• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Jinsi dhana zilivyotumiwa katika methali za Kiswahili

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Jinsi dhana zilivyotumiwa katika methali za Kiswahili

Na ENOCK NYARIKI

KATIKA kuunda methali za Kiswahili, dhana ziliteuliwa kwa makini ili kutilia mkazo ujumbe fulani uliokusudiwa.

Katika makala haya nitaziangazia dhana mtambuko katika methali za Kiswahili na zile ambazo zilitumiwa kwa njia finyu.

Nimelitumia neno ‘mtambuko’ hapa kwa maana ya dhana ambazo hazikuchipuza wala kujikita katika mazingira fulani maalumu. Hapa tena nimeitumia kauli ‘mazingira maalumu’ kusudi kwa sababu kila methali imechipuza katika mazingira ya aina fulani ila kuna zile dhana ambazo zilipotumiwa katika baadhi ya methali, kila jamii iliweza kujinasibisha nazo.

Aidha, kunazo dhana ambazo jamii fulani bali si nyingine ndizo ziliweza kujinasibisha nazo. Sababu ni kwamba, dhana hizo zimekumbatia utamaduni wa jamii husika. Ikumbukwe kwamba, methali haziwezi kutengwa na utamaduni wa jamii ambamo zimechipuka. Hapo juu tumeitumia kauli ‘kila jamii’ kwa maana ya jamii zinazopatikana katika mazingira ya Afrika na ambazo methali za Kiswahili zilitumiwa kuumulika utamaduni wake. Jambo hili lina maana kuwa kuna methali ambazo zinafungamana sana na mazingira ya kigeni. Tutalijadili suala hili katika makala yatakayofuata.

Tutaanza uchambuzi huu kwa kuangazia methali zilizozitumia dhana kimtambuko kisha tutaonyesha visawe vya methali hizo na jinsi visawe vyenyewe vilivyojikita katika mazingira maalumu.

Jambo moja ambalo litajibainisha wazi katika mjadala huu ni kuwa, methali ambazo ni visawe vya zile tutakazoziangazia zimetumia msamiati maalumu unaoakisi utamaduni wa jamii ambamo kwamo zimechipuka. Iwapo kujitokeza kwa visawe hivyo katika jamii hizo ni jambo lililokusudiwa au la kisadfa tu ni suala tutakalolijadili baadaye.

Mgonjwa haulizwi uji

Dhana tutakayoiangazia hapa ni ‘uji’. Katika kuiangazia dhana hii, tutaongozwa na swali lifuatalo: kwa nini “uji” wala si kinywaji kingine chochote kile kilichopatikana katika mazingira ya Afrika mathalani chai? Kwanza, uji ni kinywaji cha Kiafrika ambacho kimekuwapo tangu jadi. Kwa hivyo, matumizi ya dhana hiyo katika methali yenyewe yanaelekea pia kutuonyesha ujadi wayo.

Kabla ya kubuniwa kwa vinu vya kisasa vya kusaga nafaka, Waafrika walitumia vinu na michi pamoja na mawe maalumu kusaga mtama au wimbi. Unga wa wimbi ulitumiwa kutengenezea uji ambao ulinywewa hususan wakati wa asubuhi licha ya kupikiwa ugali wa wimbi ambao ulikuwa maarufu katika sherehe zilizoandaliwa na Waafrika.

Jambo jingine muhimu sana na ambalo linaifanya dhana uji kutumiwa katika methali tuliyoitaja ni kuwa ndicho kinywaji ambacho kilitumiwa kuwanywesha wagonjwa au wagonjwa mahututi ambao wasingeweza kula chakula kingine chochote. Waafrika waliamini kuwa mgonjwa akishindwa kunywa uji, basi hiyo ilikuwa ishara kwamba asingepata nafuu.

Mojawapo ya sababu zilizozifanya baadhi ya jamii za jadi kuwang’oa watu wake meno mawili au matatu ya ufizi wa chini ni ili pengo lililoachwa mahali yalipong’olewa meno yenyewe litumiwe kumnywesha mtu huyo uji awapo mgonjwa mahututi. Alhasili, umaarufu wa uji ulitokana na mambo mawili. Kwanza, ulikuwa ni kinywaji cha Kiafrika kilichonywewa hasa wakati wa asubuhi. Pili, ulitumiwa kuwauguzia wagonjwa ambao wasingeweza kula chakula kigumu kwa sababu ya hali yao ya ugonjwa.

Maiti haulizwi sanda

Methali ‘Mgonjwa haulizwi uji’ ni kisawe cha ‘Maiti haulizwi sanda’. Ifahamike kuwa usawe wa methali hautokani na umbo la nje la methali zenyewe bali maana inayopitishwa nazo. Hakika, maana inayopitishwa na methali mbili tulizozitaja ni kuwa mtu yeyote aliye na shida fulani haulizwi namna ya kusaidiwa au kile akitakacho, badala yake husaidiwa tu.

Katika methali ‘Maiti haulizwi sanda’ tutaichambua dhana sanda na jinsi dhana yenyewe inavyofungamana na utamaduni ambamo imechipuka. Ijapokuwa baadhi ya kamusi za methali zinaeleza kuwa sanda ni kitambaa anachofunikwa maiti, hakika dhana hiyo ina uzito zaidi hasa inapojitokeza katika mazingira ya Kiislamu. Kulingana na utamaduni wa Waislamu, maiti hazikwi kwa jeneza bali huzikwa kwa sanda. Kwa hivyo, sanda ni nguo aghalabu ya rangi nyeupe anayovishwa maiti kabla ya kwenda kuzikwa kaburini.

Jambo moja ambalo siwezi kusema kwa yakini ni iwapo nguo nyeupe au vitambaa vyeupe ambavyo jamii nyingine huwavisha maiti kwavyo pia vinaweza kuitwa sanda. Hata hivyo, sanda ni neno linalojulikana sana katika mazingira ya Kiislamu licha ya kuwa mtambuko wa kimatumizi wa neno lenyewe umeanza kujitokeza katika jamii za Kiafrika hasa neno hilo lilipopanua maana kujumlisha pesa wanazopewa wafiwa…

 

ITAENDELEA

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Nina mume lakini namuwaza sana...

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana ya mtindo, sajili na...

adminleo