• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 2:55 PM
TAHARIRI: Majengo kuanguka ni tunda la ufisadi

TAHARIRI: Majengo kuanguka ni tunda la ufisadi

Na MHARIRI

KUPOROMOKA kwa jengo lililosababisha vifo vya watu wanne Ijumaa katika mtaa wa Tassia jijini Nairobi ni matunda ya ufisadi katika idara husika katika serikali ya Kaunti na serikali kuu.

Inaonyesha kuwa serikali haijawajibika kikamilifu licha ya kuahidi mara kwa mara pale mikasa kama hii inapotokea kuwa itachukua hatua na kubomoa majengo yote hatari kwa umma.

Kwa sababu ya ufisadi, shughuli ya kubomoa majengo hayo huwa inakomeshwa hadi mkasa kama wa Ijumaa unapotokea.

Si ajabu basi kuanzia leo tukaona maafisa husika wakijifanya wanajua kazi na kuanza kubomoa majengo ambayo ni imara kulipiza kisasi wamiliki wao waliokataa kutoa hongo na kuacha yale hatari.

Hatusemi kuwa majengo huwa yanabomolewa bila sababu, tunachosema ni kuwa huwa kuna ubaguzi huku yale hatari kwa usalama yakiachwa na yale ya imara kama ya kibiashara kubomolewa.

Ikiwa visa vya majengo kuporomoka na kusababisha maafisa vitapungua ni lazima ufisadi ukabiliwe kikamilifu.

Hii inawezekana kukiwa na usimamizi mzuri na kuajiri watu wanaohitimu waliopigwa msasa kuhakikisha wanatimiza viwango vya juu vya maadili, wana uzalendo na wanaheshimu maisha ya binadamu.

Wanaotoa vibali na kuidhinisha majumba yanayojengwa maeneo yasiyofaa na yasiyotimiza viwango vinavyohitajika hawana utu na ni sawa na wauaji. Wanaopokea hongo kuruhusu ujenzi huo wanabeba lawama sawa na wamiliki wa majengo yenyewe.

Wanaotepetea kuyabomoa na kusubiri yaporomoke na kusababisha maafa ni sawa na wauaji. Haya yote yanatokana na usimamizi mbaya na tamaa.

Usimamizi mzuri utahakikisha ni watu wenye maadili wanaoajiriwa katika idara muhimu kama hiyo.

Usimamizi mzuri utahakikisha kuwa maafisa hawachezi karata na maisha ya wakazi. Kungekuwa na usimami mzuri katika serikali ya Nairobi majengo yote hatari yangekuwa yamebomolewa bila kujali tabaka na cheo cha wanaoyamiliki na maafisa wote waliohusika kuyaidhinisha kufutwa kazi na kushtakiwa.

Usimamizi huo unaweza kupatikana kupitia kwa debe kwa kuhakikisha kuwa ni wanaoingia mamlakani ni watu wenye maadili.

Wakazi wa Nairobi na maeneo mengine wasipohakikisha wamechagua watu wenye maadili, majanga ya majumba kuporomoka yataendelea katika miji yetu. Haya ni matokeo ya nchi ya kitu kidogo.

You can share this post!

Gari lingine latumbukia baharini, uokoaji waendelea

MBURU: Watu wachukue tahadhari kuepuka madhara ya mafuriko

adminleo