MAKALA MAALUM: Malipo duni ni miongoni mwa masaibu mengi yanayotatiza taaluma ya ualimu
Na VITALIS KIMUTAI
JINA mwalimu aghalabu huhusishwa na mtu wa hadhi na anayeheshimika katika jamii.
Si ajabu kwamba katika enzi za wazazi wetu, watoto wengi walitamani kusoma kwa bidii ili hatimaye kuwa kama walimu wao.
Hata hivyo, kadri na mpito wa wakati, hadhi ya walimu nchini imezidi kudunishwa, huku taaluma hiyo ikigeuka dhihaka kiasi kwamba sio watu wengi wangependa kuwa kama walimu waliowafunza.
Uhalisia huu wa kutamausha umedhihirika bayana kufuatia ripoti ya kushtusha, iliyotolewa na walimu wakuu wa shule za sekondari nchini.
Kulingana na ripoti hiyo, imebainika kwamba walimu wenye shahada za digrii walioajiriwa na Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) kama wanagenzi, hupokea mishahara ya kiwango cha chini zaidi kuliko mabawabu wanaofanya kazi katika shule walizotumwa kufunza!
Sh15,000
Walinzi walioajiriwa na Bodi za Usimamizi (BOMs) katika taasisi za mafunzo, hutia kibindoni jumla ya Sh 15,000 kwa mwezi.
Hata hivyo, TSC huwapa walimu wanagenzi katika shule za sekondari Sh 15,000, ambapo baada kukatwa ada mbalimbali kuambatana na sheria, hupeleka nyumbani Sh 10,000 kila mwezi.
Hali huwalemea zaidi walimu wa shule ya msingi walioajiriwa kama wanagenzi.
Walimu hao hupata jumla ya Sh 10,000 ambapo baada ya kukatwa ada anuwai, husalia na Sh 6,000 pekee, kiasi ambacho ni nusu ya mshahara wa jumla, unaopokewa na walinzi katika shule za upili.
Masaibu ya wanagenzi katika shule za sekondari ni tele huku mshahara wao mdogo ukidondolewa zaidi na ada za kila namna.
Kando na bima ya kibinafsi wanayohitajika kuchukua inayogharimu Sh 1,200 kila mwezi, Bodi ya Mikopo kuhusu Elimu ya Taasisi za Juu (HELB) hunyofoa Sh 3,000 kutoka kwenye mishahara ya walimu.
Bima ya Kitaifa kuhusu Afya (NHIF) huchukua Sh 800 huku Hazina ya Kitaifa kuhusu Malipo ya Uzeeni (NSSF) ikijitwalia Sh600, nayo Malipo ya Ushuru (PAYE) ikinyakua Sh 1,741.
Walimu wa TSC wanaoajiriwa kama wanagenzi katika shule za msingi angalau hupata afueni, maadamu hawalipi mikopo ya HELB, huku kiwango cha ushuru wanaokatwa kikiwa Sh 1,116.
NHIF na NSSF
Lakini ni sharti vilevile wajisajilishe na NSSF pamoja na NHIF ambapo ada zinazokatwa husalia sawa na zile za wenzao katika sekondari.
Si ajabu kwamba miungano mikuu ya walimu nchini imechukua hatua katika juhudi za kuokoa jahazi la walimu linaloelekea kuzama.
Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT), Chama cha Walimu wa Sekondari na Vyuo Anuai (KUPPET) na Muungano wa Walimu Wakuu katika Shule za Sekondari, sasa vinashinikiza kubatilishwa kwa masharti ya kandarasi za walimu.
Kulingana na wadau hao, hatua hiyo itasaidia pakubwa kurekebisha walakini ambao bila shaka umewaondolea motisha waajiriwa.
Isitoshe, KNUT na KUPPET vilevile zinaitaka TSC kuwaepusha wanagenzi 10,300 kutokana na sera yenye utata kuhusu uhamishaji.
Wanahoji kwamba kufanya hivi kutawezesha walimu hao kufanya kazi katika maeneo yao.
Athiri huduma
Viongozi hao wakiwemo makatibu wa KNUT tawi la Bomet na Sotik Malel Langat, na Mathias Langat mtawalia, pamoja na wenzao wa KUPPET Paul Kimetto (Bomet) na Zablon Awange (Kisumu), wamesema kwamba hali inayowakabili walimu itaathiri juhudi zao za kutoa huduma bora ya elimu katika shule za umma nchini.
“Inasikitisha kuwa walimu wanagenzi wamepatiwa kandarasi kwa mwaka mmoja ilhali hakuna sheria au hakikisho kuhusu nyadhifa za kudumu na masharti ya kustaafu baada ya muda wa kandarasi hizo kukamilika,” ilisema taarifa yao walipokua wakizungumza mjini Sotik.
Kulingana na Malel, Rais anapaswa kuwajibikia suala hili la walimu yeye binafsi ili kuzuia hali ambayo inageuka taratibu kuwa janga katika sekta ya elimu.
Alisema suala hili litagharimu pakubwa taifa hili iwapo halitarekebishwa mapema.
“Japo tunaunga mkono juhudi za serikali za kubuni ajira kwa wataalam nchini, sekta ya elimu si mahali pa kufanyia majaribio. Walimu wote wenye mafunzo wanapaswa kuajiriwa katika nyadhifa za kudumu na masharti ya kustaafu,” alisema
Ajira
Maafisa hao sasa wameitaka TSC kutenga kiasi cha fedha za kutosha kufadhili ajira ya walimu.
Wanahoji kuwa hatua hii itasaidia kuziba pengo linalosababishwa na uhaba wa walimu 100,000 katika shule za umma, kinyume na idadi finyu ya ajira inayofanyika kuziba nafasi za walimu waliondoka kutokana na sababu za kimaumbile.
“TSC inapotangaza nyadhifa ambapo jumla ya walimu 5,000 huajiriwa kila mwaka, kile ambacho taifa halifahamu ni kuwa uhaba wa walimu huzidi kuongezeka huku kukiwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na taasisi za elimu,” alisema Awange.
Kwa upande wake, Kimetto alisema mwalimu anapopokea Sh8,000 kila mwezi, ni sawa na kumweka katika kiwango sawa na mjakazi wa nyumba hali ambayo ni dhihaka kwa taaluma hiyo.
Ni kama msumari moto kwenye kidonda ikizingatiwa muda waliotumia katika masomo yao kwa miaka mingi na gharama ya elimu yao.
“Kando na ada hizo wanazokatwa, wanagenzi wanalazimika kukabiliana na uhalisia kwamba ni sharti walipe kodi za nyumba, wagharamie usafiri wao binafsi, chakula, mavazi na matumizi mengine ikiwemo kukimu familia zao,” alisema Langat.
Walimu wakuu wa shule mbalimbali waliohojiwa wamethibitisha kwamba mishahara ya baadhi ya wafanyakazi katika taasisi za elimu ni ya juu kushinda ile ya walimu wanagenzi.
“Kwa hakika wanagenzi hao hawana motisha na hali hiyo imeathiri utoaji huduma shuleni. Baadhi yao wanatoka maeneo ya mbali na hawawezi kukidhi mahitaji yao huku walinzi wakipata malipo bora kuwashinda,” alisema mwalimu mkuu
Naibu Mwenyekiti wa KUPPET, Julius Korir, na Mbunge wa Bomet ya Kati Ronald Tonui ambaye ni mweka hazina wa kitaifa KUPPET, wamehoji kwamba kuwatuma walimu mbali na kaunti wanamotoka kutawaathiri mno kiuchumi.
Motisha
“Unapowaajiri walimu kama wakufunzi na kuwapa mshahara wa Sh15,000 kisha uwatume nje ya maeneo yao, utawanyima motisha ya kufanya kazi kwa bidii maadamu hela hizo hazitatosha kuwakimu kimaisha,” alisema Bw Korir.
Kwa maoni yake, Tonui alieleza kuwa ada hizo zingepunguza malipo ya jumla ya walimu hivyo kufanya kazi hiyo kukosa maana kwa wanagenzi hao kwa kuwa hawafaidi kwa vyovyote kiuchumi.
Maoni yake yameungwa mkono na Sammy Chelanga, katibu wa Kuppet anayesimamia taasisi za Kiufundi pamoja na Katibu wa Tawi la Narok Charles Ngeno.
Wawili hao wamesema kuwa inasikitisha kuwa wanaosaka kazi wanaagizwa kujitwalia bima ya ajali ilhali hawana hata hela hizo.
Kulingana na Chelanga, viwango vya elimu katika shule za umma zimedorora mno kutokana na uhaba wa walimu.
“Ajira isiyo kamilifu kwa walimu hasa kwa lengo la kuziba nyadhifa za wanaoacha huduma kutokana na masuala ya kimaumbile si suluhu kwa upungufu uliopo shuleni pamoja na kuongezeka pakubwa kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule nchini,” alisema
Utafiti uliofanywa na TSC mwaka jana uliashiria kwamba kaunti ya Bomet ilikuwa na uhaba wa walimu zaidi ya 100,000 katika shule mbalimbali kaunti hiyo.
Hali hiyo imeathiri ubora wa elimu hasa wakati huu ambapo serikali imepania kutekeleza kiwango cha asilimia 100 kutoka shule za msingi, sekondari na vyuo.
Ripoti hiyo ya TSC yenye anwani ‘Nyadhifa za Waajiriwa Kitaifa katika Masomo Baada ya Shule ya Msingi’ inaashiria kwamba kaunti za Bomet na Migori ndizo zilizoathiriwa zaidi na uhaba wa walimu kwa asilimia 58 kila moja.
Kaunti nyinginezo ni Busia na Trans Nzoia zilizochukua nafasi ya pili zikiwa na asilimia 54 kila moja.
Nairobi na Kiambu ziliorodheshwa mwisho huku zikiwa na asilimia 24 na 23 mtawalia.