Habari Mseto

NYS kutumia mashamba yake kukuza mbegu

December 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA WAIKWA MAINA

MASHAMBA yote ya Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) yatatumika kwa upanzi wa mbegu za mimea mbalimbali hapa nchini.

Hii ni baada ya kutekelezwa kwa mradi wa majaribio wa upanzi wa viazi kwenye shamba la shirika hilo la Tumaini katika Kaunti ya Nyandarua.

Mnamo Jumamosi, mamia ya wakulima walifika shambani humo kujionea mbegu za viazi zilizokuzwa na kujifunza mengi kuhusu kilimo.

Akizungumza shambani humo, Mkurugenzi mkuu wa NYS Matilda Sakwa alisema shirika lake linaendelea kushauriana na Idara ya Kilimo ya Ukuzaji wa Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis) ambayo ilichangia ufanisi wa mradi huo wa majaribio.

“Tuna mashamba maeneo ya Turbo, Yatta, Rangwe na Mbalambala Kaskazini mwa Kenya. Tuna ekari kadhaa za ardhi ambazo tunalenga kutumia kukuza mbegu za kisasa si za viazi pekee bali hata mimea mingine kama mahindi na pamba. Ningependa kutangaza kwamba NYS sasa ni shirika ambalo limezamia miradi ya kuhakikisha kuna chakula cha kutosha nchini kwa kutoa mbegu nzuri,” akasema Bi Sakwa.

Aidha NYS itawauzia wakulima mbegu hizo kwa bei ya chini ikilinganishwa na kiwango kilichowekwa na kampuni nyingine za kuuza mbegu nchini.

Bi Sakwa alisema wakulima wengi hukosa mbegu nzuri hasa msimu wa upanzi na hilo limechangia kupungua kwa mavuno na kuweka taifa katika hatari ya raia wake kukabiliwa na njaa kila mara.

“Tunaenda kuzamia kilimo cha maua, mboga na hata matunda. NYS in ekari kadhaa za ardhi ambazo lazima zitumike kwa shughuli za kilimo. Mradi huu unaungwa mkono na Rais na washikadau wengine. Hakika NYS inajukumu kubwa la kutekeleza katika kutimiza nguzo nne kuu za serikali,” akaongeza Bi Sakwa.