• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
Viongozi waelezea umuhimu wa michezo katika utangamano

Viongozi waelezea umuhimu wa michezo katika utangamano

Na LAWRENCE ONGARO

VIONGOZI wamehimizwa kuepukana na siasa za kugawanya wananchi na badala yake wapigie chapuo utangamano miongoni mwa makabila yote.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alihimiza umuhimu wa michezo ambayo aliitaja chombo muhimu cha kuwaleta watu pamoja.

“Ni vyema kuiga ushabiki na ushiriki wa michezo ambayo kila mara huleta mashabiki pamoja bila ubaguzi wowote. Huu ndiyo uzalendo tunaotaka kwa wakati huu,” alisema Bw Wainaina.

Akaongeza: “Tumeona makabila tofauti kama Wajaluo, Wakikuyu na makabila mengine ambayo yanashirikiana pamoja michezoni bila kujali mtu anatoka eneo gani la nchi.”

Aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa michezo ya Copa Coca-Cola African Tournament katika M-Pesa Foundation Academy mjini Thika.

Wakati wa ufunguzi huo, mawaziri watatu walihudhuria na kutoa ahadi ya kuinua michezo ili vijana waweze kukuza talanta zao.

Mawaziri hao ni Waziri wa michezo Balozi Amina Mohamed, Waziri wa Masuala ya Jinsia na Vijana Profesa Margaret Kobia, na Waziri wa Elimu Prof George Magoha.

Fursa nzuri

Prof Kobia alisema vijana wana nafasi nzuri ya kuonyesha talanta zao kwa lengo la kuinua hali yao ya maisha.

“Serikali itafanya juhudi kuona ya kwamba kila kijana anapata nafasi yake mradi tu talanta yake itatambulika,” alisema waziri Kobia.

Waziri Amina alisema serikali ilitenga Sh5.3 bilioni kuendeleza michezo kote nchini huku akisema kuna talanta tele kutoka kwa vijana.

Prof Magoha alisema serikali itaendelea kutilia mkazo mfumo wa elimu wa uamilifu (CBC), kwa sababu unajumuisha mengi ya kumfaa mwanafunzi.

“Wakati huu hata talanta ya mwanafunzi itazingatiwa bila kubagua. Kwa hivyo wazazi wamehimizwa kuwapa mwongozo wana wao wakati kama huu wanapokuwa likizoni,” alisema Prof Magoha.

Mashindano hayo ya soka ya Copa Coca-Cola yanawaleta washiriki kutoka nchi tofauti kama Tanzani,a Msumbiji, Botswana, Uganda, Bukina Faso, na Angola.

Mwaka 2018 mashindano hayo yalifanyika mjini Nakuru ambapo vijana wa St Anthony Boys ya Kitale waliibuka washindi wa soka kwa wavulana.

Nao wasichana wa Moi Girls Nangili waliibuka washindi upande wa kina dada.

You can share this post!

City Stars yazidi kutetemesha Betika Supa Ligi

Gharama za juu za Intaneti nchini Uganda zawafungia wengi...

adminleo