AKILIMALI: Mkulima anavyofaidi kutokana na ukuzaji na uuzaji wa ‘Asian kales'
Na PETER CHANGTOEK
KWA miaka na mikaka, Kaunti ya Meru imekuwa ikijulikana kwa ukuzaji na uuzuji wa miraa.
Hata hivyo, upo mmea mwingine ambao umeanza kukuzwa katika eneo hilo, kwa madhumuni ya kuuzwa ughaibuni.
Ni mmea aina ya Asian kales ambao baadhi ya wakulima katika eneo hilo wameanza kuukuza.
Bw Joseph Muriithi ni mmojawapo wa wakulima wachache ambao wameanza kukishughulikia kilimo cha mmea huo, ambao husafirishwa kwa ajili ya kuuzwa jijini London, Uingereza na Oslo, Norway.
Mkulima huyo alijitosa katika zaraa ya ukuzaji wa mmea huo mwaka 2011 katika kitongoji kilichoko kwa umbali wa kilomita takribani tano, kutoka eneo la Mitunguu, katika gatuzi lilo hilo la Meru.
Bw Muriithi ana shamba lenye ukubwa wa ekari nane, japo huikuza mimea hiyo katika sehemu mbalimbali za shamba hilo. Anaikuza aina ainati za mmea huo, mathalani Karela, Dudhi, Okra, na Ravaya.
Katika shamba robo tatu (3/4), mkulima huyo anakuza mboga aina ya Karela, huku Ravaya akizikuza kwa shamba ekari moja, ilhali Dudhi na Okra, Muriithi asema, amezipanda katika shamba nusu ekari (1/2) kila moja. Sehemu iliyosalia katika shamba lake ina migomba (mimea inayozaa ndizi).
“Hali ya hewa katika eneo hili ni mwafaka kwa ukuaji wa mmea huo,’’ asema, huku akisisitiza kuwa kuwapo kwa mchanga wenye rutuba pamoja na kuwapo kwa maji pale, huchangia ukuaji mzuri wa mmea huo.
Muriithi anasema kuwa mimea hiyo inahitajika mno nje ya nchi, pamoja na humu nchini.
“Nyingi yayo hutambulika kwa sababu ya madini ambayo inayo. Kwa mfano, Okra yatambulika kuwa na nyuzinyuzi ambazo husaidia kwa mmeng’enyo wa chakula, kudhibiti viwango vya sukari kwa damu, na kuwa na Vitamini C,’’ asema.
Aina hizo nyinginezo pia, zina manufaa mengineyo mwilini mwa mlaji.
Kabla mimea hiyo haijapandwa, mkulima hana budi kuliandaa shamba vyema. Mchanga utengenezwe hadi uwe laini kabisa. Pia, mbolea zatakikana zitumiwe ili kuufanya mchanga uwe na rutuba kwa ukuaji bora wa mimea hiyo.
Baada ya kuchipuka kwa mimea hiyo, mbolea aina ya DAP hutumiwa ili kuifanya mizizi kuwa na nguvu. Hali kadhalika, mkulima anastahili kuwa chonjo ili kuyakabili magonjwa pamoja na magugu.
Mimea inyunyiziwe dawa za kuzuia na za kuyakabili magonjwa yanayoiathiri. Vilevile, ipaliliwe ili kuyaondoa magugu. Mbali na hayo, dawa za kuwaua wadudu waharibifu zitumike au mbinu nyingine isiyokuwa ya kutumia kemikali itumiwe kuwakabili wadudu hao.
Mimea hiyo huchukua muda wa miezi tofauti tofauti ili kukua na kuwa tayari kuchumwa.
Okra huchukua siku 45 baada ya kupandwa ili kuwa tayari kwa ajili ya kuchumwa. Karela na Ravaya huchukua muda wa miezi mitatu au siku 90. Aina hizo mbili, yaani Karela na Ravaya huchumwa kwa muda wa siku 60. Dudhi nayo huchukua muda wa siku 90 kutoka wakati wa kupandwa hadi wakati wa kuchumwa. Aina hiyo huendelea kuchumwa kwa muda wa siku 60.
Baada ya kuchumwa, mboga hizo huchaguliwa ambapo zile ambazo zina ubora wa juu zaidi, husafirishwa kuuzwa ughaibuni na zile nyingine zinazosalia kuuzwa humu nchini.
Changamoto
Changamoto kuu, kwa mujibu wa mkulima Muriithi, ni kutokuwapo kwa utaratibu mwafaka wa uuzaji. Anasema kuwa awali, wakulima walikuwa wakikutana ana kwa ana na wasafirishaji wa mazao, lakini jambo hilo lilitatizwa miaka mitatu iliyopita, na hivyo basi, wakashurutika kufanya kazi na madalali anaodai huwapunja wakulima.
Madai yake yanaungwa mkono na Erastus Gituma, ambaye ni wakala wa usafirishaji na uuzaji mazao kwa nchi za nje.
“Tunapitia changamoto wakati wa usafirishaji kwa sababu mchakato huo ni mgumu. Kampuni za kusafirisha zimelazimishwa kufanya ukaguzi maradufu,’’ asema wakala huyo.
Ushauri kitaalamu
Kuhitajika kwa wingi kwa aina hizo za mboga ni kichocheo tosha kinachofaa kuwasukuma wakulima kujitosa katika shughuli ya ukuzaji wa mboga aina ya Asian kales. Hata humu nchini Kenya, upo uhitaji wa aina hizo za mboga.
Hata hivyo, wakulima hawana budi kupata habari na maelezo kuhusu jinsi ya kuzikuza kutoka kwa wataalamu wa masuala ya kilimo, kusudi kuwawezesha kufikia viwango vya juu vya ubora ambao unahitajika kwa mazao hayo, hususan yale ya kusafirishwa na kuuzwa katika nchi za nje.
Manufaa
Mboga hizo zina manufaa tele mno kwa afya binadamu. Zina virutubisho mbalimbali mwilini. Okra, kwa mfano, huwa na nyuzinyuzi ambazo husaidia kuendelea bara bara kwa mchakato wa mmeng’enyo (digestion) wa vyakula tumboni. Pia, zina Vitamini C na husaidia kudhibiti viwango vya sukari katika mwili. Hali kadhalika, zina madini aina ya kalisiamu (calcium) na ‘potassium’.
Aidha, ni bora kwa wajawazito. Isitoshe, zaweza kuzuia kutokea kwa maradhi ya sukari na ya figo.
Mboga hizo aina ya Dudhi nazo zina madini kama vile, ‘magnesium’, potassium, fosiforasi (phosphorous), vitamini, na husaidia mwili kwa kinga dhidi ya baridi na homa. Mbali na hayo, husaidia kuvipunguza visa vya ugonjwa wa kiharusi na ugonjwa wa sukari. Karela nazo husaidia kupunguza viwango vya sukari kwa damu. Ravaya nazo zina kalori kidogo na husaidia kupunguza kwa mwili kolestro.