JAMHURI DEI: Uhaba wa chakula bado donda ndugu mamia wakifa njaa kila mwaka
Na CHARLES WASONGA
TANGU taifa hili lipate uhuru 1963, kilimo kimetajwa kama nguzo kuu ya uchumi wa taifa. Hata hivyo, sekta hiyo imekabiliwa na changamoto nyingi na kupelekea taifa kutojitosheleza kwa chakula.
Huku Kenya ikiadhimisha leo miaka 56 tangu itawazwe kuwa Jamhuri, wakulima wa mimea kama vile miwa, mahindi, kahawa, majani chai, pareto na viazi kati ya mazao mengine hawana furaha kwani mapato yao yamekuwa yakishuka kila uchao.
Lakini kwa upande wake, Serikali ya Kitaifa imechelea kuweka mikakati madhubuti kukabili changamoto katika sekta hii huku ikiendelea kuinyima ufadhili wa kutosha.
Kwa mfano, katika bajeti ya mwaka huu wa kifedha, 2019/2020 ya kima cha Sh3.02 trilion sekta ya kilimo ilitengewa Sh52 bilioni, sawa na asilimia 2.9 ya bajeti hiyo. Hii ni licha ya kwamba kilimo huchangia asilimia 26 ya jumla ya utajiri wa nchini (GDP).
Mgao huo, wa Sh52 bilioni, unakwenda kinyume na Mwafaka wa Malabo, nchini Equitorial Guinea 2014, ambapo viongozi wa mataifa ya Afrika, ikiwemo Kenya, walikubaliana kutenga angalau asilimia 10 ya bajeti zao kwa sekta ya Kilimo. Lengo hapo lilikuwa ni kupiga jeki sekta hii ili itimize kiwango cha ukuaji cha asilimia 6.
Kulingana na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF), Kenya inatarajia kuandikisha kiwango cha ukuaji wa kiuchumi wa hadi asilimia 6.2 katika mwaka huu wa kifedha unaokamilika Juni 30, 2020. Sekta ya Kilimo ni mojawapo ya zile ambazo shirika hilo limetambua kuchangia ukuaji huo.
Lakini utekelezaji wa kiholela wa sera za kilimo, mabadiliko ya hali ya anga, ukosefu wa fedha za kufadhili tafiti za kilimo kati ya changamoto zingine zinaendelea kuizonga sekta hiyo.
Na licha ya uwepo wa chakula cha kutosha nchini kuorodheshwa mojawapo ya Nguzo Nne Kuu za Serikali ya Jubilee, serikali haijachukua hatua za kimakusudi kuimarisha kilimo cha zao hili. Gharama ya uzalishaji ni juu kufuatia kupanda kwa bei ya pembejeo muhimu kama vile mbolea huku wakuzaji wakilipwa bei duni ya Sh2,300 kwa gunia.