Sababu ya King Kaka kuimba kibao 'Wajinga Nyinyi'
Na LEONARD ONYANGO
MWANAMUZIKI Kennedy Ombima, maarufu kama “King Kaka”, amedai maisha yake yamo hatarini, siku moja baada ya kutoa wimbo wa kushutumu wanasiasa wanafiki.
Wimbo huo wa “Wajinga Nyinyi”, umezua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii huku wengi wakimsifu kwa kuwa mkakamavu katilka kusema kweli’
Wimbo huo uliowekwa katika mtandao wa Youtube mnamo Jumamosi, Jumatatu uliendelea kuzua hisia kali huku baadhi ya Wakenya wakihimiza mapinduzi ya kiraia ili kujiokoa na wanasiasa ambao wamekuwa wakitumia vibaya wapigakura kwa masilahi yao ya kibinafsi.
Kupitia kwa kaulimbiu #RevolutionNow (mapinduzi ni sasa), waliochangia walisema wimbo huo umezindua wapigakura ili wawe wakichagua viongozi kwa busara.
Katika wimbo wake, King Kaka, anazungumzia kuhusu ufisadi ambao umekita mizizi katika jamii ambapo wapigakura wanawachagua ‘wezi’ wanaopora fedha zao za ushuru.
Msanii huyo pia anashambulia Wakenya kwa kwa kuwa na chuki kwa msingi wa kikabila.
“Wimbo huo umesuta kila Mkenya – matajiri kwa maskini, wafisadi na wapigakura wanaochagua viongozi kwa misingi ya kikabila. Mapinduzi ni sasa,” akasema Mash Bismark kupitia mtandao wa Twitter.
“Mapinduzi yaja na tuko tayari,” akasema Stephen Ochieng.
Mkurugenzi wa Bodi ya Kutathmini Filamu nchini (KFCB), Ezekiel Mutua amempongeza King Kaka kwa wimbo huo.
Kulingana na Dkt Mutua, watu wanaohisi kwamba wamekerwa na wimbo huo waende mahakamani akisisitiza bodi yake haitaagiza uondolewe YouTube.
Saa chache baada ya kuweka wimbo huo King Kaka aliomba ulinzi akidai kuwa amepokea vitisho kutoka kwa wanasiasa ambao hakuwataja.
Wimbo huo, hata hivyo, ungali kwenye Youtube na umetazamwa mara 700,000.
Wimbo huo ndio umetazamwa na kusikilizwa zaidi katika mtandao wa Youtube kwa siku mbili zilizopita.
Idadi kubwa ya Wakenya wanakubaliana na maoni ya msanii huyo.