HabariSiasa

Kuria adai BBI ina ripoti fiche

December 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NDUNG’U GACHANE Na BENSON MATHEKA

RIPOTI ya Jopo la Maridhiano (BBI), iliyozinduliwa mwezi uliopita katika ukumbi wa Bomas, Nairobi, ni tofauti na ile iliyokusudiwa kutolewa kwa umma, amedai mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria.

Mbunge huyo amesema kwamba, jopo hilo lilikuwa limependekeza Mfumo wa Utawala wa Bunge ambapo Waziri Mkuu ana mamlaka makubwa.

Hili ni kinyume na pendekezo katika ripoti iliyotolewa kwa umma ambapo Waziri Mkuu atakuwa mbunge asiye na mamlaka makuu na atakayeteuliwa na Rais na kuidhinishwa na bunge.

Kulingana naye, Waziri Mkuu angekuwa na manaibu wawili huku idadi ya maeneobunge ikiongezwa.

Anasema kuwa, Serikali inataka kubuniwa kwa nafasi za Waziri Mkuu na manaibu wake kwa kuwa haina nyadhifa zozote za kuwapa viongozi wa Upinzani waliokumbatia handisheki.

Ripoti ilidumisha maeneo bunge 290 na kaunti 47. Lakini Kuria anasema ripoti ya mwanzo iliyoandaliwa na Jopokazi hilo ilipendekeza kaunti kuwa chini ya miungano ya kimaeneo kuimarisha ugatuzi kiuchumi.

Kamati iliyosimamiwa na Seneta wa Garissa, Yusuf Haji, ilisema kaunti zihimizwe kuunda miungano ya kimaeneo kukuza uchumi kwa hiari.

Ripoti hiyo ilizinduliwa mwezi uliopita na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga katika Jumba la Bomas, jijini Nairobi.

“Wanataka nafasi za manaibu waziri mkuu kwani hawana lolote la kuwapa Mabwana Musalia Mudavadi na Kalonzo Musyoka. Nafasi za Rais, Naibu Rais na Waziri Mkuu zimetengewa Bw Odinga, Seneta Gideon Moi (Baringo) na kiongozi mmoja mwenye ushawishi katika eneo la Mlima Kenya,” Bw Kuria alisema kwenye mahojiano na Taifa Jumapili.

Kulingana na Bw Kuria, ripoti ya awali ya BBI ilipendekeza wabunge kuchaguliwa kutoka orodha maalum ya wanachama wa chama husika cha kisiasa, ili kuviwezesha vyama hivyo kudhibiti aina ya wabunge wanaochaguliwa katika maeneobunge.

Ripoti iliyozinduliwa kwa umma inapendekeza utaratibu wa kuteua wawaniaji wa vyama vya kisiasa moja kwa moja na raia. Bw Kuria anasema alipata ripoti hiyo kutoka kwa “washirika wake wa kuaminika.”

“Ripoti iliweka idadi ya watu katika eneobunge kuwa 137,000. Hilo linafikisha idadi ya maeneobunge nchini kufikia 350. Ukiongeza maeneobunge ambayo hayajafikisha idadi hiyo kwa sasa, idadi hiyo inafika maeneobunge 500. Hili linalenga kusawazisha uzito wa kila kura. Mkakati ulikuwa kutimiza Mfumo wa Utawala wa Bunge,” akasema.

Alieleza kuwa, chini ya mfumo huo, Waziri Mkuu na Rais wangechaguliwa na wabunge ili kuhakikisha Wakenya hawapigani kutokana na utata ambao huletwa na uchaguzi wa urais kila baada ya miaka mitano.

Katika ripoti iliyozinduliwa, Rais atachaguliwa moja kwa moja na raia na atakuwa na mamlaka makuu huku waziri mkuu akiteuliwa kutoka chama kilicho na idadi kubwa ya wabunge katika bunge la taifa.

Bw Kuria anadai lengo kuu la ripoti hiyo lilikuwa kuondoa nafasi za viti maalum katika mabunge ya kaunti na Seneti.

Vile vile, ilipendekeza Kilimo na Afya kurejeshwa chini ya usimamizi wa Serikali ya Kitaifa, hali ambayo ingeifanya nchi kuandaa kura ya maamuzi kulingana na Kipengele 255 cha Katiba.

Ripoti ya kamati ya Bw Haji ilipendekeza majukumu hayo yaimarishwe huku kukiwa na Tume ya Huduma ya Afya kuhakikisha kuna usawa wa wahudumu kote nchini. Bw Kuria anadai kwamba ripoti ya mwanzo ilifichwa katika hali tatanishi.