Habari MsetoSiasa

JAMHURI DEI: Tangatanga na Kieleweke wakwaruzana Nyeri

December 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

SIASA za Tangatanga na Kieleweke zilitawala sherehe za Jamhuri Dei mjini Nyeri, madiwani walipokwaruzana na Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu.

“Wanasiasa na viongozi wengine wa kitaifa wanafaa kuwaheshimu madiwani kwa sababu tumechaguliwa na wananchi,” alisema diwani wa Wamagana, Bw Sebastian Mugo akiongea kwa niaba ya wenzake katika uwanja wa Kamukunji kulikoandaliwa sherehe hizo.

Hata hivyo, taharuki ilishuhudiwa Bw Wambugu aliponyanyuka kuhutubu huku sehemu moja ya umati ikimshangilia na wengine wakimzomea.

Bw Ngunjiri alisisitiza kwamba madiwani hao wataheshimiwa tu iwapo wao pia watawaheshimu watu wengine. Gavana wa kaunti hiyo Mutahi Kahiga alilaani fujo hizo za wiki jana.

Katika Kaunti ya Mombasa, Kamishna Gibert Kitiyo aliagiza maafisa wa usalama kukamata waganga wanaohadaa magenge ya wahalifu kwa kuwapa dawa za kulevya ili kuwasaidia kukwepa walinda usalama.

“Mkiwapata hao waganga, ambao wanadanganya vijana kuwa wanaweza kutekeleza uhalifu bila kuchukuliwa hatua, watieni mbaroni kwani wao pia ni wahalifu,” alisema Bw Kitiyo alipohutubia wananchi waliokusanyika katika uwanja wa Tononoka.

Huko Meru, Seneta Mithika Linturi alishambulia Idara ya Mahakama kwa kuwazuia magavana wanaokabiliwa na kesi za ufisadi kuingia ofisini mwao.

“Watu milioni moja hawawezi kumchagua mtu kisha umsimamishe kupitia mahakama. Hii ni sawa na mapinduzi. Baadhi ya magavana wanalengwa kwa kutotii mkondo fulani wa kisiasa,” alisema katika sherehe za Jamhuri zilizoandaliwa kwenye uwanja wa shule ya msingi ya Maua.

Katika Kaunti ya Pokot Magharibi Gavana John Lonyangapuo na Kamishna Apollo Okello walionya wanasiasa dhidi ya kumtusi Rais Uhuru Kenyatta, kwa madai kuwa aliwatekeleza waathiriwa wa mapororoko ya ardhi na mafuriko katika eneo hilo. Watu 50 waliuawa wiki tatu zilizopita.

Kwingineko Naibu Kamishna wa Naivasha Mbogo Mathioya walihimiza wakazi kuchukua vyeti vya kuzaliwa na vifo walivyokuwa wameandikisha.

“Jumla ya vyeti 16,000 vya kuzaliwa na vifo havijachukuliwa kutoka kwa idara husika,” akasema Bw Mathioya.

Wito sawa ulitolewa kule Machakos ambapo Kamishna wa Kaunti Esther Maina alihimiza wanawake kuchukulia watoto wao vyeti vya kuzaliwa.

Mjini Narok viongozi wa kisiasa wakiongozwa na Gavana Joseph Tunai walikariri kuunga mkono ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) kwa lengo la kuleta umoja nchini.

Katika Kaunti ya Kajiado uhasama kati ya Gavana Joseph Ole Lenku na Mbunge wa Kajiado Mashariki, Peris Tobiko haukuvuruga sherehe ilivyodhaniwa.

Sherehe za Jamhuri zilifanywa katika kila kaunti huku magavana wengi wakitumia fursa hiyo kueleza hatua walizopiga katika juhudi za kuleta maendeleo kwa wananchi mwaka huu.

Taarifa za REGINAH KINOGU, MISHI GONGO, CHARLES NYORO, GEORGE SAYAGIE, STANLEY NGOTHO, MACHARIA MWANGI na OSCAR KAKAI