• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
KCB inavyojiandaa kwa kipute cha voliboli

KCB inavyojiandaa kwa kipute cha voliboli

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wanawake ya KCB inajiandaa kutifua vumbi kali kwenye kampeni za Voliboli ya Klabu Bingwa Afrika (CAVB) mwaka ujao.

Wanabenki hao wa kocha, Japheth Munala na David Kinga mara ya mwisho kushinda taji hilo ilikuwa mwaka 2006.

Kwenye mechi za kipute hicho mwaka huu zilizofanyika nchini Misri, wana dada hao walishindwa kufana na kumaliza nafasi ya tisa.

KCB ilimaliza ya tisa baada ya kupepeta Revenue Authority ya Rwanda seti 3-0 pale nahodha, Noel Murambi alipoongoza wenzake kutesa wapinzani wao na kunasa ufanisi wa alama za 25-15, 25-13, 25-11.

KCB ilijikatia tiketi ya mchezo huo ilipozoa seti 3-0 (25-10, 25-15, 28-0) mbele ya USFA ya Burkina Faso. Pia kwenye robo fainali za kuwania nafasi ya tisa KCB iliitandika Shooting ya Misri kwa seti 3-0.

”Bila shaka mwaka ujao tutakuwa tunalenga kujituma mithili ya mchwa ili kutwaa ubingwa huo,” makocha hao walisema.

Wachezaji wa KCB kabla ya kushuka dimbani kukabili Kenya Prisons katika fainali ya Ligi Kuu ya KVF muhula huu. Picha/ John Kimwere

KCB itashiriki kipute hicho kwa mara ya pili mfululizo baada ya kumaliza ya pili kwenye kampeni za Ligi Kuu ya KVF mwaka huu.

KCB iliyopania kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya KVF msimu huu iliteleza na kumaliza ya pili iliposhindwa kuhimili makali ya Kenya Prisons na kukubali kupigwa seti 3-0(25-22, 32-30, 25-22) katika fainali kali iliyopigwa Ukumbi wa Safaricom Arena, Kasarani.

KCB ilijikuta njiapanda licha ya wachezaji hao kuonyesha ushirikiano mwema kupitia juhudi za Noel Murambi na Ernestine Akimanizanye kati ya wengine.

Kwenye mechi za utangulizi Prisons ilizoa ushindi wa mechi mbili kwa seti 3-0 kila moja dhidi ya Pipeline na DCI. Nao wanabenki hao walikomoa DCI seti 3-0 na kuzoa idadi sawa na hiyo mbele ya Pipeline.

Kocha huyo alijiunga na KCB mwishoni mwa mwaka 2018 akiandamana na wachezaji saba wakitokea Pipeline.

Mchezaji wa KCB, Belinda Barasa arukia mpira walipocheza na Kenya katika fainali ya Ligi Kuu ya KVF muhula huu. Picha/ John Kimwere

KCB ilinasa huduma za wachezaji hao wanaoshirikisha wanavoliboli watatu ambao hupigia timu ya taifa maarufu Malkia Strikers.

Saba hao wakiwa Violet Makuto, Noel Murambi na Leoninda Kasaya. Wengine ni Jemima Siangu, Christine Njambi, Veronica Kilabat na Truphosa Chepkemei.

Baada ya kunasa saba hao pia iliachia idadi sawa na hiyo inayojumuisha Lucy Mumbo, Ruth Jelagat, Millicent Wanjala, Joyce Njeri, Stella Kawos, Everlyne Asiko na Lydia Too.

KCB na Kenya Prisons ndizo zitakaowakilisha Kenya kwenye mashindano hayo ya Klabu Bingwa Afrika (CAVB) kwa kina dada.

You can share this post!

RIZIKI: Kilimo kinamsaidia pakubwa

Wakenya wahimizwa kuvalia mavazi yaliyoundwa nchini

adminleo