MakalaSiasa

JAMVI: Safari ya BBI kutoka Bomas hadi Bungeni

December 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHARLES WASONGA

HUKU suala la iwapo ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) linapasa kutekelezwa kupitia bunge au kura ya maamuzi likiendelea kushika kasi, imebainika kuwa ripoti hiyo inaweza tu kuletwa bungeni kama mswada au hati ya sera ya serikali kuu.

Kulingana na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, ni mapendekezo ya ripoti hiyo ambayo yanahitaji kutekelezwa kupitia mageuzi ya kisheria na kikatiba ndio yatungiwa mswada.

“Na ripoti hii pia inaweza kufika bungeni kama ripoti kuhusu sera ya serikali ya kitaifa. Na baada ya kuwasilishwa bungeni kwa njia hiyo inaweza kujadiliwa namna ambavyo ripoti nyinginezo kutoka afisi ya Rais hujadiliwa bungeni na kupitishwa,” anasema Bw Muturi.

Hata hivyo, Bw Muturi anashikilia kwamba kufikia sasa afisi yake haijapata nakala za ripoti hiyo ya BBI. Anasema kuwa juhudi za Afisi ya Karani wa Bunge Michael Sialai kuomba ipewe ripoti hiyo na afisi ya Rais au Mpiga Chapa wa Serikali (Government Printer) hazijafua dafu.

“Kwa hivyo, hadi kufikia sasa ripoti hiyo ni mali ya Serikali Kuu hadi pale mapendekezo ya mabadiliko ya kisheria yatakapoletwa bungeni,” Bw Muturi anafafanua.

Wiki jana, Bw Muturi aliripotiwa akisema kuwa bunge halipasi kuongoza mchakato wa utekelezaji wa ripoti hiyo ya BBI bali shughuli hiyo inapasa kuachiwa wananchi waishughulikie kupitia kura ya maamuzi.

Kulingana na sheria, miswada ya marekebisho ya sheria na katiba itakayotumika kufanikisha utekelezaji wa baadhi ya mapendekezo ya ripoti ya BBI inapasa kutayarishwa na afisi ya Mwanasheria Mkuu Paul Kihara.

Hii ni baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa katika Kikao cha Baraza la Mawaziri, kujadiliwa na kuidhinishwa ili iwe stakabadhi rasmi ya serikali ya kitaifa kuhusu sera mbalimbali.

Wakili James Mwamu anasema kuwa baada ya Afisi ya Bw Kihara kuandaa miswada mbali mbali kuihusu ripoti ya BBI, miswada hiyo inapasa kuwasilishwa bungeni kupitia Afisi ya Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale.

“Hii ni kwa sababu chini ya mfumo wa utawala chini ya Katiba ya sasa Bw Duale, kama kiongozi wa chama au mrengo tawala bungeni ndiye daraja kati ya Serikali ya Kitaifa na Bunge la Kitaifa,” anasema.

Bw Mwamu anakubaliana na Spika Muturi kwamba kufikia sasa mkondo kama huo haujatafutwa katika jitihada za Serikali Kuu za kutaka kufanikisha utekelezaji wa ripoti ya BBI.

“Kwa hivyo, ni makosa kwa baadhi ya wabunge kudai kuwa tayari wamebuni kamati mbalimbali teule za wabunge kuongoza mchakato wa utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti ya BBI. Swali langu, ni je, wanawezaje kushughulikia utekelezaji wa ripoti ambayo haijawasilishwa rasmi bungeni kupitia taratibu zilizowekwa na sheria za bunge?” anauliza.

Mnamo wiki jana zaidi ya wabunge 40 kutoka eneo la Mlima Kenya ambao ni wandani wa Naibu Rais William Ruto walikutana katika mkahawa mmoja mjini Embu na kutangaza kuanzisha mchakato wa kutekeleza ripoti ya BBI kupitia asasi ya bunge.

Wakiongozwa na Seneta wa kaunti hiyo Njeru Ndwiga na Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, wabunge hao walishikilia kuwa bunge ndio mkondo mwafaka wa kufanikisha utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti hiyo wala sio kura ya maamuzi.

“Tumebuni kamati mbalimbali teule za wabunge na maseneta ambao wataketi na kuunda miswada itakayofanikisha utekelezaji wa sehemu mbalimbali za ripoti hii. Ripoti ya BBI haipaswi kuwasilishwa tena kwa ‘Wanjiku’ kupitia kura ya maamuzi kwani mkondo kama huu utapandisha joto la kisiasa nchini na kuvuruga mipango ya serikali ya kutekeleza mipango na miradi ya maendeleo,” akasema Seneta Ndwiga.

Naye Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria aliwasuta wabunge wandani wa Kiongozi wa ODM Raila wanaopendekeza kufanyike kura ya maamuzi kufanikisha utekelezaji wa ripoti hiyo akisema serikali haina fedha za kufadhili mchakato huo.

“Serikali inapasa kuelekeza fedha katika shughuli za kuwasaidia wahanga wa mafuriko wala sio kufadhili kura ya maamuzi kuhusu ripoti hii. Jopo hilo tayari limekusanya maoni kutoka kwa wananchi katika vikao ambavyo iliandaa kote nchini, ikitumia mamilioni ya fedha. Sasa kazi ambayo imesalia ni ya bunge kama asasi iliyopewa wajibu wa kikatiba wa kutunga sheria,” akasema Bw Kuria.

Na wiki jana, Spika Muturi alizima mipango ya kamati mbili za bunge la kitaifa kujadili ripoti ya BBI na kutoa mwelekeo kuhusu utekelezaji wake.

Kamati ya Bunge inayosimamia Utekelezaji wa Katiba (CIOC) inayoongozwa na Mbunge wa Ndaragua Jeremiah Kioni ilitaka idhini ya Spika ili iweze kufanya mikutano ya kuchambua ripoti hiyo katika mkahawa mmoja mjini Mombasa

Ombi sawa na hilo liliwasilishwa na Kamati ya Bunge la Kitaifa Kuhusu Haki na Masuala ya Kisheria inayoongozwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini William Cheptumo.

Kulingana na Bw Muturi kamati hiyo zinaweza tu kushughulikia ripoti hiyo endapo itawasilishwa bungeni kama mswada wa serikali au stakabadhi rasmi ya kisera kutoka kwa Ikulu ya Rais.

Bw Muturi pamoja na wakili Mwamu wanakubaliana kuwa mapendekezo ya ripoti ya BBI yanayohusu mageuzi ya mfumo wa uongozi sharti yaidhinishwe kupitia kura ya maamuzi.

“Kwa mfano, pendekezo la kubuniwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu, mawaziri kuteuliwa miongoni mwa wabunge na wale ambao watateuliwa kutoka nje kutawazwa kuwa wabunge linabadili mfumo wa uongozi. Kwa hivyo, suala hili sharti liamuliwe na raia katika kura ya maamuzi kulingana na kipengele cha 255 cha Katiba ya sasa,” akasema wakili huyu ambaye pia ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.