Makala

MAZINGIRA NA SAYANSI: Watoto kucheza na mchanga ni hatari kwa afya zao

December 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na LEONARD ONYANGO

WATOTO wako wanachelewa kukua, hawafanyi vyema shuleni au wanapoteza fahamu bila sababu?

Huenda ‘wamerogwa’ na mchanga wa eneo unapoishi.

Wataalamu wa afya wanasema kuwa watoto wanaoishi katika maeneo yaliyo na ardhi iliyo na madini ya chuma aina ya ‘lead’ wako katika hatari kubwa ya kuathirika kiafya na kiakili.

Dalili nyingine za mtoto aliye na kiasi kikubwa cha madini ya lead mwilini ni kukosa hamu ya kula, kupoteza uwezo wa kusikia, upungufu wa damu na kukosa usingizi kati ya nyinginezo.

Madini ya lead husababisha kansa na maradhi ya figo.

Madini ya lead hupatikana ardhini na hutumika kutengeneza rangi ya kupaka nyumba na magari, vipodozi, mafuta ya magari, betri, mikufu kati ya vitu vinginevyo.

Shirika la Kutathmini Ubora wa Bidhaa nchini Amerika (FDA) linasema kuwa rangi ambayo inatumiwa na akina dada kupaka mdomo, maarufu lipstick, imetengenezwa kwa lead japo kwa kiwango cha chini kinachokubalika.

Madini hayo huingia mwilini kupitia chakula, maji, kupumua hewa nakadhalika. Watoto wadogo ambao hawajazaliwa wanaweza kupata madini hayo hatari kutoka kwa mama kupitia kitovu.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Tulane cha nchini Amerika ulibaini kuwa watoto wanaoishi katika maeneo yenye ardhi iliyo na lead wana kiwango kikubwa cha madini hayo kwenye damu yao.

Japo lead huathiri hata watu wazima, watoto wako katika hatari zaidi kwani wao huchezea mchanga na hata kutia vitu vichafu mdomoni kila wakati.

“Kila mtu yuko katika hatari ya kuingiza madini ya lead mwilini lakini watoto wako kwenye hatari zaidi. Hii ni kwa sababu watoto huchezea mchanga na vitu vichafu wanapotangamana na mazingira,” inasema ripoti ya wataalamu hao.

Mnamo Februari 2018 Shirika la Kudhibiti Ubora wa Bidhaa nchini (Kebs) lilipiga marufuku kuingizwa humu nchini rangi iliyo na viwango cha juu vya madini ya lead.

Kenya ilikuwa nchi ya nne barani Afrika kupiga marufuku uuzaji wa rangi iliyo na kiwango kikubwa cha lead, baada ya Afrika Kusini, Cameroon na Tanzania.

Kenya ni miongoni mwa mataifa yaliyotia saini mkataba wa kimataifa unaolenga kuhakikisha kuwa rangi iliyo na lead inapigwa marufuku kufikia Desemba mwaka ujao.

Watoto wadogo hawajui ni vitu vipi havifai kuliwa. Wanaweka mdomoni kila kitu wanachoshika mkononi hata bidhaa zilizotengenezwa kwa lead kama vile rangi au vipodozi,” inasema ripoti ya watafiti wa Chuo Kikuu cha Tulane.

Nchini Amerika, madini ya lead yametajwa kuwa kisababishi kikubwa cha maradhi ya moyo.

Madini ya lead hushambulia ubongo na kusababisha watu kupoteza fahamu mithili ya waathiriwa wa kifafa.

Tafiti ambazo zimefanyiwa Wanyama zimeonyesha kuwa madini hayo yanaweza kusababisha maradhi ya kansa.

Madini ya lead huathiri sehemu za ubongo ambazo hutumika katika kufanya maamuzi na kudhibiti hasira na furaha.

Madini hayo hupita kwa urahisi ndani ya misuli inayokinga ubongo dhidi ya sumu.

Lead inapoingia kwenye ubongo huathiri mishipa inayopitisha taarifa kutoka kwenye ubongo hadi katika maeneo mengineyo ya mwili.

Madini hayo pia huathiri sehemu ya ubongo ambayo hutumika katika kujifunza mambo mapya na kuhifadhi kumbukumbu.

Viwango vya lead huwa vya juu karibu na barabara zenye shughuli nyingi na maeneo ya mijini.

Watafiti wa Chuo Kikuu cha Tulane walipima viwango vya lead katika mchanga kwenye eneo la New Orleans kati ya 2001 na 2017.

Watafiti pia walikusanya na kupima sampuli za damu ya watoto kila baada ya miaka mitatu.

Walibaini kwamba watoto wanaoishi katika maeneo yaliyo na kiwango kidogo cha lead walikuwa na kiwango kidogo cha madini hayo kwenye damu.

Damu ya watoto wanaoishi katika maeneo yaliyo na kiwango cha juu cha lead, ilikuwa imesheheni madini hayo.

“Katika utafiti wetu tumebaini kwamba ardhi inachangia katika watoto kuwa na madini ya lead mwilini,” wakasema watafiti hao.

Kuvalishwa viatu

Kupunguza hatari ya kuingiza madini ya lead mwilini, Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri kwamba wazazi wazuie watoto kuchezea mchanga mara kwa mara na wavalishwe viatu wanapotembea nje.

Maji yanayotoka kwenye mifereji iliyotengenezwa kwa lead yasitumiwe katika kupika au kunywa.

Shirika la WHO pia linashauri kuwa mikono ya watoto ioshwe mara kwa mara ili kuepuka kuweka mdomoni vitu vichafu vilivyo na chembechembe za lead.

Mazingira ya nyumbani yasafishwe ili kuepuka vumbi ambalo husheheni chembechembe za madini ya chuma.

Usihifadhi pombe aina ya waini, spiriti ndani ya vyombo vilivyopakwa rangi iliyo na lead kwani inaweza kuchujuka na kuingia ndani ya mvinyo.

Kulingana na WHO, watoto wanafaa kupimwa kiwango cha lead ndani ya damu yao mara kwa mara ili waweze kutibiwa.

“Hata kiwango kidogo cha lead ndani ya damu ya mtoto kinaweza kuathiri ubongo wake na kumfanya kushindwa kuelewa masomo darasani,” linasema shirika la WHO.