Habari Mseto

Onyo kali kwa wanaotumia watoto kuuza chang'aa

December 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MISHI GONGO

MKURUGENZI wa kukabiliana na makosa ya jinai (DCIO) katika eneobunge la Changamwe mjini Mombasa Bw Josiah Jiro amewaonya wauza chang’aa dhidi ya kutumia watoto katika kufanya biashara hiyo haramu.

Akizungumza na Taifa Leo kwa simu, Bw Jiro alisema Jumatatu wafanyabiashara hao hutumia watoto kupeleka chang’aa hiyo kwa wateja ili kukwepa mitego ya maafisa wa polisi.

Mkurugenzi huyo wa polisi akishirikiana na afisa katika idara ya watoto Bw Philip Nzenge walisema hatua kali itachukuliwa dhidi ya wafanyabiashara hao ambao wanawaajiri watoto na kuwaweka katika hatari ya kuingililia ulevi wakiwa wangali wadogo kiumri pamoja na kuhatarisha afya zao.

“Wauza chang’aa katika eneo la Changamwe wamekithiri wakilinganishwa na wengine katika maeneo mengine. Ili kuepuka kukamatwa na maafisa wa polisi, baadhi ya wanawake wanawapa watoto pombe hiyo kufikisha kwa wateja,” Bw Jiro alisema.

Bw Jiro alisema tayari wamewakamata watu watano kuhusiana na makosa hayo.

Afisa katika idara ya watoto Philip Nzenge alisema kuruhusu watoto kufanya kazi katika vilabu vya kuuza ‘pombe za kienyeji’ kunawaweka katika hatari ya kunajisiwa na hata kushuhudia matukio ya ukosefu wa adabu.

“Mambo mengi maovu yanatokea katika vilabu vya pombe. Kuna walevi ambao huzua vurugu na kuanza vita, matusi na mambo mengi machafu ambayo hayafai kushuhudiwa na watoto,” alisema.

Kulingana na mkurugenzi huyo, baadhi ya mimba za mapema kwa watoto husababishwa na wao kuhudumu katika vilabu.

“Ni huzuni kubwa kuona watoto wadogo wanadanganywa na watu wazima kisha kuwatumia kimapenzi. Na hata baya zaidi ni kuwa watu hawa hawatumii kinga hivyo kuwaweka watoto katika hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa,” alisema.

Alisisistiza kuwa watahakikisha yeyote atakayedhulumu mtoto kimapenzi anachukuliwa hatua kali kisheria.