• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
AKILIMALI: Ajabu ya mkulima aliyeacha ufugaji wa kuku na kuanza kufuga mbwa

AKILIMALI: Ajabu ya mkulima aliyeacha ufugaji wa kuku na kuanza kufuga mbwa

NA STEVE NJUGUNA

KUFIKIA mwaka wa 2016, mayai yaliyoingizwa humu nchini kutoka mataifa ya nje yalikuwa yameanza kufurika katika masoko ya Kenya na wafugaji wengi wa kuku walikuwa wakiamua kuachana na ufugaji huo.

Wakulima hao walikuwa wameanza kujitahidi kupambana kustahimili ufugaji huo kutokana na gharama kubwa ya chakula cha kuku ikilinganishwa na mapato ya chini ya kazi hiyo.

Hii ndiyo sababu iliyomfanya Bw Michael Njoroge kuachana na ufugaji huo na kujiingiza katika ufugaji wa mbwa, biashara anayosema kuwa mafanikio yake yamemshangaza hata yeye mwenyewe.

Kwa miaka miwili iliyopita, Bw Njoroge ambaye ni mkaaji wa mtaa wa Huruma katika mji wa Ol Kalou, Kaunti ya Nyandarua alikuwa ni mfugaji mashuhuri wa kuku kwani alikuwa amefuga zaidi ya kuku 200 wa Kienyenji katika shamba lake dogo.

Kwa viwango vyote, majirani walimwona Bw Njoroge mwenye umri wa miaka 30 kama mfugaji wa kuku aliyefanikiwa maishani kwa sababu ya idadi kubwa ya kuku aliowafuga.

Bw Njoroge, ambaye taaluma yake ni upishi anasema kuwa aliamua kujiingiza katika ufugaji wa kuku kwani tangu jadi alikuwa akipendezwa na ndege na mifugo.

Anasema kuwa siku moja, aliamua kupeleka trei kadhaa za mayai na kuku 10 sokoni.

“Wakati huo ndipo niligundua kuwa haikuwa rahisi kupata faida kwa kuuza mayai huko nje kwa sababu soko lilionekana limejaa mayai kutoka nje ya nchi,” asema Bw Njoroge.

Mkulima huyu asema mayai ya bei rahisi kutoka nchi jirani yalikuwa yameanza kufurika katika soko na kukandamiza bei.

“Sikuweza hata kununua chakula cha kuku kutokana na uuzaji wa mayai. Kila mara nililazimika kurudi mfukoni ili kununua chakula cha kuku, kwani mapato niliyokuwa nikipata kutokana na uuzaji wa mayai hayakutosha, “alisema.

Mwisho wa mwaka 2016, Bw Njoroge anasema tayari alikuwa na wazo la kujiingiza kwenye biashara ya ufugaji wa mbwa ambayo kulingana na yeye ilikuwa haihitaji pesa nyingi.

“Baada ya kumwambia mke wangu alishtuka sana. Hakuweza kutafakari jinsi mbwa watakavyotunufaisha kwa sababu yeye pamoja na binti yangu, walikuwa wamezoea kuchinja kuku wakati wowote walipotaka kula nyama au kupika mayai, “akasema Bw Njoroge.

Anasema baadaye aliwaalika majirani kuja kununua kuku ambao waliunuliwa mara moja.

“Mwisho wa mauzo, nilikuwa nilijipatia Sh90,000. Jambo hili lilikuwa la kuvunja moyo kwa kuzingatia kwamba nilikuwa nimetumia zaidi ya Sh280,000 katika miaka hiyo miwili kwa chakula pekee,” alisema.

Bw Njoroge alianza biashara ya kuzalisha na kufuga mbwa. Leo hii, ana mbwa 19 mchanganyiko wa mbwa wakubwa na wadogo.

Kati ya mbwa anaofuga ni pamoja na wale wa German Shephard, Chihuahuas, hunters na wale wa kawaida.

Anasema kwamba yeye huuza mbwa mmoja wa Chihuahua kwa kati ya Sh25,000 na Sh30,000.

Bw Njoroge anafichua kuwa anapokea wateja wake kutoka kaunti za Nairobi, Nakuru na mji wa Nyahururu katika kaunti jirani ya Laikipia.

Asema kwamba kwa sababu ya kuongezeka kwa ukosefu wa usalama katika mji wa Ol Kalou, watu wanaotafuta kuboresha usalama nyumbani kwao pia hufurika nyumbani kwake kuwanunua mbwa wa kawaida.

Mfugaji huyo anasema kwamba hana changamoto ya kulisha wanyama hao kwani hukusanya mabaki ya chakula kutoka kwenye mikahawa katika mji wa Ol Kalou na pia kutoka kwa biashara yake ya upishi.

Changamoto ambazo anakabiliana nazo katika biashara hii ni kukosa nafasi kubwa ya kufunzia mbwa wake.

Baadhi ya mbwa maarufu nchini ni German Shephard, Rottweiler, English Springer spaniel na Labrador Retriever.

Mbwa wadogo kama vile Kimalta, Chihuaha na Pomeranian pia ni maafuru.

Bwana Njoroge anasema wakati wa kuanza mradi wa ufugaji mbwa; mtu hawapaswi kuhukumu mbwa kwa sura yake.

“Ni vizuri kuwa na ufahamu kuhusu mwenendo na tabia ya mbwa na ufanye uchunguzi wa kina kuhusu mazingira, upatikanaji wa soko na mahitaji ya kisheria kwa biashara ya ufugaji mbwa,” anasema.

Anabainisha kuwa kuna pia haja ya kuhakikisha kuwa una faili ya rekodi za mbwa wako.

You can share this post!

Mashabiki wa Spurs wamlia Mourinho kumchezesha Wanyama

AKILIMALI: Ajali haikuua ari yake, yeye sasa ni mkulima wa...

adminleo