Drama Sonko akitiwa ndani
Na BENSON MATHEKA na WANDERI KAMAU
ZILIKUWA kasheshe, sarakasi na kukuru kakara za aina yake pale Gavana wa Nairobi, Mike Sonko, aliponyakwa Ijumaa katika eneo la Voi na maafisa wa polisi waliotua ghafla kwa helikopta na kumtia pingu.
Gavana huyo mwenye makeke na viroja vya sampuli mbalimbali alibambwa baada ya purukushani za muda kuhusiana na madai ya utumizi mbaya wa takribani Sh357 milioni, mali ya Kaunti ya Nairobi.
Kukamatwa kwa Sonko, hata hivyo, kumeibua maswali mengi kuhusu serikali ya kaunti yake itakavyosimamiwa na iwapo atajiuzulu alivyoahidi alipoanza kuchunguzwa kwa madai hayo ya ufisadi.
Sonko alikamatwa akiwa Voi, Kaunti ya Taita Taveta, saa chache baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kuagiza akamatwe na kufunguliwa mashtaka ya ufisadi.
Kama ilivyo kawaida yake, Sonko alizua kizaazaa akikataa kutiwa mbaroni na maafisa wa usalama waliomfuata kwa helikopta ya polisi kwenye barabara ya Mombasa.
Ofisi ya Bw Haji ilisema kwamba alikamatwa akijaribu kutoroka alipofahamu kuwa alikuwa akisakwa.
Kwenye kikao na wanahabari Ijumaa asubuhi, Bw Haji alikuwa amemuonya Sonko na washtakiwa wenzake wasikatae kutiwa mbaroni au kutumia wafuasi wao kujikinga. Hata hivyo, kanda ya video iliyosambazwa mtandaoni inaonyesha kundi la maafisa wa usalama liking’ang’ana kumkamata Bw Sonko ambaye kwa muda, anawakemea na kujaribu kuhepa.
Maafisa hao wanaonekana wakimzingira na baada ya dakika kadhaa, wanamzidi nguvu na kumtia pingu na kumwelekeza kwenye helikopta ambayo ilimsafirisha hadi uwanja wa ndege wa Wilson, Nairobi ambapo usalama ulikuwa umeimarishwa.
Kabla ya kutiwa nguvu, Bw Sonko anaonekana akimrushia mikono afisa wa cheo cha juu wa polisi. Haikubainika iwapo atakachukuliwa hatua kwa kukataa kutiwa mbaroni.
Kutoka uwanja wa ndege wa Wilson, Bw Sonko alisindikizwa hadi makao makuu ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ambako alifungiwa.
Usalama uliimarishwa karibu na ofisi hizo huku barabara kadhaa zikifungwa kuzuia wafuasi wake kuzua ghasia.
Wakenya wanasubiri kuona ikiwa Sonko, ambaye ni gavana wa nne kushtakiwa akiwa enzini, atajiuzulu alivyoahidi Septemba 2019.
Akihutubu katika ibada ya wafu ya aliyekuwa mbunge wa eneo la Kibra, Marehemu Ken Okoth, Sonko alisema iwapo EACC itapendekeza ashtakiwe naye Bw Haji aidhinishe kushtakiwa kwake, angeondoka mamlakani.
“Lazima tuendeleze vita dhidi ya ufisadi kikamilifu. Hatuwezi kufanya hivyo ikiwa tutaendelea kuwa afisini baada ya kushtakiwa. Kwa hivyo, huo ni msalaba nitakaobeba binafsi ili kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta kwenye vita vyake dhidi ya ufisadi,” alisema Bw Sonko.
Ikizingatiwa kwamba amekuwa akihudumu bila naibu tangu kujiuzulu kwa Polycarp Igathe mwaka 2018, wengi wanasubiri kuona serikali ya Kaunti ya Nairobi itakavyosimamiwa.
Magavana wanaoshtakiwa kwa ufisadi wamekuwa wakiagizwa kutokanyaga katika ofisi zao japo wakiruhusiwa kuendelea kutekeleza majukumu yao inavyofanyika katika Kaunti ya Kiambu na Samburu baada ya wenzake Ferdinard Waititu na Moses Kasaine waliposhtakiwa.
Kulingana na wadadisi, kukamatwa kwa Bw Sonko kunautia uongozi wa Kaunti ya Nairobi hatarini, ikizingatiwa kuwa hana naibu gavana huku baraza lake la mawaziri likiwa halijakamilika.
Kulingana na Bw Martin Andati, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uongozi, pengo hilo ni hatari sana na linaweza kuiweka Nairobi katika mzozo wa uongozi.
“Bila uwepo wa naibu gavana na baraza maalum la mawaziri, ni dhahiri kuwa Kaunti ya Nairobi inakumbwa na tishio kubwa kuhusu uongozi wake,” akasema Bw Andati.
Uongo
Hali ni tete kwa Sonko ambaye anachunguzwa kwa madai ya kutoa habari za uongo kwa EACC ili kuidhinishiwa ugombezi wake wa ugavana.
Tume hiyo inasema Sonko alisema hakuwahi kufungwa jela katika maisha yake alipokuwa akijaza fomu za maombi ya cheti cha kuidhinishwa na EACC kushiriki katika uchaguzi wa 2017. EACC inasema kwamba ina habari Sonko alitoroka jela ya Shimo la Tewa, Kaunti ya Mombasa kabla ya kukamilisha kifungo. Gereza hilo linataka arudishwe humo ili akakamilishe hukumu yake na pia ashtakiwe kwa kutoroka kinyume cha sheria.
Ikiwa ombi la gereza hilo litakubaliwa, Bw Sonko huenda akawa mahabusu huku kesi yake ya ufisadi ikiendelea.
Ijumaa, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Ufisadi, Douglas Ogoti alikataa ombi la kumpa Sonko dhamana akisubiri kushtakiwa.
Miongoni mwa sakata zinazomwandama ni inayohusu utoaji wa zabuni kwa kampuni ya Jambopay iliyokuwa ikikusanya ada za maegesho ya magari jijini.
Bw Sonko pia anakabiliwa na tuhuma za kutozingatia kanuni zifaazo kwenye ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Dandora wenye gharama ya Sh300 milioni na kupotea kwa Sh160 milioni katika kandarasi tata ya uzoaji taka jijini Nairobi.
Wengine watakaoshtakiwa pamoja na Sonko ni karani wa kaunti hiyo Bw Peter Mbugua, mkuu wa idara ya ununuzi Patrick Mwangangi na wanachama wa kamati ya tenda Samuel Ndung’u, Edwin Kariuki, Lawrence Mwangi, Preston Miriti, Wambua Ndaka na Andrew Nyasiego.
Wamiliki wa kampuni husika pia watakamatwa na kushtakiwa.