Asimulia mahakama alivyoleweshwa na kubakwa usiku kucha na dereva wa teksi
Na RICHARD MUNGUTI
DEREVA wa magari ya teksi alifikishwa mahakamani Jumatatu akishtakiwa “kumgeuza kitoweo” mteja wake pale alipomlewesha kisha akampeleka nyumbani kwake na kumbaka usiku kucha.
Sasa Shem Mokaya Nyakundi atasalia katika gereza la viwandani kuliwa na kunguni na chawa ambazo mahabusu huziita “Makamanda” na huwezi kuwaua hata wakikuuma kwa vile “utakuwa umewekea mkosi washukiwa wanaopelekwa kortini kuhukumiwa.”
Mokaya, ambaye ni kijana barobaro alifikishwa mbele ya hakimu mkazi mahakama ya Milimani Nairobi Bi Muthoni Nzibe na kukanusha mashtaka badala ya kumwimbia mteja wake simu yenye thamani ya Sh35,000.
Mshtakiwa kupitia kwa wakili wake aliomba aachiliwe kwa dhamana lakini “ombi hilo likapigwa kwa nguvu ya makurumbuti ya nyati na Inspekta Eunice Njue aliyepasua mbirika.”
“Naomba hii mahakama imzuilie mshtakiwa hadi Desemba 19 nikamilishe uchunguzi. Mbali na shtaka hili la wizi wa simu nitamfungulia shtaka la ubakaji.”
Insp Njue kutoka kitengo cha kuchunguza dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana alimweleza Bi Nzibe kuwa aliagizwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) achunguze hadi kwenye kina cha tukio hilo.
Afisa huyo alieleza mahakama kwamba uchunguzi aliofanya umebaini mshtakiwa alipigiwa simu Novemba 22, 2019 kumbeba mteja kutoka eneo la Lang’ata kaunti ya Nairobi ampeleke mjini Ruiru kaunti ya Kiambu.
“Lakini kumbe mshtakiwa alipomwona mlalamishi ambaye ni kidosho aliyeumbwa kaumbika alimlewesha na mtoto wa watu akapoteza fahamu,” Insp Njue alieleza mahakama.
Hakimu alifahamishwa mshtakiwa alimchukua mlalamishi kutoka nyumbani kwa rafikiye alipokuwa anahudhuria sherehe mwendo wa saa mbili usiku.
Alipopata ufahamu, mlalamishi alijikuta ndani ya nyumba katika mtaa wa Tassia eneo la Embakasi mnamo Novemba 23, 2019 akiwa hajihisi vyema.
Mlalamishi alikuta chupi yake imeteremshwa na ametendewa unyama.
“Mshtakiwa alimlazimisha mlalamishi kuoga mara mbili na kumpa nguo akabadilisha,” Insp Njue alimweleza hakimu.
Mlalamishi alimsihi mshtakiwa ampeleke kwao Ruiru lakini akakawia naye mtaani Tassia hadi mwendo wa saa 10 mchana.
Kabla ya kuondoka mlalamishi alisimamiwa akaoga ndipo wakafululiza hadi Ruiru alikoachwa karibu na kwao.
Mlalamishi alipiga ripoti kituo cha polisi cha Ruiru lakini akashauriwa apige ripoti kituo cha Polisi cha Embakasi ambapo tukio lilitendeka.
Mahakama ilifahamishwa mshtakiwa alipiga ripoti Embakasi lakini maafisa wakazembea kuchunguza kisa hicho.
Mlalamishi alishauriwa katika kituo cha Embakasi aende hospitali akapimwe kisha apewe cheti cha matibabu kufuatia malalamishi yake.
Mahakama iliombwa imzuilie mshtakiwa kwa vile anawatisha mashahidi pamoja na mlalamishi.
“Naomba nipewe muda hadi Ijumaa wiki hii kufika hospitali ya Nairobi Womens kupata ripoti ya matibabu ndipo nimfungulie shtaka la ubakaji,” Insp Njue.
Hakimu aliamuru mshtakiwa azuiliwe hadi Desemba 19,2019 korti itakapoamua iwapo ataachiliwa kwa dhamana au la.
Shtaka la wizi lilisema mnamo Novemba 22, 2019 katika mtaa wa Tassia aliiba simu yenye thamani ya Sh35,000.
Pia alishtakiwa kupatikana na mali aliyojua imeibiwa ama kupatikana kwa njia isiyohalali.