Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Maandalizi ya maisha ya ndoa ni muhimu kwa wanaotaka kuoana

December 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo.

Swala na salamu zimwendee Mtume Muhammad Swallallahu ‘Alayhi Wasallam, Maswahaba wake kiram na watangu wema hadi siku ya Kiyama.

Katika kumuumba kwake mwanadamu, Mwenyezi Mungu aliweka utaratibu wa kuwepo mahusiano kati ya mume na mke ili kuendeleza uzao kwa wanadamu, kuwaondolea upweke na kuwatunukia utulivu, faraja, huruma, mapenzi, upendo, na ushirikiano.

“Na katika ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo ishara kwa watu wanaofikiri”. Arruum 21.

Kutokana na umuhimu wa ndoa katika maisha ya mwanadamu, tumeona kuna haja ya kukumbushana, hasa vijana jinsi ya kujiandaa na maisha ya ndoa kabla ya kuoana.

Katika Uislamu inapofikia hatua ya kutaka kuoa au kuolewa, pande zote mbili hukabiliwa na mawazo mengi ni vipi atampata mchumba sahihi.

Tatizo kubwa ni katika kumchagua mwenza sahihi na mwenye sifa, ambaye utakapompata na kumuoa/kuolewa, atakuwa ndiye mshirika wako wa maisha.

Vilevile hutizamwa ni vigezo gani atumie muoaji au muolewa katika kufikia lengo lake la kumpata anayestahili na kukidhi.

Ikumbukwe kwamba pamoja na kwamba kuna dhana kwamba mwanamke hawezi kuchumbia na hana nafasi ya kuchagua mume anayetaka aolewe naye, lakini ukweli ni kwamba kwa utashi wake mwanamke ana haki ya kumkubali au kumkataa mchumba anayekuja kwake.

Kwa ujumla mambo ya ndoa huwasumbua watarajiwa huku kila mmoja akiwa na mitazamo tofauti katika chaguo.

Kila upande ukiwa umekua na kulelewa katika mazoea, desturi na tamaduni tofauti, mambo ambayo yana athari kwa namna moja au nyingine katika makuzi.

Baadhi ya wenye dhamira ya kuoa au kuolewa, wanakuwa hawafahamu wanahitaji mke au mume wa aina gani. Wakati mwingine wanajikuta wanaingia katika hamu ya kuwa katika ndoa, lakini bila kujua wanataka kuwa na wenza wa namna gani.

Wengine hujikuta wakijiingiza katika ndoa bila ya kuwa na ufahamu wa kutosha au taaluma yoyote inayohusiana na maisha hayo ya mahusiano na hatima yake hukosa uwezo wa kuziendesha ndoa zao.

Lakini pia wapo ambao hawana kabisa uelewa wa misingi ya kuoa na kuolewa zaidi ya kusukumwa na fikra finyu ya kutamani kuwa na mwenza kwa ajili ya kukidhi tu matamanio ya nafsi na hususan tendo la ndoa na kurahisishiwa baadhi ya majukumu kama vile kupika, usafi wa nyumba, kufua miongoni mwa mengine.

Wapo wanaotamani kuingia katika mahusiano ya ndoa kwa lengo moja tu la kupata wepesi wa kupata mali na maisha ya anasa na starehe.

Kwa ujumla wengi wanaotaka kuoa au kuolewa, mara nyingi hawana fikra halisi na pana ya kusudio la ndoa. Si kidini wala si kimazingira. Hata maandalizi katika kuliendea jambo hilowakati mwingine hayafanyiki vya kutosha na kwa kiasi kikubwa. Uchaguzi wao hautizami sekta za msingi kama dini na maadili kwa ujumla wake.

Siku hizi sehemu kubwa ya jamii yetu imezoea kuyafanya masuala ya ndoa kuwa ni mambo ya kiutamaduni na si masuala ya kidini kama inavyotakikana.

Ndiyo maana hata kipaumbele katika hizo ndoa huwekwa zaidi katika masuala ya kijamii na kitamaduni na dini ikiwekwa pembeni kama sifa ya ziada. Kwa mtazamo huo, ndoa nyingi zimekosa uvumilivu na kuendelea kuporomoka na kusababisha utengano wa kifamilia na magomvi kwa kasi ya kutisha.

Matokeo yake, badala ya kuunganisha familia kama ilivyokusudiwa na kujenga udugu, ndoa zimekuwa chachu ya utengano wa kifamilia, kuporomoka udugu na kuwa chanzo cha huduma mbovu za kijamii katika familia na wanaoathirika zaidi ni watoto.

Katika kufanya uchaguzi wa mtarajiwa, iwe ni mume au mke, kuna mambo mawili yanaweza kujitokeza, nayo ni kuwa na ndoa iliyojaa matarajio ya watarajiwa (kama yalikuwepo kabla) au kuwa na ndoa iliyokosa matarajio ya watarajiwa na hivyo mwisho wake kuwa ni balaa badala ya raha, dhiki badala ya faraja.

Anaweza mtu kuoa au kuolewa na akafurahia uamuzi wake huo kwa jinsi ndoa ilivyotimiza matakwa ya kuitwa ndoa, lakini mwingine akajutia uamuzi wake kutokana na kukithiri maudhi mpaka kufika kuhasimiana na kuachana.

Ili kuepukana na hali hii, kuna haja ya kuwa na utaratibu mahususi kwa wazazi, wazee na viongozi wetu wa dini katika jamii yetu, kujenga mazoea ya kutoa mafunzo na miongozo kwa vijana wetu ili kujaribu kutoa mwongozo kujaribu kuokoa janga hili la kasi ya kuharibika mahusiano ya ndoa, jambo ambalo Mwenyezi Mungu anasema linamchukiza sana.

Kwa mtazamo wangu, dini ndiyo mwongozo namba moja wa kujenga ustaarabu wa maisha ya mwanadamu.

Kwa maana hiyo, kuna haja hasa kwa Waislamu, ukiacha zile hutba za ndoa, kusisitizia thamani ya mafunzo ya dini katika kuliendea jambo hili.

Ifahamike tu kwamba msingi wa ndoa yoyote ili iweze kuwa imara, lazima uwe na mafunzo ya dini. Dini ndio mwalimu wa maadili, dini ndio mwalimu wa busara, dini ndio mwalimu wa uvumilivu na subra, dini ndio ustaarabu wa maisha, dini ndio chanzo cha kumjua na kumtegemea Mwenyezi Mungu aliyetuumba, ambaye ndiye mwenye dini yake na kaamuru wanadamu kuifuata ili kufaulu hapa duniani na kesho akhera.

Utulivu katika ndoa ni moja katika mambo muhimu yanayodumisha maisha ya ndoa kwa wanandoa. Vijana wanaotarajia kutimiza suna hiyo wanatakiwa kufundishwa hilo na wawe na yakini na hilo.

Haina maana kosa kidogo tu, au kosa moja likamfanya mtu mara moja akakosa uvumilivu wa kutoa nafasi ya mwenzake kuonywa au kujirekebisha, yeye keshaamua.

Lakini umuhimu wa ndoa kwa kuoa wajane, wajakazi, maskini au mafukara, kuleta maana kwamba ndoa kunusu.

“Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu”.

Ndoa huunganisha koo kufikia kuweza kurithiana kati ya mume na mke. Annisaa 12

Ndoa huzuia zinaa.

Ni jambo la msingi kwa kila mwanandoa au anayetarajia kuingia katika ndoa, afahamu kwamba ndoa ni kati ya riziki ambazo Mwenyezi Mungu amewapa waja wake. Katika ndoa kuna wajibu, haki, majukumu na utaratibu wake katika maisha. Kabla ya kuoa au kuolewa na kufunga ndoa, kuna haja ya kujiuliza kwa nini unaliendea jambo hilo. Hili ndilo swali la kwanza mhusika anapaswa kujiuliza ndani ya moyo wake na kupata majibu yake.

Ndoa humpa mtu heshima na katika jamii, kupata watoto, kutafuta sitara, kujenga familia bora, kuwaridhia wazazi wawili, na kukidhi hamu za kijinsia.

Lakini wapo pia ambao kufikia maamuzi ya kuoa kwa kufuata marafiki, kusaidiana majukumu kama vile kupika na kuosha nguo, kusaidia ulezi wa wazazi, kupata mali na utajiri, kuepuka lawama na maudhi na kadhalika.

Ni lazima yawepo malengo ya kuoa kabla ya tendo lenyewe. Lakini malengo yenyewe lazima yawe sahihi na sio ya binafsi na ya matamanio tu.

Mtume (saw) amesema, “Mwanamke huolewa kwa mambo manne. Kwa (ajili ya) mali yake, kwa nasaba yake, kwa uzuri wake na kwa dini yake, basi mtafuteni mwenye dini (kwani) mikono yako itatakatika na michanga. (Bukhari na Muslim).

Kwa mwongozo huo katika Uislamu, unaonekana umuhimu wa kujua lengo kabla ya tendo la kufunga ndoa.

Hii ni kwa kuwa ndoa ni moja ya njia za kuunda jamii. Hivyo ni vizuri malengo yakafahamika mapema na yawe katika mtazamo na madhumuni sahihi.