu,” akasema kwenye taarifa.
Mahakama hiyo pia iliwahukumu maafisa wengine sita wa zamani wa kijeshi, akiwemo balozi taifa hilo katika nchi ya Guyana.
Maafisa hao walikabiliwa na mashtaka ya mauaji na kuwahisha watu kutoka makazi yao kwa nguvu usiku.
Mnamo 1999, kiongozi huyo alihukumiwa kifungo kingine na mahakama moja nchini Uholanzi kwa tuhuma za ulanguzi wa mihadarati, ingawa alikana mashtaka hayo.
Kando na hayo, mahakama nyingine ilimhukumu mwanawe mnamo 2005 kwa madai ya kuongoza genge la ulanguzi wa mihadarati, uuzaji silaha na wizi wa magari ya kifahari.
Rais huyo alishiriki katika mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Waziri Mkuu wa kwanza Henck Arron, ambapo baadaye alijipandisha mamlaka mara moja kuwa kiongozi wa kijeshi.