JAMHURI DEI: Wakenya nchini Canada kujumuika kuadhimisha siku
NA CHRIS WAMALWA
WAKENYA nchini Canada Jumamosi wataadhimisha Sikukuu ya Jamhuri baada ya serikali ya taifa hilo kuungana nao kutambua siku hiyo muhimu kwenye ukombozi wa taifa hili.
Sherehe hiyo itaandaliwa katika mji wa Brampton katika mkoa wa Ontario na itahudhuriwa na Meya wa mji huo, Patrick Brown.
Ingawa siku hiyo inaadhimishwa nchini leo, Wakenya wanaoishi Canada watashiriki sherehe hiyo kesho kutwa huku Kenya ikitunikiwa heshima hiyo baada ya serikali ya nchi hiyo kuruhusu upeperushaji wa bendera kwa muda wa wiki mbili zijazo.
Aidha, imebainika kwamba Wakenya nchini Canada watatunukiwa nafasi ya kuadhimisha siku hiyo muhimu kila mwaka baada ya ombi lao kupitia Muungano wa Wakenya wanaoishi humo kukubaliwa na wakapokezwa cheti cha kuidhinisha sherehe hiyo.
Hafla ya kupandishwa kwa bendera ya Kenya katika jiji la Brampton itahudhuriwa na viongozi wa kisiasa na jamii wakiwemo wabunge, viongozi wa bunge la mkoa, wenzao wa kimaeneo na madiwani wa manispaa kutoka jimbo kubwa la Toronto.
Balozi wa Kenya nchini Canada pia anatarajiwa kutuma mwakilishi wake kwenye hafla hiyo ambayo itakuwa ya kwanza ya aina yake kuandaliwa nchini Canada.
“Hii ni hatua kubwa siyo tu kwa Wakenya wanaoishi Canada bali kwa taifa zima. Ni jambo la kujivunia kuiona serikali ya Canada kwa mara ya kwanza ikitambua mchango wa Wakenya katika taifa lao. Hii ni ishara kwamba uhusiano kati ya Wakenya wanaoishi Canada utakuwa imara nayo mataifa haya mawili pia yatakuwa na uhusiano mzuri,” akasema Rais wa Muungano wa Wakenya wanaoishi Canada(KCA) Ephraim Mwaura.
Muungano wa KCA haujikiti katika kupata faida ila kutatua masuala yanayowahusu Wakenya wanaoishi nchini humo.
KCA pia huwasaidia Wakenya wageni wanaoanza maisha au kazi nchini Canada na kuwashauri namna wanavyoweza kutimiza malengo yao au ndoto zao.