Kamwe hatuwezi kutoza ushuru kwa mahari – KRA
Na MARY WANGARI
MAMKALA ya Kukusanya Ushuru (KRA) imelazimika kukanusha madai kwamba ilikuwa na mipango ya kuanza kutoza ushuru kwa wanaopokea mahari.
Mamlaka hiyo iliandika katika mtandao wa Twitter ikijitetea dhidi ya madai hayo, ambayo tayari yalikuwa yamepingwa vikali na Wakenya.
“Hii stori hata sisi tumeisikia,” KRA ilichapisha katika ukurasa wake huku ikitaja ripoti hizo kama habari feki.
Awali, ripoti zilienezwa mitandaoni kuwa KRA ilikuwa imeafikia uamuzi wa kutoza ushuru wa mahari baada ya kushindwa kutimiza kiwango cha ushuru ilichohitajika kukusanya.
“Uzuri mumefafanua. Nilikuwa nishaanza kujipanga tulete mbuzi katika ofisi zenu,” aliandika Gakunga.
“Niliona habari hizi mapema asubuhi. Ahsante kwa kufafanua kuwa ni feki. Nilikuwa ninashangaa tu ikiwa ingetekelezwa basi kila bwana harusi moja kwa moja angekuwa ajenti wa kukusanya ushuru. Nikilipa mbuzi 10 naleta mmoja Times Tower,” Stano Mwasi akasema.
Baadhi ya Wakenya walifahamisha mamlaka hiyo kwamba vijana tayari wamelemewa na maisha, na hivyo hawakuhitaji mzigo mwingine wa ushuru.
“Msijaribu kutupima! Waambieni viongozi wenu kuwa Wakenya ni takriban milioni 47 na nyinyi hamfiki watu 1,000. Wasitubebe ujinga! Vijana wanashindwa kuoa kutokana na hali ngumu ya maisha halafu mnataka kuleta ushuru mwingine. Tunawaona!” akasema Maryam Omar.
Hata hivyo kuna wengine waliosisitiza kwamba KRA ilikuwa kweli imetoa tangazo hilo, lakini ikabadili nia haraka baada ya kuona hisia za Wakenya.
“Semeni tu mmeogopa. Mlijaribu kuweka miguu majini mkaona ni baridi sana,” alisema Omar Bamzer.
Kwa uhalisia, inaweza kuwa vigumu kwa KRA kutoza ushuru wa mahari, ikizingatiwa kuwa wanaooana hawana mitambo ya kielektroniki (ETR), ambayo hutumika kuweka ithibati ya malipo.