• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Wakenya washauriwa kutumia baiskeli kama njia mbadala ya usafiri

Wakenya washauriwa kutumia baiskeli kama njia mbadala ya usafiri

Na MAGDALENE WANJA

WAKENYA wameshauriwa kutumia njia mbadala za usafiri ili kupunguza msongamaono wa magari pamoja na kuimarisha afya zao.

Njia hizi ni pamoja na kutembea – kwenda kwa miguu – na kutumia baiskeli.

Akizungumza jijini Nairobi, mkurugenzi mkuu wa wa UN-Habitat Bi Maimunah Mohd Sharif alisema Wakenya wengi hupoteza wakati mwingi katika misongamano ya magari kila siku.

Bi Sharif aliitaka serikali kutenga nafasi salama barabarani kwa waendeshaji baiskeli ili kuwapa watu nafasi ya kufika kazini mapema.

“Jiji la Nairobi linaweza kuwa la kuvutia sana iwapo barabara zitakuwa salama kwa waendeshaji baiskeli. Hali ya hewa ya Nairobi pia ni bora kwa uendeshaji baiskeli,” akasema Bi Sharif.

Kulingana na mamlaka ya usalama barabarani nchini (NTSA) magari 90,000 mapya huongezeka kila mwaka jijini Nairobi.

“Hii inasikitisha sana ukizingatiwa kuwa msongamano wa magari uliopo tayari ni mkubwa sana,” aliongeza Bi Sharif.

Hamasisho

Alizungumza baada ya shughuli ya kuwahamasisha watu wanaoishi mijini kutumia baiskeli kama njia mbadala ya usafiri.

Katibu mkuu katika wizara ya nyumba na maendeleo ya mijini Bw Charles Hinga alisema kuwa kanuni ya Kaunti ya Nairobi – NMT Policy – inatambua njia hizo mbadala za usafiri.

“Nairobi Integrated Urban Masterplan (NIUPLAN) ya mwaka 2014– 2030 tayari imebaini kuwa jijini Nairobi hakuna njia za kutosha za kutumika na waendeshaji baiskeli na wanaoenda kwa miguu,” alisema Bw Hinga katika taarifa iliyosomwa na Bw Michael Owino.

You can share this post!

Dereva wa teksi ashtakiwa kumbaka mteja na kuiba mali yake

Kauli za watoto kuhusu Krismasi

adminleo