KCPE: Maelfu wavunjika moyo
OUMA WANZALA Na CHARLES WANYORO
MAELFU ya watahiniwa wa mtihani wa mwaka huu wa Darasa la Nane (KCPE), wamevunjika moyo baada ya kukosa nafasi katika kidato cha kwanza kwenye shule za upili walizokuwa wamechagua.
Kati ya watahiniwa waliokuwa wamechagua shule kubwa kubwa za kitaifa, ni elfu 33 pekee ambao ndoto zao zilitimia, kulingana na matokeo ya uteuzi yaliyotolewa jana na Waziri wa Elimu, Prof George Magoha.
Shule ya Pangani Girls jijini Nairobi ilipokea maombi mengi zaidi ya watahiniwa ambao wangetaka kujiunga nayo kwa jumla ya wanafunzi 110,835. Lakini ni 336 pekee walioweza kuitwa kujiunga na shule hiyo.
Alliance Girls nayo ilipokea maombi ya wanafunzi 92,067 lakini ingeweza tu kuchukua 384.
Kwa upande wa wavulana, Mang’u High ilipendelewa zaidi na wanafunzi kwa maombi 86,976 lakini ikaweza tu kuchukua 384 sawa na Alliance High iliyovutia jumla ya watahiniwa 81,943.
Shule zingine zilizovutia wanafunzi wengi ni Lenana School, Nairobi School, Starehe Boys, Maseno School, Kapsabet Boys, Maranda High, Kenya High, Limuru Girls, Mary Hill Girls na Nakuru Girls.
Waziri alisema uteuzi huo ulifanyika kwa njia ya uwazi na ulizingatia chaguo la mwanafunzi binafsi.
“Mwaka huu tuligundua kwamba wanafunzi wengi ambao walikuwa na uwezo wa kupata alama za juu walichagua shule chache tu ambapo ni vigumu kwa shule hizo kuchukua idadi yao wote,” akaeleza Prof Magoha.
Lakini watahiniwa walioandikisha alama za juu kwenye matokeo yaliyotangazwa wiki mbili zilizopita walitimiza ndoto zao kwa kuitwa kujiunga na shule walizokuwa wamechagua.
Mwanafunzi nambari moja kitaifa, Andy Munyiri aliyezoa alama 440 kati ya 500 atajiunga na Alliance High huku June Jeptoo aliyekuwa wa pili kwa alama 439 akiitwa akialikwa Pangani Girls.
Onyango Flavian, ambaye pia alipata alama 439, atajiunga na Alliance Girls.
Mwanafunzi wa nne bora kitaifa, Trevor Kipkoech atajiunga na shule ya upili ya Kapsabet katika Kaunti ya Nandi huku Delci Achieng wa shule ya Makini aliyeongoza katika Kaunti ya Nairobi akijiunga na shule ya upili ya Kenya High.
Derrick Kibiwott ambaye alifanya mtihani wake katika shule ya msingi ya Keplonik, Kaunti ya Nandi ameteuliwa kujiunga na shule ya upili ya Alliance huku Kimutai Caren Jerotich wa shule ya msingi ya Chugur, Elgeyo Marakwet akijiunga na shule ya wasichana ya Alliance.
Kulingana na Prof Magoha, watahiniwa wengine 184,816 watajiunga na shule za mikoa, 188,454 shule za kaunti na 669,145 watapata nafasi katika shule za kaunti ndogo.
“Idadi hii ni baada ya kuondoa wafungwa, wanafunzi wa ngumbaru na wakimbizi walioko kwenye kambi. Wote ambao wamepata nafasi za shule za upili wanawakilisha asilimia 100 ya mpito wa shule ya msingi hadi ile ya upili, chini ya sheria ya Kenya inayoruhusu kutolewa kwa elimu ya bure kwa kila mtoto,” akasema Prof Magoha.
Katika Kaunti ya Meru, mwanafunzi bora alieleza kuvunjika moyo baada ya kukosa mwaliko wa kujiunga na shule ya Mang’u, ambayo alikuwa amechagua ikiwa ya kwanza.
Mwanafunzi huyo, Roy Koome kutoka St Ann and Boarding Mission Primary School-Kariene, ameitwa Friends School Kamusinga baada ya kuzoa alama 433.
Lakini kwa watahiniwa wengine kutoka kaunti hiyo ilikuwa ni furaha baada ya kualikwa katika shule walizotaka. Hao ni Mbaabu Nick Kimathi (422) atakayejiunga na Alliance High, Kirianki Keith (421) Mang’u, Nia Lareto Kiara (419) Kenya High na Ringera Griffin Mugambi aliyeitwa Kagumo High.