• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
JAMHURI DEI: Wakenya bado walia kuhusu umiliki wa ardhi

JAMHURI DEI: Wakenya bado walia kuhusu umiliki wa ardhi

Na CHARLES WASONGA

HAKI za umiliki wa ardhi imekuwa suala nyeti nchini Kenya tangu taifa hili lilipopata uhuru kutoka kwa mkoloni.

Msukumo mkubwa wa waliopigania uhuru wa taifa hili ulikuwa ni kupata haki ya kumiliki ardhi, ikizingatiwa kuwa rasilimali hii ni hitali la kimsingi katika shughuli zozote za uzalishaji chakula na mali.

Waafrika walitaka kukomboa ardhi yao ambayo ilitwaliwa na wakoloni mwishoni mwa karne ya 18.? Lakini kinaya ni kwamba baada ya Kenya kupata uhuru, ardhi iliendelea kuwa chanzo cha mizozo kati ya jamii mbalimbali nchini kando na matabaka ya matajiri na masikini kuwa sababu.

Walioingia mamlakani walipokonya masikini ardhi, haswa katika maeneo ya Pwani na Rift Valley kwa sababu hapakuwa na sera madhubuti ya kuongoza usimamizi na umiliki wa ardhi nchini Kenya.

Ghasia za kikabila zilishamiri katika sehemu kadha za mkoa wa Rift Valley mapema miaka ya tisini kutokana na hisia miongoni mwa makabila ya huko kwamba ardhi yao ilitwaliwa na “walowezi weusi”.

Wakenya wanakumbuka kuwa maovu ya kihistoria kuhusiana na umiliki na usimamizi wa ardhi ndio kati ya sababu zilizochangia kutokea kwa ghasai za kisiasa za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Ni kwa sababu hii ambapo Serikali ilitangaza kujitolea kutoa suluhu la mwisho kwa tatizo la ardhi nchini kama njia ya kupalilia amani na utangamano kote nchini.

Isitoshe, Katiba ya sasa imebuni Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) na kuweka misingi ya kisheria ambayo kwayo matatizo yanayozingira usimamizi na umiliki wa ardhi yatapata uvumbuzi.

Lakini juhudi za serikali za kufanikisha mageuzi katika sekta ya ardhi nchini huenda zikagonga mwamba kufuatia pingaminzi zinazokumba miswada kadha kuhusu ardhi itakayojadiliwa bungeni wiki hii.

Kwa mfano, wabunge kutoka eneo la Pwani wametaja Mswada kuhusu Ardhi ya Kijamii, 2015 kama itakayoongeza dhuluma za kihistoria kuhusu ardhi katika eneo hilo kwani unaweka usimamizi wa ardhi ya kijamii chini ya serikali kuu.

You can share this post!

JAMHURI DEI: Juhudi kuleta usawa katika elimu zatiliwa mkazo

JAMHURI DEI: Utangamano bado ni fumbo

adminleo