• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Sonko akataa chakula cha polisi, alia anaumwa

Sonko akataa chakula cha polisi, alia anaumwa

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko aliyeshtakiwa kwa ubadhirifu wa zaidi ya Sh381 milioni alikuwa anapelekewa chakula na vinywaji kutoka nyumbani kwake baada ya kukataa kula chakula cha polisi.

“Mteja wangu alikataa kabisa kula chakula kutoka mahala pengine isipokuwa kutoka kwa watu wa familia yake na mkewe. Hakuamini chakula na vinywaji kutoka mahala pengine ila kwa watu wa familia yake,” wakili Cecil Miller aliambia Taifa Leo Dijitali katika mahojiano ya faragha.

Hata Jumanne Sonko alipelekewa chakula katika seli ya mahakama ya Milimani alikozuiliwa.

Maafisa wa polisi walimruhusu Gavana Sonko awasiliane na mawakili hata akaruhusiwa kutoa taarifa kwa wafuasi wake “waduminishe amani hata mahakama itoe uamuzi katika kesi aliyofunguliwa.”

Gavana Sonko alipelekewa viatu na nguo zake zinazong’aa alipokuwa korokoroni. Pia kortini alikuwa amevalia nadhifu na ametulia tuli kama maji ya mtungi.

Lakini Bw Miller aliambia wanahabari hawezi kuzugumzia kule Sonko alikokuwa akilala kwa vile alikuwa akihojiwa na maafisa wa polisi na maafisa wa Tume ya Kupambana na Ufisadi Nchini (EACC).

Kiongozi wa mashtaka James Kihara katika wasilisho lake. Picha/ Richard Munguti

Bw Miller aliongeza kusema “kutokana na ripoti ya Dkt Esther Nafula Nekesa, Sonko analalamika yuko na maumivu makali kifuani na yuko na matatizo ya kupumua.”

Dkt Wekesa alipendekeza Sonko apimwe haraka iwezekanavyo kubaini iwapo “amevunjika mbavu.”

Bw Miller alisema Sonko anadai alijeruhiwa alipokuwa akitiwa nguvuni Voi kaunti ya Taita Taveta. “Yamkini Sonko alivunjika mbavu kutokana na kichapo alichopata akitiwa nguvuni Voi,” alisema Bw Miller.

Bw Miller aliomba hakimu mkuu anayesikiza kesi za ufisadi Douglas Ogoti amwachilie Sonko kwa dhamana na aamuru dhamana hiyo itumike katika kesi anayotazamiwa kushtakiwa katika mahakama ya Voi ya kuwajeruhi maafisa wa usalama.

Bw Sonko, mahakama ilifahamishwa, aliondolewa lawama katika madai kuwa alitoroka jela la Shimo la Tewa miaka ya 2000.

Bw Sonko, hakimu alielezwa kifungo alichokuwa akitumika katika gereza la Shimo la Tewa kilifutiliwa mbali na marehemu Jaji Samuel Oguk.

“Madai eti Sonko anasakiwa kwa makosa ya kutoroka gerezani hayana msingi wowote na hayana mashiko kisheria kwani aliachiliwa huru ya Mahakama kuu mwaka wa 2000,” alisema Bw Miller.

Kesi dhidi ya Bw Sonko imevutia watu wengi jijini Nairobi. Picha/ Richard Munguti

Pia alisema aliyekuwa hakimu mkuu Cecilia Githua ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama kuu mwaka wa 2000 aliamuru Sonko azuiliwe kwa siku 19 katika kituo cha polisi cha Kileleshwa.

Hakimu alifahamishwa afisa mkuu wa Polisi Muga Nyale alichunguza madai yoyote dhidi ya uhalifu na “kueleza korti katika ripoti kwamba Sonko hakuwa na dosari.”

Alisema madai Sonko alitoroka jela yangefikia ukingoni pale alipotembelea gereza la Shimo la Tewa kushauriana na wafuasi sugu wa kundi la Mombasa Republican Council (MRC).

Aliwalipia dhamana wafuasi wa MRC waliokuwa wameshtakiwa.

 

You can share this post!

Kibra United, Gogo Boys zalenga Ligi ya Taifa

Jogoo wa jiji alivyozimwa, sasa ajikunyata

adminleo