• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
KIKOLEZO: Kuzirai stejini, inakuwaje?

KIKOLEZO: Kuzirai stejini, inakuwaje?

Na THOMAS MATIKO

WIKENDI iliyopita kulikuwa na sherehe kibao mjini Nairobi, viunga vyake na pia miji mingine hapa nchini.

Pale Bomas of Kenya, kulikuwa na Koroga Festivals, Kanda Bongo Man na Mbilia Bel wakifanya yao. Kwenye mgahawa wa Dari mtaani Karen ilikuwa ni Nairobi Cocktail Festivals.

Katika Chuo Kikuu ch Nairobi kulikuwa na Infinix Beat ya Campo. Mjini Thika ikawa ni Tusker Lite Neon Rave Party, halafu Kisumu kulikuwa na Luo Festivals.

Yaani ndio msimu wa Krismasi ulivyoanza kwa fujo. Sasa katika pilka pilka za shehere zote hizo, kule Kisumu kulitokea tukio moja ambalo liliwafanya wengi kupaniki. Msanii Akothee akitumbuiza jukwani mara ghafla alizimia na kudondoka.

Kwa bahati nzuri walikuwepo watu karibu naye waliompa huduma ya kwanza na akaweza kurejelea fahamu zake.

Lakini Akothee sio msanii wa pekee kudondoka stejini na kuzirai. Wapo kibao tu, na baadhi yao, haikuwaendea poa.

AKOTHEE (Luo Festivals, Kisumu 2019)

Akiwa stejeni majira ya saa saba hivi, akiwatumbuiza mashabiki huku akipewa sapoti na FBI Dancers, ghafla Akothee alipoteza fahamu na kudondoka sakafuni, mic mkononi.

Kwa bahati nzuri Madam Boss hakuumia sababu wale madansa wa FBI waliokuwa nyuma yake, walimwahi kipindi akiwa anadondoka na kumlaza kabla ya kumpa huduma ya kwanza na kisha kumwondoa ukumbini.

Akothee hakuweza kuendelea na utumbuizaji. Meneja wake Nelly Oaks akizungumzia tukio hilo la Jumamosi iliyopita, alisema mwanamuziki huyo alijipata katika hali hiyo kutokana na uchovu mkubwa aliokuwa nao.

“Kwa sasa anapumzika. Kuzirai huko kulichangiwa na uchovu ambao ni hivi majuzi tu ulimpelekea kulazwa hospitalini,” Oaks alisema.

Kabla ya tamasha, Akothee alikuwa amelazwa hospitalini kwa siku tano hapo awali kutokana na kile madaktari walikitaja kuwa uchovu. Baada ya kuruhusiwa kuondoka hospitalini, alianza kujiandaa kwa shoo hiyo ya Kisumu.

LAVA LAVA (Wasafi Festival, Morogoro 2018)

Ilikuwa ni kwenye tamasha moja alilokuwa akitumbuiza kule Morogoro. Sasa akiwa stejini mara ghafla alipanda demu jukwani na akaanza kudensi nae huku anaimba.

Yule dada akiona hamna tatizo kama akimpiga busu supastaa na mara boom, midomo ikakutana na wakabadilishana mate.

Kilichofuatia ni Lava Lava kudondoka na kuzimia ghafla. Alifanyiwa huduma ya kwanza na aliporejelewa na fahamu, kukazuka tetesi kwamba alikuwa akisaka kiki.

Lakini Lava alijitetea kwa kusema hajui kilichosababisha hadi akazirai. Hajui kama ni lile busu lililomchizisha au ni kitu kingine.

PAPA WEMBA (Abijan, 2016)

Marehemu mkongwe huyu wa muziki wa lingala alikuwa akitumbuiza mjini Abijan, Ivory Coast alipodondoka ghafla na kuzirai.

Bendi yake ikawahi kumfanyia huduma ya kwanza lakini haikusaidia. Wakajaribu kumharakisha hospitalini lakini wakawa wamechelewa kwani Papa alikuwa tayari ameshafariki dunia.

Papa alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 66. Tetesi zinadai kwamba alitiliwa sumu kwenye Mic yake aliyoipumua kipindi akiwa anatumbuiza na mara moja ikamdhuru na kumtoa uhai.

JUSTIN BEIBER (London 2013)

Staa huyu alikuwa akipiga shoo katika uwanja wa London 02 Arena Uingereza 2013. Mara ghafla alianza kulalamika kushindwa kupumua vyema. Lakini licha ya kujihisi vibaya, alisisitiza kwamba lazima amalize kupiga shoo. Aliishia kula ujeuri wake sababu hewa ilimkatikia ghafla na akazirai stejini. Alikimbizwa hospitalini ambapo alifanyiwa huduma ya kwanza na kuweza kurejeshwa kwenye ufahamu.

KELLY ROWLAND (This Day Music Festival, Lagos 2007)

Mwanamuziki huyu aliyepata umaarufu mkubwa na kundi la Destiny Child liliwajumulisha vile vile Beyonce na Monica, naye aliwahi kuzirai stejini kipindi akiwa anatumbuiza.

Kelly ambaye umaarufu wake ulizidi hata zaidi alipofanya hiti collabo ya Dilemma na Nelly, alikuwa amesafiri hadi Lagos, Nigeria kwa ajili kutumbuiza kwenye shoo ya This Day Festival.

Akiwa stejini mara ghafla alishindwa kumaliza shoo baada ya kuzimia na kuzirai. Alikimbizwa katika hospitali moja na kupewa huduma. Wawakilishi wake baadaye walisema kuzirai huko kulitokana na mwili wake kupungukiwa na kiwango cha maji hivyo kumnyonya nguvu hata zaidi alipokuwa akitumbuiza.

MARILYN MANSON (Houston, 2018)

Nyota huyu wa muziki wa Rock kutoka Marekani alikuwa akitumbuiza kwenye ziara ya shoo zake za Twins of Evil- The Second Coming Tour.

Mara ghafla alianza kusikia maruweruwe wakati akiwa anaimba. Wale mashabiki waliokuwa karibu zaidi na steji, Manson akawaambia kwamba alikuwa anahisi joto kali. Ghafla alionekana akiyumbayumba na kisha akadondoka mara tu baada ya kumaliza kuimba wimbo wake wa Sweet Dreams. Tukio hilo lilimpelekea kusitisha shoo yake lakini aliirejelea baada ya siku mbili za mapumziko.

LILY ARMSTRONG (Agosti, 1971)

Akiwa anatumbuiza kwenye shoo ya kumbukumbu ya mume wake marehemu Louis Armstrong aliyekuwa amefariki mwezi mmoja kabla, Lilly alizidiwa na hisia na kuzirai juu ya Piano yake. Alifariki dunia kipindi akiwa anakimbizwa hospitalini kwa ajili ya huduma.

IRMA BLUE (Karawang, West Java 2016)

Irma alikuwa msanii maarufu sana nchini Indonesia na alifahamika sana kwa kupenda kutumbuiza stejini akiwa na nyoka wa kufugwa.

Sasa kwenye shoo hii, alikuja na nyoka aina ya Cobra stejini. Wakati akitumbuiza kwa bahati mbaya alimkayaga yule nyoka kwenye mkia naye akajibu mapigo kwa kumng’ata kwenye paja. Wadau wake wakamletea dawa ya kuangamiza ile simu ambayo walikuwa wakiibeba endapo kungetokea hatari. Hata hivyo Blue alikataa kunywa na aliendelea kutumbuiza kwa dakika 45. Ghafla alianza kutapika na kisha akazirai na kufariki papo hapo. Tetesi zilidai kwamba Blue alikataa tiba sababu alidhani yule nyoka alikuwa tayari ameshang’olewa meno zake za sumu.

You can share this post!

Waliomlaghai mama Sh40,000 wauawa na umati

ANA KWA ANA: Nguli Chris Martin kaja na wazee wake wa kazi

adminleo