HabariSiasa

Eric Wainaina atunga wimbo akimuumbua Sonko

December 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MARY WANGARI

MWANAMZIKI aliyevuma Eric Wainaina amechangamsha mitandao ya kijamii kufuatia wimbo wake mpya akimdhihaki Gavana wa Nairobi Mike Sonko anayekabiliwa na wakati mgumu pamoja na maafisa wakuu serikalini.

Mwimbaji huyo nyota alijitosa katika mtandao wa kijamii wa Twitter mnamo Jumatano, Novemba 11, huku akicheza kinanda, aliimba kibao hicho akiwashauri wanasiasa kutoka chama tawala cha Jubilee kusafisha mazingira ya jela za Kenya maadamu huko ndiko wanaelekea hatimaye.

“Hapa kuna ngoma mnayoweza kusakata. Safisheni magereza Jubilee kwa kuwa huko ndiko mnakoelekea. Boresheni mazingira ya jela, mnaenda nyumbani,” aliimba.

Mwimbaji huyo wa kibao kilichovuma cha Nchi ya Kitu Kidogo pia alisisitiza ujumbe huo kwa bosi wa kaunti ya Nairobi aliyefikishwa kortini mnamo Jumatatu, kufuatia kukamatwa kwake Ijumaa, kuhusiana na madai ya ufisadi.

“Ng’arisha magereza Bw Sonko maadamu humo ndimo unamoelekea. Boresha mazingira yake, unaenda nyumbani, sakata ngoma hiyo bwana mkubwa,” ulisema wimbo huo.

Isitoshe, msanii huyo alimkashifu gavana kwa kumshambulia afisa aliyekuwa akimkamata huku akihoji kwamba, ilikuwa haki kwa kiongozi huyo kuhudumu kifungo chake cha jela ingawa katika mazingira safi, kwa makosa aliyotenda.

“Sitaki mtu yeyote avunjiwe heshima hata ingawa hii ilikuwa hali ya kulipiza kisasi tunapaswa kupiga foleni ili kukuzaba makofi sawa na jinsi ulivyomfanyia Mkenya huru kwenye video,”

“Natumai uishi maisha ya hadhi – yenye vitabu, runinga, ziara za haki za ndoa, kutembelewa kila mara, bila kunguni, wanyama wa aina yeyote – lakini ukiwa gerezani kwa muda unastahili kutii sheria,” alieleza.

Kwa wafuasi wake Sonko, mwanamziki huyo pia alikuwa na ujumbe wa kuwafariji akiwahakikishia kuwa maadui wa gavana huyo kisiasa, pia wangefuata mkondo huo.

“Na kwa wale wote wanaoandika mitandaoni wakikuunga mkono wakidai kuwa umetelekezwa ninasema, msijali. Tutawaandama maadui zako kisiasa vilevile. Hapa kuna wimbo unaoweza kusikiza huku ukisubiri,” alishauri.

Mwimbaji huyo aliyegeuka kuwa mwalimu wa mziki katika Shule ya Kimataifa ya Brookhouse, Karen, si mgeni kwa kashfa, kutokana na ujasiri wake wa kuwakashifu viongozi wakuu kwa kuendeleza ufisadi na maovu ya kijamii.

Wainaina aligonga vichwa vya habari mnamo 2001 baada ya utawala wa Rais Mstaafu Daniel Moi kupiga marufuku kibao chake maarufu ‘Nchi ya Kitu Kidogo’ kilichoangazia maovu yaliyokithiri nchini yaliyoendelezwa na wanasiasa.