• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:47 PM
Gor Mahia yajikwaa Homeboyz, KCB wakiimarika

Gor Mahia yajikwaa Homeboyz, KCB wakiimarika

Na GEOFFREY ANENE

UONGOZI wa Gor Mahia wa alama sita juu ya jedwali la Ligi Kuu sasa umekatwa hadi nne baada ya mabingwa hao watetezi kudondosha alama mbili katika sare tasa dhidi ya Ulinzi Stars, wikendi.

Gor ya kocha Steven Polack ina jumla ya alama 25 baada ya mechi za raundi ya 12.

Mabingwa wa zamani Tusker walipunguza uongozi wa Gor baada ya kuzima Bandari 1-0 pamoja na kunufaika na sare ya vijana wa Polack.

Wanamvinyo wa Tusker, ambao wamesalia katika nafasi ya pili, wamevuna alama 21 kutokana na mechi 11. Wamesakata mechi moja zaidi ya Gor.

Kakamega Homeboyz na KCB wamerukia nafasi ya tatu na nne kwa alama 20 na 18, mtawalia. Hii ni baada ya Homeboyz kuzamisha washindi wa mwaka 2008 Mathare United 3-1 na kupaa nafasi tatu nayo KCB ililipua Kariobangi Sharks 5-2 na kupiga hatua sita mbele.

Mabingwa wa zamani Ulinzi wamekwamilia nafasi ya tano kwa alama 18. Wanazidiwa kwa tofauti ya ubora wa magoli na KCB. Ulinzi pia wako mbele ya washindi wa mwaka 2009 Sofapaka na wanaumeme wa Western Stima, ambao wanashikilia nafasi ya sita na saba mtawalia, kwa ubora wa magoli. Sofapaka na Stima walipaa nafasi moja kila mmoja baada ya kugawana alama katika sare ya 1-1 mjini Kisumu.

Posta Rangers ni ya nane kwa alama 17. Rangers ilitupwa chini nafasi tano kwa sababu haikuwa na mechi wikendi. Mabingwa mara 13 AFC Leopards almaarufu Ingwe wamekwamilia nafasi ya tisa kwa alama 17 baada ya kukabwa 2-2 dhidi ya Nzoia Sugar.

Mathare inafunga mduara wa 10-bora baada ya kichapo dhidi ya Homeboyz kufanya isukumwe chini nafasi sita. Timu ya Mathare iko nyuma ya Rangers na Ingwe kwa tofauti ya magoli.

Zoo Kericho

Zoo haijasonga kutoka nafasi ya 11 licha ya kujiongezea alama tatu muhimu baada ya kupepeta washiriki wapya Kisumu All Stars 3-0. Klabu hiyo kutoka kaunti ya Kericho ina jumla ya alama 13, mbili zaidi ya nambari 12 Wazito, ambayo ilimiminia Chemelil Sugar mabao 6-0 na kuimarika kutoka nafasi ya 14 hadi nambari 12. Wanasukari wa Nzoia, ambao hawajapata ushindi katika mechi sita mfululizo, wanafuata katika nafasi ya 13 kwa alama 10.

Bandari, ambayo inanolewa na kocha wa zamani wa Nzoia Sugar Bernard Mwalala, inapatikana katika nafasi ya 14 kwa alama tisa.

Vijana wa Mwalala wamevuna ushindi mmoja pekee katika mechi nane zilizopita ligini. Hawana ushindi katika mechi tano mfululizo.

Sharks na Kisumu zinasalia katika nafasi za 15 na 16 mtawalia kwa alama nane kila mmoja nayo Chemelil inavuta mkia kwa alama moja.

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Baada ya kutema mihadarati sasa amegeuka...

Onyo kali kwa wanaotumia watoto kuuza chang’aa

adminleo