BBI: Macho yote sasa kwa Ruto
Na WANDERI KAMAU
MACHO yote sasa yako kwa Naibu Rais William Ruto na kundi la Tangatanga kuhusu ikiwa hatimaye litabadili msimamo wake mkali dhidi ya ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) iliyozinduliwa Jumatano na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Kundi hilo limekuwa likitoa misimamo mikali dhidi ya ripoti hiyo, likiitaja kuwa njama ya kisiri ya Mabwana Kenyatta na Odinga kuzima nia ya Dkt Ruto kuwania urais mnamo 2022.
Imefichuka kuwa Dkt Ruto hakujumuishwa moja kwa moja kwenye shughuli nyingi za uzinzudi wa ripoti hiyo katika Jumba la Bomas, jijini Nairobi licha ya juhudi zake kuonyesha umoja na ushirikiano mzuri kati yake na Rais Kenyatta.
Dkt Ruto hakuonekana mchangamfu kama ilivyo kawaida yake, wadadisi wakisema kuwa hiyo ni ishara tosha huenda akaanza harakati za kuipinga.
Kando na hayo, waandani wake wa karibu walionekana kutengwa katika hafla hiyo, kiasi cha kuwakasirisha baadhi yao.
Wale walioalikwa kuhutubu ni wanasiasa wanaoegemea mirengo ya Kieleweke na ‘Team Embrace’ hali iliyozua ghadhabu kubwa miongoni mwa waandani wa Dkt Ruto.
Miongoni mwa waliohutubu ni ni magavana Anne Waiguru (Kirinyaga), Bi Gladys Wanga (Homa Bay) na Gavana Charity Ngilu (Kitui) ambapo wote ni wa kundi la ‘The Embrace.’
Upeo wa taharuki hiyo ulikuwa wakati Kiongozi wa Wengi katika Seneti Bw Kipchumba Murkomen aliamka kwa hasira na kudai kwamba kuna maonevu ya wazi dhidi ya wanasiasa wanaomuunga mkono Dkt Ruto.
“Mheshimiwa Rais, ningependa kueleza ukweli kwamba hafla hii imepangwa kwa kuwatenga watu ambao wamekuwa wakitoa maoni tofauti kuhusu ripoti hii. Lazima tuelezane ukweli. Ikiwa hatutasikizwa, basi itabidi tutoke nje kutoa sauti zetu kwa njia huru,” akasema Bw Murkomen, akionekana mwenye ghadhabu.
Kando na hayo, baadhi ya viongozi wa Tangatanga walisema kuwa walishangazwa na mpangilio mzima kuhusu hafla hiyo.
“Tulishangaa kukuta kwamba Naibu Kiranja wa Wachache Bungeni Junet Mohamed ndiye mratibu mkuu wa hafla hiyo. Hii ni ishara ya wazi kuna wanaopendelewa kwenye mchakato mzima wa maandalizi ya hafla hii,” akasema mbunge mmoja ambaye hakutaka kutajwa.
Wachanganuzi wanasema kuwa hiyo ni dalili kuwa Dkt Ruto bado hajashawishika na kauli ya Rais Kenyatta kwamba ripoti hiyo ni ya kuwaunganisha Wakenya, ila ni mpango wa kuzima nia yake kuwania urais.
“Dhana iliyopo hadi sasa ni kuwa BBI ni njama ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kuzima nia yake kuwania urais. Ingawa baadhi ya wanasiasa wanaoegemea mrengo wa Tanga tanga wameonekana kuonyesha dalili za kuunga mkono ripoti hiyo, hatima yake italingana na kauli ya mwisho watakayotoa,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi siasa.
Kwenye hafla hiyo, Dkt Ruto alionekana mwenye mawazo mengi, kinyume na Rais Kenyatta na Bw Odinga, walioonekama wachangamfu. Kwa wakati mmoja, waliangua vicheko huku Dkt Ruto akionekana kununa.
Kundi la Tangatanga limekuwa likidai kwamba litaipinga ripoti hiyo kwa kila namna, ikiwa haitazingatia matakwa ya watu wao, hasa kuhusu masuala ya kiuchumi.
Baadhi ya wanasiasa katika kundi hilo wameanza kuonekana kushusha misimamo yao mikali, kwa kusema kuwa “wataisoma na kutoa misimamo yao huru.”
Wale wameonyesha dalili za kubadili misimamo yao ni wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Rigathi Gachagua (Mathira), Seneta Susan Kihika (Nakuru), Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen kati ya wengine.
Dkt Ruto pia alitoa kauli kama hiyo, wachanganuzi wakisema kuwa muda ndiyo utakuwa mwamuzi mkuu kuhusu mwelekeo ambao kundi hilo litachukua.
Na kwenye hotuba yake, Dkt Ruto hakueleza moja kwa moja ikiwa anaiunga mkono ripoti, lakini alieleza kuwa “ataisoma kama Wakenya wengine.”
“Tutaisoma na kutoa msimamo huru bila shinikizo lolote. Hata hivyo, lazima tuhakikishe kuwa matakwa ya watu yamezingatiwa kikamilifu,” akasema Bw Nyoro, ambaye amekuwa mmoja wa wale ambao wamekuwa wakiipinga.
Licha ya hakikisho hilo, wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa ingali mapema kutabiri msimamo wa kundi hilo kuhusu ripoti hiyo kwani kama Dkt Ruto, wanasiasa wa ‘Tanga Tanga’ hawajatoa kauli za moja kwa moja kuonyesha ikiwa wataiunga mkono.
“Kauli zao zinaonyesha kuwa taharuki kubwa ingalipo kuhusu ripoti hiyo ambapo huenda ikazua migawanyiko zaidi ya kisiasa kuliko ilivyokuwa hapo mbeleni,” asema Bw Javas Bigambo, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.
Mbunge Moses Kuria (Gatundu Kusini) anasema kuwa hawataiunga mkono ripoti hiyo ikiwa haitatilia maanani changamoto zinazowakumba Wakenya.
Mabunge huyo mbishi anasema kuwa lazima ripoti itilie maanani masuala ya kilimo, hasa katika eneo la Mlima Kenya ambalo limekuwa likilalamika kusahaulika na Rais Kenyatta.
“Wakazi wetu wanataka suluhisho kwa changamoto zinazowakumba; si ripoti ambayo inaangazia mipango ya kubuni nyadhifa za kuwafaa watu wachache,” akasema Bw Kuria