• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
JAMHURI DEI: Matarajio makuu ya Wakenya kutoka kwa hotuba ya Rais

JAMHURI DEI: Matarajio makuu ya Wakenya kutoka kwa hotuba ya Rais

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuelezea Wakenya hatua ambazo serikali yake imepiga kutekeleza Ajenda Nne Kuu atakapohutubia taifa kwenye maadhimisho ya 56 ya Jamhuri Dei.

Ingawa siku hii inapaswa kuwa ya kukumbuka ufanisi wa nchi tangu ilipokabidhiwa mamlaka ya ndani, marais wamekuwa wakiitumia kueleza ufanisi wa serikali zao na mipango ambayo inaweka kutimiza ajenda zake.

Mbele ya maelfu ya Wakenya wanaotarajiwa kuhudhuria sherehe katika uwanja wa michezo wa Kasarani na mgeni wa heshima, waziri mkuu wa Barbados Mia Amor Mottley, Rais Kenyatta ataeleza anayotarajia serikali yake itimize katika muda wa miaka miwili na nusu iliyobakia.

Ajenda hizo ni utoshelezaji wa chakula, viwanda, makao na afya kwa wote.

Ingawa Serikali imepiga hatua katika kufanikisha mpango wa afya kwa wote, imejivuta katika ujenzi wa nyumba 500,000 za bei nafuu, ufufuzi wa viwanda huku kampuni nyingi zikiwa zimezama au kuhamia nchi nyingine na kuacha maelfu ya Wakenya bila ajira.

Ni machache iliyofanya kusaidia wakulima kuongeza ukuzaji wa mazao Kahawa, Majanichai na Mahindi.

“Nafikiri Rais atafafanua hali ilivyo na mipango ya serikali yake kuendelea mbele. Kumbuka ana chini ya miaka mitatu kutimizia Wakenya ahadi alizowapa na kuacha kumbukumbu,” alisema mtaalamu wa masuala ya utawala, Bonface Maina.

Ukiwa wakati ambao vita dhidi ya ufisadi vimeshika kasi huku baadhi ya maafisa wa serikali wakikabiliwa na mashtaka kortini, Rais Kenyatta anatazamiwa kutangaza kuwa serikali yake inaendelea kutimiza moja ya ahadi alizotoa kwenye sherehe za Jamhuri mwaka jana.

“Hatutatimiza maono yetu ya kuwa na Kenya bora kwa Wakenya wote iwapo sisi, kama taifa, hatutaungana kuangamiza zimwi hili la ufisadi. Ni kwa sababu hii ambapo tumezidisha vita dhidi ya ufisadi,” Rais Kenyatta alisema kwenye hotuba yake siku ya Jamhuri mwaka jana.

Alisema vita dhidi ya ufisadi havingemsaza yeyote na anatarajiwa kutangaza hatua kali zaidi huku maafisa zaidi wa serikali wakitarajiwa kufikishwa kortini.

Ikizingatiwa kuwa sherehe za mwaka huu zinafanyika wakati ambao mjadala kuhusu ripoti ya Jopokazi la Maridhiano unaendelea, Rais Kenyatta anatazamiwa kutilia mkazo msimamo wake kuihusu na itakavyofaidi Wakenya.

Rais Kenyatta pia anatarajiwa kuangazia sekta ya elimu hasa baada ya Kenya kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani, usalama wa Wakenya na uhusiano na mataifa ya nje hasa wakati huu inapogombea uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Chini ya utawala wa Rais Kenyatta Kenya imepanua ushirikiano wake na mataifa mengi ulimwenguni hasa barani Afrika.

You can share this post!

Wezi waogelea katika mafuriko kuibia wahamaji

JAMHURI DEI: Uhaba wa chakula bado donda ndugu mamia wakifa...

adminleo