Wetang’ula alia ODM inavuruga umoja Magharibi
Na SHABAN MAKOKHA
KINARA wa Ford Kenya, Moses Wetang’ula amewalaumu wafuasi wa ODM kutoka Magharibi mwa nchi kwa madai ya kutatiza kuunganishwa kwa chama chake na kile cha ANC cha Musalia Mudavadi.
Seneta huyo wa Bungoma amedai wafuasi hao wa Kinara wa ODM, Raila Odinga wamekataa kuunga mkono jitihada za jamii ya Waluhya kuungana ndani ya chama kimoja.
Alisema matumaini yaliyosalia kuishawishi ya muungano ni majadiliano wanayoendelea nayo na Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya ili kumshawishi aungane nao na kutoa mwaniaji moja wa urais 2022.
“Tunaendelea kuandaa mazungumzo na Oparanya ili ajiunge nasi na kuwaleta pamoja watu wa Magharibi. Sisi watatu tukiungana, basi tutakuwa na nafasi nzuri ya kumteua moja wetu kupeperusha bendera ya urais 2022,” akasema Bw Wetang’ula.
Alieleza masikitiko kwamba jamii hiyo imekuwa ikiwaunga mkono wawaniaji wa urais kutoka jamii zingine ambao wanapotwaa mamlaka huisahau.
“Tumewasaidia watu wengi kupata mamlaka na baadhi wamekuja kutushukuru ilhali wengine wamekuwa wakitupiga teke na hata kutuondoa kwenye nyadhifa muhimu. Wakati umewadia ambapo sisi kama jamii lazima tuweke mbele maslahi yetu kabla ya kuwaunga mkono watu kutoka nje,” akasema.
Hata hivyo, kauli ya Bw Wetang’ula imeshutumiwa vikali na baadhi ya wakazi ambao wanasema tabia ya viongozi wa jamii hiyo kukubali kutumiwa kwa maslahi yao wenyewe ndio imewafanya wasalie imara nyuma ya Bw Odinga.
“Viongozi wetu hushawishiwa kwa pesa na kutumiwa kutenganisha jamii,” akasema mkazi wa eneobunge la Matungu, Bw Fadhil Eshikwekwe.