• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Vipi Sonko alipona kimiujiza?

Vipi Sonko alipona kimiujiza?

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko alienda nyumbani moja kwa moja baada ya kuweka dhamana ya Sh15 milioni pesa taslimu mnamo Jumatano, licha ya kuwa alitarajiwa kwenda kulazwa hospitalini.

Wakati alipokuwa mahakamani, mawakili wake walimwambia Hakimu Mkuu Douglas Ogoti kwamba alikuwa mgonjwa sana na wakaomba wakubaliwe kumpeleka Hospitali ya Kiataifa ya Kenyatta (KNH) alikokuwa ameondolewa kwa ambulensi kwenda mahakamani.

“Sonko anahitaji matibabu ya dharura kwa vile ripoti kutoka KNH yasema anapasa kuwa amelazwa. Ilibidi tuwambebeleze madaktari wamruhusu gavana afike kortini kwa dakika chache asikize uamuzi wa dhamana,” Wakili Cecil Miller anayemtetea Bw Sonko katika kesi ya ubadhirifu wa Sh381 milioni aliambia Taifa Leo jana.

Lakini licha ya Hakimu Ogoti kukubali ombi lao, Bw Sonko hakupelekwa hospitalini mbali alirudishwa nyumbani mara baada ya kulipa dhamana.

“Gavana Sonko yuko nyumbani kwake sasa. Anaendelea kutumia dawa alizopewa KNH,” Bw Miller alisema.

Mnamo Jumatano, gavana huyo alifikishwa mahakamani kwa ambulensi ambayo mawakili wake waliambia korti ilikuwa inasubiri kumrudisha hospitalini.

Akiwa kortini Bw Sonko alikuwa ameweka sindano mikononi ambazo hutumiwa kumtilia mgonjwa dawa.

“Mawakili walimsindikiza Bw Sonko hadi nyumbani kwake baada ya dhamana yake ya Sh15 milioni kutiwa sahihi na Hakimu Mkuu Douglas Ogoti,” akaeleza Bw Miller.

Bw Sonko, ambaye alishtakiwa pamoja na washukiwa wengine 24, aliondolewa mahakamani kwa mwendo wa kasi na msafara wa magari yake zaidi ya manne mnamo Jumatano usiku.

Ombi la mawakili hao la kibali kuwa Bw Sonko arudishwe KNH lilikuwa mbinu ya kuzuia asikamatwe tena mara baada ya kuachiliwa kwa dhamana.

Mawakili hao walihofia kuwa polisi wangemkamata tena na kumpeleka hadi Voi kushtakiwa kwa madai ya kupigana na polisi alipokuwa akitiwa nguvuni Ijumaa iliyopita.

Baada ya uamuzi wa dhamana kutolewa, Bw Miller alimweleza Bw Ogoti: “Polisi wanamsubiri Sonko hapa nje ya mahakama kumkamata. Polisi wameizingira mahakama kwa lengo la kumkamata Sonko. Naomba uamuru gavana arudishwe KNH vile madaktari wameagiza hivyo.”

Bw Ogoti alikuwa ameshangaa kwa nini walimtoa hospitalini katika hali mbaya ya kiafya, ilhali bado angetoa uamuzi kuhusu ombi la dhamana kwa njia ya haki hata kama mshtakiwa hangekuwa mahakamani kwa sababu anaugua.

Lakini Bw Murkomen alijibu na kusema hawakutaka Bw Sonko aonekane kana kwamba anahepa kufika kortini ikitiliwa maanani inadaiwa alitoroka kifungoni alipokuwa akitibiwa hospitali ya Pwani awali.

Hakimu aliwaamuru maafisa idara ya magereza wanaomlinda Bw Sonko KNH wamrudishe Sonko hospitali endapo hatalipa dhamana aliyopewa.

Alhamisi, ilibainika Sonko alikuwa nyumbani kwake wakati wa sherehe za Jamhuri Dei zilizoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta katika uwanja wa michezo wa Nyayo, jijini Nairobi.

Hapakuwa na kiongozi yeyote wa kaunti aliyetoa hotuba ya kukaribisha wageni wakati wa hafla hizo kama ilivyo desturi.

Badala yake, Sonko alituma ujumbe wa heri kwa wakazi wa Nairobi na Wakenya kwa jumla kupitia mitandao ya kijamii.

“Jamhuri Dei hutukumbusha kuhusu nguvu za uhuru na kwa nini ni muhimu kwetu sote kupigania nafasi yetu ya haki katika jamii na maishani,” sehemu ya ujumbe huo ikasema.

Mahakama ilimpiga marufuku gavana huyo na wahusika wengine wasijadili kesi inayowakabili mitandaoni.

You can share this post!

JAMHURI DEI: Tangatanga na Kieleweke wakwaruzana Nyeri

Kuria adai BBI ina ripoti fiche

adminleo