Mahakama yaagiza serikali TZ kumuachilia Robert John Penessis
Na MAGDALENE WANJA
MAHAKAMA ya Afrika ya Haki za Watu – African Court on Human and Peoples Rights – imeiamuru serikali ya Tanzania kumuachilia mfungwa Robert John Penessis ambaye amekuwa jela kwa makosa ya “kuwa nchini humo kinyume cha sheria”.
Mahakama hiyo pia iliamuru serikali ya Tanzania kumlipa Penessis Sh10 milioni pesa za Tanzania, kwa kuzuiliwa kinyume cha sheria.
Serikali hiyo ilikuwa imemzuilia kwa madai kuwa hakuwa raia wa Tanzania na kuwa alikuwa na uraia wa nchi mbili ambazo ni Afrika Kusini na Uingereza.
Kufuatia madai hayo, alitozwa faini ya Sh80,000 ama kifungo cha miaka miwili kuanzia Januari 2010.
Mnamo Juni 2015 aliwasilisha ombi katika mahakama ya Afrika kwa madai kuwa serikali ya Tanzania ilikiuka haki zake za kibinadamu na kumzuilia kinyume cha sheria.
Katika ombi hilo, Penessis alidai kuwa yeye ni raia wa Tanzania kama wazazi wake.
Ombi hilo liliwasilishwa na nyanyake Bi Georgia J. Pennesis ambaye anaishi Ugiriki lakini ni mzaliwa wa Tanzania.
Mahakama hiyo ya Afrika pia imeamuru alipwe Sh300,000 za Tanzania kwa kila mwezi ambao alizuiliwa kinyume cha sheria.
Mahakama pia iliamuru mamake kulipwa Sh5 milioni za nchi hiyo kwa masaibu aliyopitia mwanawe alipokuwa korokoroni.