• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 10:55 AM
Afisa wa ‘Taifa Leo’ ashinda tuzo ya kimataifa

Afisa wa ‘Taifa Leo’ ashinda tuzo ya kimataifa

Na WANDERI KAMAU

MMOJA wa wasimamizi wakuu wa gazeti la Taifa Leo Bw Nuhu Bakari ameibuka mshindi kwenye tuzo za kimataifa kuhusu tafsiri.

Bw Bakari, almaarufu kama Al Ustadh Pasua aliibuka bora barani Afrika katika shindano lililoandaliwa na shirika la Proz.Com, lenye makao yake jijini New York nchini Amerika.

Kauli mbiu ya shindano hilo ilikuwa “The 21st Century Translation Contest: The Tides of Tech” (Shindano la Tafsiri katika Karne ya 21: Mawimbi ya Teknolojia).

Kwa mujibu wa Bw Bakari, mchakato wa kuwateua washindi ulikuwa wenye ushindani mkali kwani zaidi ya watu 100 walishiriki. Shindano hilo lilichukua muda wa miezi minne.

“Katika awamu ya kwanza, washiriki zaidi ya 100 walituma nakala yao kwa kundi la majaji. Idadi hiyo ilipuguzwa hadi chini ya watu 10 kwa mujibu wa ubora wa makala. Makala yangu yalitangazwa bora na majaji,” akasema.

Kati ya watu watatu bora kwenye shindano hilo, wawili wao ni Wakenya. Mkenya Bw Frederick Otiato ndiye aliibuka wa pili.

Bw Bakari amekuwa mtetezi wa lugha ya Kiswahili kwa muda mrefu kupitia vyombo mbalimbali vya habari kama vile kipindi cha Kamusi ya Changamka kilichopeperushwa na mwanzo kabisa na Idhaa ya Nation FM na baadaye mubashara kwa sambamba kupitia runinga ya Qtv na Qfm vyote hivi vikiwa vituo vinavyomilikiwa na kampuni ya Nation Media Group.

Vile vile, alikuwa miongoni mwa wale waliohusika kwenye mchakato mzima wa tafsiri ya Rasimu ya Katiba ya 2010.

Kikosi kizima cha Taifa Leo pamoja na Kampuni ya Nation Media Group ilimmiminia sifa kede kede ulama huyu wa masuala ya lugha na utangazaji na kumtakia kila la kheri katika juhudi zake za kukuza ya Kiswahili.

You can share this post!

Mke alimsukuma mwanangu baharini, mama sasa alia

Msichana amuua mwanamume aliyemtongoza

adminleo