MAKALA MAALUM: Wiper yaanza kusaka kura za 2022 mapema
Na KITAVI MUTUA
CHAMA cha Wiper kimeanza mikakati ya kuwarai vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini kujiunga nacho kwenye harakati za matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.
Kwenye mikakati hiyo, chama kinawashinikiza vijana kuchukua nyadhifa za uongozi ili kukipa sura ya kitaifa.
Wale watakaochukua nyadhifa hizo watatwikwa majukumu ya kuwatafuta wanachama zaidi, ili kuondoa dhana kwamba uwepo wake ni katika eneo la Ukambani pekee.
Mwenyekiti wake wa kitaifa, Prof Kivutha Kibwana, alisema kuwa wanapanga kuitisha Kongamano la Kitaifa la Wajumbe ili kujadiliana kuhusu mpango wa kubadili jina lake kutoka Wiper hadi One Kenya Movement (OKM).
Mipango mingine iliyowekwa ni maandalizi ya ziara za viongozi wake wakuu chini ya uongozi Kalonzo Musyoka katika nchi za Ulaya. Ziara hizo ni za kuwawezesha viongozi hao kufahamu njia za kuendesha vyama vya kisiasa ili kuviimarisha kuwa vya kitaifa.
“Tunakigeuza chama ili kuwafikia Wakenya zaidi kama njia moja ya kutuwezesha kufikisha ushindani wetu katika kiwango cha kitaifa, hasa tunapojitayarisha kwa uchaguzi wa urais mnamo 2022,” akasema Prof Kibwana, aliye pia Gavana wa Makueni.
Mwenyekiti huyo alisema kwamba Bw Musyoka atazuru Uingereza, ili kushauriana na viongozi wa vyama vya Conservative na Labour. Katika ziara hiyo, Bw Musyoka pia atakutana na Wakenya wanaoishi jijini London, kwenye juhudi za kutafuta uungwaji mkono kwa Wakenya wanaoishi ughaibuni.
Kumvumisha Kalonzo
Kulingana na waandani wa karibu chamani, mpango huo unalenga kuimarisha ushawishi wa Bw Musyoka kisiasa. Vile vile, unalenga kumsaidia kutafuta miungano zaidi ya kisiasa itakayompa nguvu kisiasa anapojitayarisha kuwania urais kwa mara ya pili.
Miaka minane iliyopita, chama hicho kilibadilisha jina lake kutoka ODM Kenya hadi Wiper Democratic Movement (WDM).
Chama pia kilibadilisha nembo zake kutoka chungwa moja na nusu na kuanza kutumia mwamvuli.
Zaidi ya hayo, kilibadilisha rangi yake kutoka rangi ya chungwa ambapo kilianza kutumia samawati, kuashiria matumaini.
Hii ni mara ya pili kwa chama kubadilisha mwonekano wake, japo ingali kubainika ikiwa kitabadili nembo na rangi zake.
Kulingana na Prof Kibwana, chama kilianza mikakati ya mageuzi pindi tu baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti, ili kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza baada ya uchaguzi huo. Mojawapo ya mipango hiyo ilikuwa kuimarisha udhibiti wake wa kisiasa katika eneo la Ukambani.
Hatua ya kwanza ilikuwa kutia saini mwafaka wa kisiasa na chama cha Narc, ambacho kinaongozwa na Gavana Charity Ngilu wa Kitu.
Wiper kumsaidia Ngilu
Kwenye mwafaka huo, Wiper itamsaidia Bi Ngilu kutekeleza manifesto yake, ikizingatiwa chama chake kina idadi ndogo wa madiwani katika Bunge la Kaunti ya Kitui. Kwa upande wake, Bi Ngilu atamsaidia Bw Musyoka kuyafikia maeneo mengine.
Na kutokana na mwafaka huo, huenda Bi Ngilu akatetea kiti chake cha ugavana kwa tiketi ya chama cha Bw Musyoka mnamo 2022, kama walivyofanya Prof Kibwana na Bi Wavinya Ndeti, aliyewania ugavana katika Kaunti ya Machakos.
Mnamo 2013, wawili hao waliwania nyadhifa hizo kwa Chama Cha Muungano (CCM) na Chama Cha Uzalendo (CCU) mtawalia. Hata hivyo, waliwania kwa tiketi ya Wiper kwenye uchaguzi wa Agosti.
Aidha, Prof Kibwana alisema kwamba ushirikiano huo wa kisiasa utavifaidi vyama hivyo viwili, hasa katika uendeshaji wa serikali za kaunti.
Mwafaka huo ndio ulipelekea kuandaliwa kwa mkutano wa viongozi wa jamii ya Akamba katika eneo la Komarock, Machakos, mapema wiki iliyopita.
Kwenye mkutano huo, Bw Musyoka alipewa kibali cha kutafuta uungwaji mkono na ushirikiano wa kisiasa kutoka maeneo mengine.
Aliyekuwa Seneta wa Machakos, Johnstone Muthama, alitangaza kurudi kwake katika Wiper, ili kumsaidia Bw Musyoka kufikia malengo yake. Awali, Bw Muthama alikuwa ametangaza kujiondoa katika chama hicho, akidai ukosefu wa uongozi mzuri.
Kwa miaka mingi, siasa za Ukambani zimehimiliwa na uhasama mkubwa wa kisiasa kati ya Bw Musyoka na Bi Ngilu, ambaye ashatangaza nia ya kumuunga mkono Musyoka kuwania urais mnamo 2022.
Vigumu kuvuruga
Na kutokana kuungana kwa wawili hao, wale ambao wataupinga watakuwa na kibarua kigumu kujinadi kisiasa katika eneo hilo.
Bi Ngilu alitangaza kwamba wale ambao wanalenga kugawanya kura za Ukambani watakuwa na kazi ngumu.
“Lazima tuungane sote ili kuhakikisha kwamba jamii ya Akamba inamuunga mkono mtoto wetu (Kalonzo) ili kuanza harakati za kutafuta uungwaji mkono wa kisiasa mapema,” akasema.
Kuna kambi mbili zinazompinga Bw Musyoka, moja ikiongozwa na Gavana Alfred Mutua wa Machakos, huki nyingine ikiongozwa na wabunge Victor Munyaka (Machakos Mjini), Rachael Nyamai (Kitui Kusini) na Nimrod Mbai (Kitui Mashariki).
Hata hivyo, kambi hizo zina miegemeo tofauti ya kisiasa; kwani Dkt Mutua ametangaza kuwania urais mnamo 2022, huku wabunge hao wakitangaza kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto.