• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
JAMHURI DEI: Utangamano bado ni fumbo

JAMHURI DEI: Utangamano bado ni fumbo

Na BENSON MATHEKA

KENYA inaadhimisha miaka 56 ya kujitawala huku kukiwa na mjadala kuhusu juhudi za kubadilisha katiba ili kuimarisha uwiano na ushirikishi.

Kupitia ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), inatarajiwa kuwa baadhi ya vifungu vya katiba iliyopitishwa 2010 vitafanyiwa mageuzi kutekeleza mapendekezo ya ripoti ya kamati iliyoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Japo Kenya imekuwa na marais wanne tangu uhuru, siasa za nchi hii zimejikita katika familia za Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Baba ya Uhuru, Mzee Jomo Kenyatta alikuwa rais wa kwanza wa Kenya naye Jaramogi Oginga Odinga, baba ya Raila alikuwa makamu wa rais wa kwanza wa Kenya huru.

Wawili hao walitofautiana 1969 na wadadisi wanasema tofauti zao ndizo chimbuko la matatizo ya siasa za Kenya.

Katiba iliyopitishwa 2010 ilikuwa ya kwanza kuandaliwa na Wakenya wenyewe.

Hata hivyo, ilichukua miaka 20 ya umwagikaji wa damu wanaharakati waliotaka mabadiliko wakikadamizwa na serikali ya chama cha Kanu kilichotawala Kenya kwa miaka 40 chini ya katiba ambayo nchi ilirithi kutoka kwa wakoloni.

Wanaharakati walianza kwa kupigania mfumo wa siasa za vyama vingi vya kisiasa ambao ulikubaliwa 1992. Mfumo wa vyama vingi vya kisiasa uliweka hitaji la rais kuhudumu kwa vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja.

Baada ya siasa za vyama vingi kukubaliwa, wanaharakati walianza kupigania mabadiliko ya kikatiba ili kuhakikisha kulikuwa na utawala bora uliokumbatia usawa wa kimaeneo, haki za binadamu na demokrasia.

Ni baada ya uchaguzi mkuu wa tatu chini ya mfumo wa utawala wa vyama vingi uliofanyika 2007 ambapo Kenya ilikubwa na ghasia mbaya zaidi za kisiasa na kikabila ambapo watu 1,300 walikufa na zaidi ya 600,000 kufurushwa makwao.

Kupitia juhudi za upatanishi zilizoongozwa na jamii ya kimataifa, vyama vya kisiasa vilivyokuwa vikizozona viliunda serikali ya muungano Mwai Kibaki akiwa na Rais na Bw Odinga akiwa Waziri Mkuu. Hii ilituliza joto la kisiasa nchini na mchakato wa kubadilisha katiba ukaanza.

Mnamo Agosti 4 Wakenya kupitia kura ya maamuzi walipitisha katiba mpya iliyozinduliwa Agosti 27 mwaka huo.

Wengi walifungwa jela, kulemazwa na kufariki wakipigania katiba ambayo hata baada ya kupitishwa 2010, haikutekelezwa kikamilifu.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kwamba Kenya imepiga hatua kubwa chini ya katiba ya sasa ambayo ilileta utawala wa maeneo kukawa na kaunti 47.

Chini ya utawala huu, Wakenya wanafurahia maendeleo na hudumu bora katika maeneo yao.

Japo Kenya imeafikia ustawi mkubwa wa kiuchumi tangu 1964 ilipokuwa Jamhuri, wadadisi wanasema ghasia za kisiasa ambazo zimekuwa zikitokea kila baada ya miaka mitano zimekuwa zikitia doa sifa za nchi hii.

Mnamo 2017, kwa mara ya kwanza nchini na barani Afrika, uchaguzi wa kura ya urais ulibatilishwa na mahakama.

Rais Kenyatta wa chama cha Jubilee aliyekuwa amechaguliwa kwa kipindi cha pili alikubali kushiriki uchaguzi wa marudio lakini mpinzani wake Raila Odinga alijiondoa akitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ifanyiwe mageuzi kwanza.

Baada ya uchaguzi wa marudio, Rais Kenyatta wa chama cha Jubilee alitangazwa mshindi lakini Bw Odinga wa muungano wa NASA alijitangaza rais wa wananchi na kujiapisha katika hafla iliyofanyika bustani ya Uhuru Park Januari 30.

Muafaka wao wa Machi 9 2018 ulishangaza wengi wakiwemo washirika wao wa karibu ambao walikuwa gizani.

Wawili hao walieleza kwamba waliweka kando tofauti zao za kisiasa ili kuunganisha nchi, kupigana na ufisadi, ukabila, kukuza uwiano, kuimarisha ugatuzi na kuhahakikisha kuna ushirikishi serikalini.

“Tumeamua kuzika tofauti zetu na kujenga daraja za urafiki,” walisema na kuzindua kamati ya watu 14 ambayo ilikusanya maoni kutoka wakazi wa kaunti zote kuandaa ripoti kuhusu mabadiliko waliyotaka ili kuafikia malengo ya wanasiasa hao.

Hata hivyo, ripoti hiyo iliyotolewa mwezi jana, imezua mgawanyiko kuhusu utekelezaji wake.

You can share this post!

JAMHURI DEI: Wakenya bado walia kuhusu umiliki wa ardhi

JAMHURI DEI: Wakenya nchini Canada kujumuika kuadhimisha...

adminleo