Makala

'Uuzaji matunda unalipa kuliko biashara ya bodaboda'

December 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

NA SAMMY WAWERU

CHINI ya utawala wa rais mstaafu Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, Henry Kamau alikuwa mmoja wa walionufaika na biashara iliyoibuka ya bodaboda.

Hata ingawa wakati huo zilikuwa bei ghali, Bw Kamau alijikakamua na kuwekeza katika sekta hiyo ya usafiri na uchukuzi.

Ni sekta ambayo imebuni nafasi za ajira kwa mamilioni ya vijana, waliokumbatia huduma za bodaboda. Zinasifiwa kwa uwepesi wake kuingia maeneo yasiyoweza kuingilika hususan kwa magari.

Miaka minane baadaye, Kamau alihisi amechoshwa na kazi hiyo. Japo ina mapato ya haraka, anasema ina changamoto zake.

“Mwendeshaji asipovalia mavazi mazito, anahatarisha kuugua kifua kwa sababu ya upepo kwa ajili ya kasi yake. Pia msimu wa mvua iwapo hana mwavuli kugonjeka Kifua Kikuu ni rahisi,” afafanua.

Licha ya bodaboda kuwa zenye manufaa tele, zimehusishwa na visa vya uhalifu kama vile wizi wa nguvu za kimabavu. Isitoshe, wahudumu wenyewe wamejipata kunyang’anywa pikipiki.

Akikumbuka pandashuka hizo, mwishoni mwa mwaka uliopita Kamau alichukua hatua nyingine, kuwekeza kwenye biashara na anasema moyo wake sasa ni tulivu.

Mjasirimali huyo huuza matunda aina mbalimbali kama vile machungwa, ndizi, maparachichi, matundadamu maarufu kama tree tomato, maembe, miongoni mwa mengine.

Anaiambia Taifa Leo Dijitali kwamba ilimgharimu mtaji wa Sh4, 000 pekee kuingilia biashara hiyo ambayo kwa sasa inampa tabasamu.

Anafafanua kwamba alinunua mwavuli mkuukuu wa Sh1, 000, kujenga kibanda tamba na kununua matunda ya kuanzisha yakagharimu pesa zilizosalia.

“Uuzaji wa matunda ni biashara inayoshika kasi upesi, haina vikwazo vile kwa kuwa yana walaji wengi,” asema Bw Kamau ambaye ni baba wa watoto watatu.

Shughuli hiyo anaiendeshea eneo la Progressive, ambalo linaunganisha mtaa wa Githurai na Mumbi na Mwihoko. Yuko pembezoni mwa barabara yenye wapita njia wengi. “Biashara inahitaji kulenga mahala maalum, hasa penye watu wengi,” ashauri.

Ni mwendo wa saa sita hivi za mchana, tunampata akiwa katika harakati za kukokotoa hesabu ya mauzo yake. “Biashara, iwe kidogo au kubwa inapaswa kuwa na rekodi na ndio maana nasawazisha hesabu ya kununua bidhaa na mauzo kwenye kitabu hiki,” anasema, akionekana kuzamia shughuli hiyo.

Ananakili idadi ya matunda, kwa mujibu wa aina yake, bei aliyonunua. Jioni, ataondoa na kujaza yaliyosalia, pamoja na mapato kuona iwapo amepata faida.

Mojawapo ya mashine ya kuunda sharubati, ili kuongeza thamani kwa matunda. Bw Kamau anapania kukumbatia wazo hilo. Picha/ Sammy Waweru

“Kando na faida, rekodi hii pia inaniongoza kujua matunda yanayonunuliwa kwa kasi na yenye faida,” aeleza. Hata ingawa biashara haitabiriki, Bw Kamau anasema uuzaji wa matunda una faida.

“Nikilinganisha na kazi niliyoifanya awali – uendeshaji bodaboda, gange hii haina changamoto nyingi,” aisifia.

Anafichua kwamba siku bora hakosi kupata faida ya Sh1, 000, akidokeza kwamba majira ya jioni ndipo biashara hiyo hunoga hasa watu wakitoka kazini kuelekea katika makazi yao. Hata hivyo, baridi ikisheheni kiwango cha mauzo hushuka.

Mfanyabiashara huyo anasema huyaendea katika soko la ‘Migingo’ ndogo, lililoko mtaa wa Githurai. “Matunda humo huuzwa kwa bei nafuu, haswa kwa wanaoyauza kwa kijumla,” akasema.

Ili kuimarisha biashara hiyo, Dennis Muchiri ambaye ni mjuzi wa masuala ya kiuchumi na biashara anahimiza haja ya kutathmini uongezaji thamani kwa matunda (value addition).

Katika muktadha huo, anaeleza kuhusu utengenezaji wa sharubati ya matunda. “Kuna vifaa ambavyo huunda sharubati. Msimu wa jua wengi wanapenda kuzima kiu kwa vinywaji baridi,” aeleza mtaalamu Muchiri.

Isitoshe, mdau huyo anasema mfanyabiashara muuzaji wa matunda ataweza kuepuka kero la bidhaa za aina hiyo kuoza upesi.

Mengi ya masoko nchini matunda yaliyooza, hasa kwa sababu ya kukosa wateja haykosi kutapakaa, suala ambalo mtaalamu anasema litaepukwa kwa kukumbatia uongezaji wa thamani.

Kero la mawakala, ambao wameshika mateka masoko na wakulima wazalishaji wa bidhaa za kilimo pia linachangia kuoza. Hilo hasa linashuhudiwa shambani ambapo wakulima wananunuliwa mazao na madalali kwa bei duni.

Pia, kuna mashine za kipekee zinazotumika kutengeneza sharubati, pia juisi. Aidha, mashine hizo hutengeneza juisi kwa matunda mbalimbali, na pia kuchanganywa na ile ya mia.

Ili kupata soko baadaye, mwekezaji anaweza kufikiria namna ya kuhifadhi sharubati kwa jokofu. Wakati wa mahojiano Bw Henry Kamau alisema anapania kupanua kibanda chake kiwe sawa na green grocer – maduka maalum ya kuuza matunda.

Hilo likiafikika, anasema ataweza kuongeza thamani bidhaa zake ili kupanua soko. “Nina matumaini biashara hii ikipanuka nitaweza kukumbatia wazo la uongezaji thamani,” akasema.